Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kapombe, Tshabalala wanavyopima upeo wetu wa kufikiri

Kapombe Na Tshabalala Mohamed Hussein Kapombe, Tshabalala wanavyopima upeo wetu wa kufikiri

Wed, 27 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Watanzania bwana. Watu wa ajabu kidogo. Kaa chini ujaribu kuwafikiria pindi suala la mabeki wawili wa pembeni wa Simba linapowekwa mezani. Inachekesha kidogo. Tusianzie mbali. Tuanzie mwishoni mwa msimu uliopita.

Kocha wa Timu ya Taifa, Adel Amrouche aliwaacha mastaa hawa katika kikosi ambacho kingekwenda kucheza na Uganda pale Ismailia, Misri katika pambano la kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika. Zilipigwa kelele nyingi zilizopitiliza.

Kwamba Amrouche alikuwa ameacha nchini mabeki bora zaidi wa pembeni nchini. Bahati nzuri ni kwamba Taifa Stars ilishinda bao 1-0 kupitia kwa Saimon Msuva. Ni bao ambalo kwa kiasi kikubwa lilimuokoa Amrouche kutoka katika lawama. Kama tungepoteza basi ingeonekana tumepoteza kwa sababu Kapombe na Tshabalala wameachwa.

Novatus Dismas alikwenda kucheza kushoto wakati Dickson Job alicheza kulia. Mambo yalikwenda sawa. Kelele zikazimwa. Mechi ya marudiano Taifa Stars ikakubali kichapo cha bao moja pale Temeke katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Mashabiki waliamua kukaa kimya kwa sababu Kapombe na Tshabalala waliitwa katika mechi hii na wakacheza.

Hali ilikuwa shwari. Mwanzoni mwa msimu huu Simba haikuonekana kurudi vema uwanjani kama ambavyo ilikuwa imetabiriwa baada ya kukosa chochote kwa misimu miwili. Baadaye timu ya taifa ikaitwa kwa ajili ya pambano dhidi ya Algeria pale Afrika Kaskazini.

Ilisikika tu minong’ono ya hapa na pale baada ya Kocha Amrouche kuwaacha tena nje ya kikosi Kapombe na Tshabalala. Tulisafiri kwenda Algeria kukiwa hakuna matumaini ya Stars kufuzu kwenda katika fainali za mataifa ya Afrika kule Ivory Coast mwakani.

Wachezaji wa Stars walipambana wakapata suluhu. Kama ilivyokuwa pale Misri, Amrouche alimchezesha Novatus kushoto halafu kulia akampanga Job. Mechi ilipoisha wachezaji wote wa Taifa Stars wakaibuka mashujaa. Ilimsaidia Amrouche kwa kiasi kikubwa. Watanzania hawa hawa wangemgeuka Amrouche na kumuhoji kwanini amewaacha Kapombe na Tshabalala. Kuna watu wangehoji “Unakwendaje kujaribu kufuzu kule Algeria ukiwa umewaacha Kapombe na Tshabalala nyumbani? Huyu kocha vipi jamani?” Huu ndio ukinyonga wa Watanzania.

Wangeenda mbali zaidi kwa kumuhoji Amrouche kwanini alimuacha Fei Toto. Fei ambaye alikuwa amefunga mabao matatu ndani ya dakika 20 katika pambano la Ligi kuu lililovunjika dhidi ya Kitayosce pale Mbagala. Ni vile tu Stars ilifuzu ndio maana hatukusikia tena kelele za Fei, Kapombe na Tshabalala. Unawajua Watanzania au unawafahamu?

Kukawa na mambo mawili. Kwanza kabisa ilionekana Stars inaweza kucheza kibabe bila ya Tshabalala na Kapombe. Tuliwaimba zaidi kina Nova. Lakini pili hapa nyumbani Simba haikuwa katika ile kasi yake ya kawaida. Hapo tukaunganisha haya mambo mawili na kupata jibu moja la uongo tu kwamba Kapombe na Tshabalala wamechoka.

Tukaamua pia kuhalalisha jibu letu kwa kuangalia namna ambavyo watani walikuwa wanatambia sana viwango vyao vya mebeki wao. Yao Kouassi wa Yanga alionekana moto katika upande wa kulia akiziba nafasi ya Shaban Djuma, wakati Joyce Lomalisa alionekana moto upande wa kushoto. Iliongeza kelele kutoka kwa mashabiki wa Simba kwamba Kapombe na Tshabalala wamechoka.

