Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Karibu Awamu ya Nane Zanzibar

5bd090fe5557e6b0f4b218fc442e4db0 Karibu Awamu ya Nane Zanzibar

Tue, 3 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

DAKTARI wa binadamu, Hussein Ali Mwinyi jana aliapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

Dk Mwinyi anaingia madarakani kuchukua nafasi ya daktari mwingine wa binadamu, Ali Mohamed Shein ambaye muhula wake wa pili wa urais wa Zanzibar umekamilika jana kikatiba, na hivyo kukamilisha uongozi wake wa awamu ya saba ulioanza Novemba 3, 2010.

Chini ya uongozi wa Dk Shein, Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya kimaendeleo katika mihula yake miwili ya uongozi, akibadilisha kwa kiasi kikubwa hali za maisha za watu, lakini pia akisogeza mbele maendeleo katika sekta mbali mbali za kijamii na kiuchumi, kiasi cha kuifanya Zanzibar iwe inasonga mbele kwa kasi.

Tunampongeza Dk Shein kwa kazi nzuri aliyowatendea Wazanzibari kwa miaka yake 10 na tunaamini historia ya Zanzibar itakapoandikwa, atakuwa miongoni mwa viongozi watakaoandikwa kwa wino wa dhahabu.

Kuanzia jana Novemba 2, 2020, Dk Mwinyi amekabidhiwa kijiti cha kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake na kutokana na ukweli kuwa rais huyu pia anatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ataendeleza yote mazuri yaliyoanzishwa na kutekelezwa na mtangulizi wake huyo Dk Shein.

Kama ilivyokuwa kwa Dk Shein, Dk Mwinyi ameinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambayo ndio itakuwa dira yake ya kumuongoza katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar, hivyo hakuna shaka kuwa ataitumia vyema katika kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa zaidi.

Kama alivyoeleza jana katika hotuba yake fupi baada ya kuapishwa, kuwa serikali yake atakayoiunda itakuwa makini, yenye uadilifu na kasi ya kuleta maendeleo huku ikiongozwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na Dira ya Maendeleo 2050, ni uthibitisho tosha kuwa amedhamiria kuwaongoza vyema Wazanzibari na wote kwa ujumla.

Si hilo tu, pia ameahidi kuwa anataka kuona kila mtu anafaidika na rasilimali zinazopatikana nchini, kwa serikali yake mpya itazingatia usawa na uwezo wa mtu kufanya kazi bila ya kuangalia mtu anatoka wapi.

Kwetu sisi hizi ni kauli zenye kuonesha matumaini makubwa kwa kiongozi huyu mpya wa Zanzibar na hakuna shaka atatekeleza haya yote kwa vitendo, na hasa ikizingatiwa rekodi yake nzuri katika maeneo mbali mbali ambayo aliaminiwa na kupewa kazi ya kuongoza, zikiwamo wizara nyeti katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tunamtakia kila la heri Dk Mwinyi pamoja na serikali yake atakayounda hivi karibuni, tukiamini yale yote yaliyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na ahadi zake binafsi katika kampeni, zitatekelezwa kwa maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar ili visiwa hivyo viendelee kupiga kasi ya maendeleo.

Columnist: habarileo.co.tz