Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kama zali, kutoka mtaani hadi Ulaya

Kama Zali Ulaya Kama zali, kutoka mtaani hadi Ulaya

Tue, 11 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yale ambayo yamekuwa yakifanyika kwa wingi kwenye mataifa ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika, yameanza kushika kasi Tanzania na huenda miaka michache ijayo kikosi cha timu yetu ya taifa ‘Taifa Stars’ kikasheheni idadi kubwa zaidi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Ulaya.

Vikosi vya wenzetu vimekuwa vikisheheni nyota kutoka Liverpool, Manchester City, Chelsea, Arsenal, Barcelona, Bayern Munich, Inter Milan, PSG na klabu nyingine kubwa barani Ulaya, yote hiyo ni kutokana na misingi wameyojiwekea ndiyo maana nguvu yao ya ushindani inaonekana kuwa kubwa.

Kuanzia leo, Jumatatu zaidi ya wachezaji 10 wa Kitanzania mmoja baada ya mwingine watapanda ndege kwenda kwenye akademi za klabu mbalimbali barani Ulaya, hayo ni matokeao ya utafutwaji vipaji ambao ulifanywa kwa zaidi ya wiki tatu kuanzia Tanzania Bara hadi Visiwani Zanzibar na taasisi ya African Youth Empowerment (AYE).

Maskauti kutoka Ulaya waliweka kambi nchini na kuzunguka mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo, Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Muyimba Gerald anasema; “Kila kitu kimeenda vizuri katika awamu yetu ya kwanza ya utafutaji wa vipaji ambayo ilienda kwa kaulimbiu yetu ya ‘nyota ajae ni wewe’, tumepata zaidi ya vijana 10.”

“Mmoja ataanza safari kesho (leo) ambaye ni Haroun Ally tumempata kwenye skauti ya Dar es Salaam, huyu ataenda moja kwa moja Antalyaspor inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki, tunaimani atafanya vizuri huko na kuwa balozi mzuri wa vipaji ambayo vipo Tanzania.”

Muyimba anasema nyota wengine ambao wataenda Uturuki ni Revocatus James ‘Dyabala’ ambaye amechanguliwa kutoka Morogoro kwenye uwanja wa Jamhuri, Buruhani Kenith Akimu kutoka Kagera Wilaya Missenyi,

Matheo Emmanuel Kayanda mwenye miaka 12 anaenda Olympiakos ya Ugiriki ametolewa Kilimanjaro Wilaya Moshi mtaa wa Bonite, Osman Iddy Salum mwenye miaka 15 anaenda Uturuki pamoja na Nassoro Salum Said kutoka Tegeta na Mohammed Issa kutoka Zanzibar.

Nassoro Mbarouk anaenda Moldova, Laurent Haji anaenda Romania, Salum Abubakar, Hassan Abubakar, Adrian Ambros nao Uturuki.

“Wataenda kwa awamu lakini ndani ya wiki chache zijazo kila mmoja atakuwa ameanza safari ya kutimiza ndoto zake, kazi yetu ni kuwashika mikono vijana na nafasi zipo nyingi ishu ni kupata vipaji ambavyo tunaona vinaweza kukubalika,” anasema mkurugenzi huyo na kuongeza;

“Kati ya wachezaji ambao tumewachagua kwenye awamu hii ya kwanza kwa mwaka huu, yupo wa miaka 12 huyo ni hatari sana, watu wanapaswa kushika maneno yangu huko ambako anaenda (Ugiriki) atapata pia nafasi ya kuendelezwa kimasomo na kipaji chake anaweza kuwa tishio kwa baadae.”

Sehemu ya pili na mwisho kwa mwaka huu kwa mujibu wa Muyimba katika mchakato wao wa kusaka nyota ajae itakuwa mwishoni mwa mwaka na wamepanga kuifanya kwa ukubwa zaidi hasa maeneo ya vijijini.

“Vijijini wapo wachezaji wengi wazuri hivyo tumepanga nao kuwafikia, kipekee niwashukuru wote ambao wamekuwa sehemu ya kufanikisha zoezi letu kwenye awamu ya kwanza, kila tulipokuwa tukitembelea vyama vya soka vya mikoa vilikuwa vikitupa ushirikiano mkubwa sana,” anasema.

Kwa upande wake, Firat Totik ambaye ni mmoja wa maskauti waliokuwa sehemu ya utafutaji huo vipaji nchi nzima, anaeleza namna ambavyo Tanzania imebarikiwa kuwa na vipaji na inaweza kuwa moja ya mataifa tishio.

“Nimezunguka mataifa mengi Afrika nimegundua Tanzania ni moja ya mataifa yaliyobarikiwa vipaji vikubwa vya soka, nakumbuka miaka iliyopita tulimpata Shaffih (Omary) na amekuwa akisifiwa huko Uturuki tulikompeleka,” anasema na kuongeza;

“Tutaendelea kuona namna ya kuwasaidia kwa sababu hakuna klabu ambayo inaweza kumkataa kijana mwenye kipaji, Ulaya klabu zipo nyingi na kama anapatikana mwenye maajabu zaidi anaweza kwenda kwenye klabu kubwa zaidi, nimefurahi kuwa hapa hadi wakati mwingine.”

Haroun ambaye ameondoka leo na kwenda kujiunga na Antalyaspor inayoshikiri Ligi Kuu Uturuki, anasema, “Nashukuru sana kwa nafasi niliyoipata, nitajitahidi kuwa msikivu na kupambana kadiri nitakavyoweza ili kufikia malengo yangu ya kucheza soka la kulipwa kwenye klabu kubwa zaidi Ulaya.”

Columnist: Mwanaspoti