Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KYOMBO: Nilisaini Singida, nikaitamani Simba...kutua Yanga iko hivi

Kyombo Bbo KYOMBO: Nilisaini Singida, nikaitamani Simba...kutua Yanga iko hivi

Mon, 29 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Habibu Haji Kyombo ni miongoni mwa usajili ambao uligusa wapenzi wengi wa soka nchini kutokana na utambulisho wake kwenye klabu ya Singida Big Stars.

Kabla ya utambulisho huo gazeti hili lilikupatia taarifa ya Kyombo kusaini Simba miaka miwili ingawa kuna wengi ambao walibisha na kupinga ila mwishowe Simba walikuja kumtambulisha kama nyota wao mpya.

Kyombo anasema ni kweli alianza kusaini Singida ila siku chache baadae alipata fursa kubwa na Simba ilionyesha nia ya kumtaka na ilikuwa ngumu kuachana nayo.

“Nilikaa chini na viongozi wa Singida na walikubaliana na mimi kwenda kucheza Simba ila kwa kufuata utaratibu wa kuwapatia zile stahiki zao ambazo walinipa hapo awali ambazo kwangu hazikuwa shida baada ya maelewano,” anasema Kyombo na kuongeza;

“Niwapongeze Mwanaspoti mmekuwa wa kwanza kufahamu ukweli wangu wa kusaini Simba hata yalipotokea maneno mengine wala hamkuondoka katika ukweli wenu na hitamaye sasa nacheza hapa.”

Mwanaspoti lilifanya mahojiano maalumu na Kyombo na amefunguka mambo mbalimbali ikiwemo malengo yake akiwa Simba, huku akiwaomba mashabiki wa timu hiyo wawe pamoja katika vipindi vyote ambavyo watakutana navyo vigumu na vile vya furaha.

MAISHA YA MPIRA

Kyombo anasema maisha ya soka yalianzia kwenye Academy ya BQ ipo Mbezi Beach Makonde, kabla ya kwenda Villa Squad, Kinondoni FC na baadaye timu ya vijana ya Simba ingawa hawakaumsajili.

Anasema hakumbuki ni mwaka gani ila sababu ya kutosajiliwa na Simba B, ni baada ya kupata timu nyingine, Lipuli FC iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja La Kwanza.

“Lipuli nilicheza nusu msimu ila kuna kaka yangu mmoja wa mtaani, Faraji Henzo ambaye kwa sasa hivi ndio Meneja wa KMC, alinipigia simu, amesikia habari zangu nikiwa na Lipuli,” anasema Kyombo na kuongeza;

“Wakati huo Henzo alikuwa Meneja wa Mbao FC, aliniita Mwanza kwenda kufanya majaribio chini ya Kocha Ettiene Ndayiragije ambaye alinikubali na kunichukua katika timu yake,” anasema Kyombo.

“Chini ya Ndayiragije ndani ya mwaka mmoja nikiwa Mbao FC nilifanya vizuri msimu wangu wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara hadi kupata fursa katika sehemu nyingine,” anasema Kyombo ambaye alijiunga na Singida United kabla ya kupata nafasi ya kufanya majaribio soka la kulipwa Afrika Kusini kwenye klabu kubwa Mamelodi Sundowns na kuchukuliwa na timu hiyo.

“Baada ya kufanikiwa walishindwa kunisajili kwa sababu dirisha la usajili lilikuwa bado halijafunguliwa nchini huko na hivyo, nilirudi Tanzania kusubiri litakapofunguliwa.”

“Bahati mbaya nikiwa Singida United ili kumalizia msimu, niliumia goti katika mechi kubwa dhidi ya Simba na nilihisi ni jeraha dogo. Niliporudi Mamelodi katika mazoezi niligusa mipira mitatu tu na kushtua tena jeraha langu la goti,” anasema Kyombo ambaye alilazimika kukaa nje kwa miaka miwili kutokana na jeraha hilo baada ya upasuaji na madaktari wa Mamelodi na klabu hiyo ilimgharimia mahitaji yake yote akiwa huko hadi alipopona.

