Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kabla ya Manara alikuwepo Mchungaji Mtikila...

Elizabeth Michael Elizabeth Michael 'Lulu'

Sun, 21 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Ustaa tangu utotoni una majaribu mengi sana. Ni vigumu sana mtoto mdogo maarufu mwenye pesa na kupendwa sana, kutuliza akili ya maisha. Wengi hupotezwa na kuzuzuka.

Watu watakuzoea kwa utoto wako. Kuhama nao kwenye utu uzima, uwe na kitu cha ziada. Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliweza. Alipendwa utoto hadi sasa akiwa mtu mzima. Na katulia vizuri.

Alichofanya Lulu ni ‘kujibrandi’ upya, toka taswira mbaya mpaka njema. Yale aliyofanya kabla, yakatufanya tuamini yalikuwa makuzi ya utoto. Ni kama kibaka aliyegeuka malaika.

Leo, yuko juu kama theluji ya Mlima Kilimanjaro. Alibadilika jumla baada ya mitihani mingi. Akafuata misingi ya binti wa Kiafrika ili kubaki njia kuu. Huwezi kuwa pisi kali kama huna akili mkichwa.

Leo ana mpangilio mzuri wa maisha kuliko mastaa kibao. Alirudi ‘skonga’ kwa imani kuwa huko ndiko iliko njia sahihi ya kutoboa kimaisha. Maisha ya kutegemea kamera, alijua yana njia chafu na fupi kimaisha.

Leo Paula akizingua shule. Akizingua kwa ‘mshua’ akiwa bado kinda. Yeye siyo wa kwanza, kuna Lulu, alizingua ‘bigi taimu’. Dunia ilipomuelemea tu fasta akarudi njia kuu. Mtazame leo yuko wapi?

Miaka ya 2000 mwanzoni. Hili jiji la Dar es Salaam lilitawaliwa na watu wawili kwenye dansi. Ally Choki na Banza Stone (RIP). Walikuwa ni wao tu. Walipigana madongo ya kila aina.

Wakawa maarufu, wakapata watu na pesa. Walipounda kaumoja f’lani hivi, stori ya upinzani wao ikaishia hapo. Waliendelea kutupa nyimbo nzuri lakini mzuka wake kwa mashabiki wao ukatoweka.

Kinondoni ilikuwa chini yao. Bongo nzima na Afrika Mashariki, miamba hii ilitamba kwenye dansi. Leo hii ukiona Mbosso na Aslay wanaleta kwere mjini tambua kulikuwa na baba zao.

Dudu na Nice, walienda mbele zaidi kiupinzani. Wakatwangana mitama ‘amazing’ jukwaani. Hawakuwa na muziki mzuri wa kuzidi wenzao. Ila walikuwa ndiyo kila kitu.

Magazeti yaliwapamba. Vipindi vya radio vikafunga nao ndoa isiyo rasmi. Waliongelewa wao tu. Wakapata pesa za kununulia Balloon na kukaa kwenye viti virefu. Walikuwa juu kinoma na pesa nyingi walipata.

‘Vita’ ya Dudubaya na Mr Nice, ni vigumu kuielezea chanzo chake. Hata wao hawajawahi kuweka wazi chanzo cha ‘bifu’ lao. Tunaweza sisi wenyewe kuchagua, kwamba ilikuwa ujinga na ujana.

Leo Kiba na Mondi, wasikupe wenge kwa ‘bifu’ lisilokuwa na kichwa wala miguu. Walikuwepo Dudubaya na Mr Nice, waliopata pesa, mashabiki na walichukiana.

Ndivyo ilivyokuwa kwa ‘bishoo’ wa Ilala Dully Sykes na ‘muhuni’ wa Kinondoni TID. Nao walikuwa kama wamekodisha akili za mashabiki wa muziki. Walikuwa na uwezo mkubwa wa kuimba na kucheza.

Wenye kutaka pesa za haraka haraka wakawapa jukwaa moja. Baada ya kugawana pesa za viingilio upinzani wao ukatoweka ghafla. Hii ya Dully na TID, pia hakukuwa na msingi wa chanzo cha ‘bifu’ lao.

Walichokuwa wanafanya mashabiki ni kuwalinganisha. Nani ni mkali wa kumiliki jukwaa pindi wafanyapo shoo. Na wao wakaamua kuwekana katika mazingira ya ‘bifu’ ili kupiga pesa.

Leo Konde na Vanboy wakizinguana puuzia. Kuna kaka zao walipiga pesa, walidaka pisi kali tena zile ‘klasiki’. Wao wakiwa bado ni madogo sana huko Nzovwe na Newala. Leo haya wanarudia yale yale.