Hii ndio kawaida yetu. Kila kitu tunachunguliana. Ni kama Simba iliposhinda mabao matatu kwa bila wiki iliyopita dhidj ya Coastal Union lakini mashabiki hawakuridhika. Kisa? Hapo nyuma tayari Yanga ameshinda mabao matano kwa takribani mechi tatu mfululizo. Kama Simba angefikisha idadi ya mabao matano basi hali ingekuwa shwari. Kila kitu ni lazima tufanane.

Hizi kelele za Kapombe na Tshabalala kuchoka zilinishangaza. Ni Tanzania pekee ndipo mchezaji anaweza kuisha ghafla au kuchoka ghafla. Hii ni kwa mujibu wa mashabiki. Simba kukosa mwendo wa uhakika ukijumlisha Stars kufuzu kwenda Afcon bila ya Tshabalala na Kapombe kuwa uwanjani kuliongeza moto wa madai ya kwamba wamekwisha.

Mchezaji kama Tshabalala anawezaje kuisha ghafla baada ya kutoka katika msimu mzuri uliopita akiwa amesaidia kutengeneza mabao mengi ya Simba? Hii huwa inatokea Tanzania tu. Shomari alikuwa na mwendo lakini hakuwa bora zaidi ya Tshabalala. Wote wawili hakuna aliyechoka wala aliyekwisha. Lakini pia tukumbuke kiasili mabeki wa pembeni wanaoshambulia zaidi huwa wanakuwa na wakati mgumu kama timu zao hazikai na mpira kwa muda mrefu au kutawala mechi kwa ujumla. Mara nyingi wanajikuta katika jukumu kubwa la kukaba kuliko kushambulia. Na wakati mwingine ndipo unapogundua wana udhaifu katika eneo la ukabaji kama hawasaidiwi.

Majuzi tu Simba walikuwa wameikamata mechi katika pambano dhidi ya Coastal Union na Tshabalala alipika bao la pili la Jean Baleke. Hivi ndivyo mabeki wa pembeni wanavyofurahia mechi. Sio tu kwa Tanzania, bali hata Ulaya kuna wachezaji wengi wa pembeni waliobebwa na ubora wa timu zao.

Dani Alves asingekuwa anahemea lango la adui kila mara kama Barcelona ingekuwa mbovu. Uhodari wake wa kupanda na kushambulia ulitokana na timu yake kupeleka mashambulizi mbele kwa muda mrefu zaidi. Hivyo hivyo kwa kina Roberto Carlos na wengineo. Ukiangalia mabeki wengi bora wa pembeni waliotamba Ulaya ni wale ambao timu zao zilikuwa zinashambulia zaidi.

Kama wote tunahafikiana Simba haijafikia kiwango cha juu cha moto wake itakuwa ngumu kwa Tshabalala na Kapombe kuwika kwa sababu aina yao ya mchezo inashehereheshwa zaidi na mchezo wa kushambulia na kumiliki mchezo. Wachezaji wazuri huwa hawaishi ghafla kama tunavyolazimisha.

Kitu kingine ambacho kimezua balaa hili la kudai Kapombe na Tshabalala wamechoka ni inatokana pia na Simba kuchungulia kwa jirani na kuona mabeki wao wanavyobadilika mara kwa mara. Kuanzia msimu uliopita Yanga imekuwa ikibadilisha wachezaji wengi uwanjani kutokana na kukaribiana kwa viwango kwa wachezaji wake.

Djuma angeweza kuwa nje halafu Shomari Kibwana akaanza. Msimu huu tumeona Nickson Kibabage akianza badala ya Lomalisa. Tatizo kubwa kwa Simba kuna pengo kubwa la kiuwezo kati ya wachezaji wanaoanza na wale wa benchi. Siamini kama mashabiki wa Simba watatulia vitini kama mechi dhidi ya Power Dynamo kulia akianza David Kameta ‘Duchu’ na kushoto akiwa ameanza Israel Mwenda. Hapa ndipo tunapojaribu kuficha unafiki wetu wakati ukweli tunaufahamu.

Columnist: Mwanaspoti