“Baada ya kupona sikupata nafasi ya kucheza na niliomba kurudi Tanzania,” anasema na kuongeza;

“Nakumbuka mkataba wangu ulikuwa unakaribia kuisha na walitaka kuniongeza mwingine ila kwa upande wa masilahi haukuwa mzuri, ikanibidi kurudi Tanzania kujiunga na Mbeya Kwanza ingawa kuna timu nyingine zaidi ya nne zilikuwa zikinihitaji.”

KWA NINI MBEYA KWANZA?

“Niliamua kwenda Mbeya Kwanza licha ya udogo wake na ugeni katika ligi. Kwanza niliamini nitapata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na timu nyingine ingawa ningeweza kucheza zaidi,” anasema kuongeza;

“Mwenye timu ya Mbeya Kwanza alikuwa kama kaka yangu kwa jinsi tulivyokuwa tunafahamiana pamoja na ukaribu wetu kwani ni kaka yake na Eliuta Mpope kwa hiyo ilikuwa ngumu kumkatalia,” anasema Kyombo ambaye alimaliza msimu akiwa na mabao sita na asisti moja ya bao na kuongeza, licha ya mazingira magumu alijiamini na kujituma na amekuwa akifanya hivyo katika timu nyingi alizopita.

“Siwezi kuacha kutaja ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu ni miongoni mwa vitu vilivyo changia kufikia ubora huo hadi Simba kuvutiwa na kunisajili.”

MBEYA KWANZA KUSHUKA

Kyombo anasema ni mara yake ya kwanza kukutana na changamoto ya kucheza timu ambayo inakwenda kushuka daraja, ingawa alienda kwenye timu ikiwa katika hali mbaya ndio maana alipambana kutoa mchango wa kutosha.

“Kiukweli watu wa huku nje hawafahamu wachezaji ndani tulikuwa tunaumia kutokana na matokeo mabaya kiasi, tulikuwa hadi chakula tunashindwa kula ingawa kiliandaliwa vizuri na uongozi wetu.”

“Kushusha timu si kitu rahisi watu wengi walikuwa wananiangalia kama kiongozi kimsingi ilikuwa ni mwaka mbaya kutokana na jambo hilo ila kwa binafsi ulikuwa mzuri baada ya kusajili na timu kubwa nchini.”

KUZIFUNGA SIMBA, YANGA

Rekodi zinaonyesha Kyombo aliwahi kuifunga bao Simba Septemba 21, 2017 na hakuishia hapo aliwahi kuifunga Yanga katika mchezo wa Ligi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Kyombo anasema kila mchezo huwa anafanya maandalizi ya kitimu pamoja na yale binafsi ili kuhakikisha wanafanya vizuri.

“Watu wengi huwa hawafuatilii mechi nyingine tofauti na zile za Simba, Yanga na Azam ila nimekuwa nikifanya vizuri na kufunga mabao mazuri katika michezo mingine,” anasema Kyombo na kuongeza;

“Unajua kuzifunga Simba na Yanga kuna raha yake lakini unajiweka mazingira mazuri ya kibiashara kama mchezaji, ndio maana kila nilipokuwa nakutana nao nilitolea macho mchezo huo na kutamani kuwafunga.”

“Nashukuru Mungu nimefanikiwa kuwafunga Simba na Yanga pengine ni moja ya njia ya kunirahisishia katika mafanikio haya madogo niliyo yapata na kama ikitokea nafasi ya kufunga katika mechi yoyote bila ya kuangalia Yanga, Azam, timu nyingine nitafunga.”

SIMBA TIMU KUBWA

Anasema siku ya kwanza aliyopewa taarifa ya kuhitajika na Simba na siku aliyotambulishwa kama mchezaji mpya wa kikosi hicho zilikuwa zenye furaha kwake.