Juma Nature na Inspector Haroun Babu. Bonge moja la ‘bato’ la watoto wa uswahilini. Waliiteka Temeke, Dar es Salaam na Tanzania yote. Mizuka ya uswahilini Kurasini na ‘swaga’ za uswazi Temeke Mikoroshini.

Zikavuka ukuta wa tabaka la wenye nacho na wasio nacho. Osterbay na Masaki waliwajua hawa ‘masela’. Kila mtoto alitamani kuingia studio. Au kuwashika mkono Nature au Babu.

Wakapiga shoo pamoja. Bonge moja la tukio. Dar es Salaam ilisimama.

Diamond Jubilee ilitapika mpaka ukuta kuvunjwa na mashabiki. Huku wakishirikiana kwenye wimbo wa ‘Mzee wa Busara’ remix.

Walikuwa juu kuliko Bongofleva yenyewe. Utafanyaje shoo bila Nature? Utatoaje ‘singo’ bila sauti ya Inspector? Baada ya ‘Ugali’ stori za Kibra na Babu zikateketea.

Hazikuhitajika tena. Vita ikawa TMK na watoto wa Upanga. Unakumbuka vurugu za ‘Wajivuni’ East Coast Team kutoka Upanga na ‘Manunda’ wa TMK? Muda haujawahi kuwa na mahaba na binadamu.

Muda unapita tunabaki na simulizi tu. Mashabiki hawaangalii tena ubora wa muziki, wao huangalia nani zaidi.

Kuanzia kuvaa, shoo, tuzo, kusafiri na kumiliki msichana mzuri. Lakini ule ufundi wa kimuziki hupuuzwa.

Leo Kiba na Diamond, huwezi kuona wakiwa pamoja. Wana ‘bifu’ ambalo halina miguu wala kichwa. Imefikia hatua kwenye tuzo za ndani na nje wanawazwa wao tu. Utadhani hakuna wanamuziki wengine.

Ben Pol na wenzake ni wahanga wa upinzani wa kishabiki kwa wawili hawa. Hawatazamwi kwa jicho lilelile wanalotazamwa Kiba na ‘Dai’. Ni kama wamelimeza jukwaa la muziki wetu.

Wameweka ukuta mrefu kati yao na wanamuziki wengine. Ni Dangote na Kiba tu. Wapo wanamuziki wengine nao wamekuwa mashabiki sasa na wanawaangalia wao. Nao hufanya kitu ili kumzidi mwenzake.

Lakini kabla ya Kiba na Mondi, kuna Khadija Kopa na marehemu Nasma Khamis Kidogo. Upinzani wao uliifanya taarabu ipae juu. Kabla ya kukumbwa na dhoruba la Bongofleva.

Kwa waliobahatika kuwepo enzi za Nasma na Khadija. Hawawezi kuona ajabu hili la Mondi na Kiba. Mambo wanayofanya yanajirudi yaliyofanywa ama na kaka zao, au mama zao hawa.

Kuna stori ya mmiliki wa gazeti moja miaka ya 90. Baada ya kukosa stori akamtafuta Mchungaji Christopher Mtikila. Ilikuwa ni mwanzoni mwa utawala wa Benjamin Mkapa.

Gazeti kesho yake likapambwa na kichwa cha habari cha, “Mtikila Asema Nyerere Anyongwe”. Saa mbili asubuhi, ‘difenda’ ya mapolisi ikawa mlangoni ofisini kwao.

Bosi akajificha na kuacha msala kwa wafanyakazi wake. Wale polisi nao walipomkosa mmiliki wakaagiza mmiliki au mhariri wao afike kituoni haraka sana. Kisha wakaondoka zao.

Mhariri, akaitikia wito na kwenda kituoni. Akakaa ndani akisubiriwa Mtikila. Naye Mtikila alifika haraka polisi, na polisi wakamuonyesha lile gazeti. Aliposoma alikana kusema lile neno.

Akisema. “Mimi sikusema Nyerere anyongwe, mimi nilisema Nyerere anyongwe hadi kufa.” Hapo hapo wale polisi wakamuachia yule mhariri wakabaki na Mtikila.

Mchungaji Christopher Mtikila, ni mwanasiasa, mwanaharakati. Na kiongozi wa dini ambaye kwa kauli au matendo yake, alijikuta akijenga urafiki wa kudumu na vituo vya polisi na korido za Mahakama.

Alikuwa mtata sana kwa siasa zake. Leo hii kauli na matukio ya Manara, hakuna jambo geni tena. Kuna mstari mwembamba sana unaomtofautisha Manara na Mtikila. Ni yale yale.

Columnist: Mwananchi