“Simba ni timu kubwa ambayo kila mchezaji kwenye ligi yetu ya Tanzania ndoto zake ni kuitumikia timu ya daraja kama hilo alilipo wakati huu au zaidi na alipokea vizuri, kwa furaha na jambo jema kwake,”

“Nimesaini Simba mkataba wa miaka miwili na mbali ya ukubwa wa timu unajua falsafa ya timu hii ni kucheza na mimi ambacho napenda ni staili hiyo ndio maana nilivutiwa kutoka kwao naamini nitakwenda kufanya vizuri.”

KUTUA YANGA

Kyombo anasema kabla ya kufuatwa na Simba kuzungumza masuala ya kumsajili Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kuwasiliana naye na aliongea na mmoja wa viongozi wa juu kwa sasa ndani ya klabu hiyo.

“Tulifanya mazungumzo vizuri na kuna nyakati hadi tulionana na niliamini kabla ya msimu uliopita kumalizika nitasaini klabu hiyo na msimu ujao kwenda kuitumikia,” anasema Kyombo na kuongeza;

“Ila nilishangaa walikaa kimya na kukata ghafla mawasiliano ambayo yalifikia hatua nzuri na hapo Simba ndio walikuja na kuonyesha nia ya dhati tena wakiwa na kila kitu ambacho nilihitaji kutoka kwao.”

“Nilikubali kusaini Simba kutokana na kila kitu ambacho walikuwa wanahitaji walinipatia kwa wakati ilikuwa ngumu kuacha nafasi kubwa kama hii katika maisha yangu.”

MASHINDANO NDANI, NJE

Msimu uliopita Simba haikufanya vizuri katika mashindano ya ndani walipoteza mataji matatu, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) pamoja na Ngao ya Jamii walifungwa bao 1-0, dhidi ya Yanga.

Kyombo anasema kuhusu hilo mpira ni historia ambayo imewekwa kwa ajili ya kuvunjwa yale ya msimu ujao yamepita na sasa wanakwenda kuangalia kilichokuwa mbele yao kwa sasa.

“Siri kubwa msimu huu ambao utafunguliwa Jumamosi timu ambayo itakuwa imefanya maandalizi ya kutosha na kujiandaa vizuri ndio itafanikiwa kufanya vizuri katika mashindano yote ya ndani,” anasema Kyombo na kuongeza;

“Katika Ligi ya mabingwa Simba jinsi ilivyo, tunakwenda kutoa ushindani wa kutosha huko ili kufika katika hatua za mbali zaidi kama malengo yetu yalivyo na hilo linawezekana.”

NAFASI YA KUCHEZA

Katika nafasi ya straika ambayo Kyombo anacheza Simba kuna ushindani wa kutosha kutoka kwa Moses Phiri, nahodha Jogn Bocco na Dejan Georgijevic wote wanaocheza katika nafasi hiyo.

Kyombo anasema amefika timu kubwa na akili yake imebadilika kutokana ushindani ni mkubwa tofauti na ule wa Mbeya Kwanza au Singida na wachezaji wote hapo ni wale wa daraja la juu.

“Juhudu zangu hapa Simba, kufanya vile ambavyo kocha anahitaji na nina imani kubwa vitanifanya nicheze kwani hata nikipata muda mchache nitahakikisha napambana na kuonyesha kiwango bora na kuisaidia timu,” anasema Kyombo.

REKODI MBAYA

Katika miaka ya hivi karibuni kuna wachezaji hasa nafasi ya ushambuliaji walifanya vizuri katika timu zao ila walipofika Simba walishindwa kuonyesha makali yao na walipotea baadhi yao ni Charles Ilanfia, Adam Salamba, Marcel Kaheza, Mohammed Rashid na wengineo.

Kyombo anasema jambo hilo analifahamu na changamoto ambazo ziliwafanya hao washambuliaji wengine kushindwa kucheza anazijua anazifanyia kazi ndani ya maisha ya Simba ili kuwa tofauti kwa upande wake.

“Timu kubwa unajua zina mambo mengi kama presha ukishindwa kuvumilia tu maana yake unashindwa kuonyesha ulichokuwa nacho kutokana na mashabiki wa timu hizi wanahitaji ubora tu na si lingine,” anasema Kyombo na kuongeza;

“Kwangu naamini nakuja kuweka rekodi nyingine mpya hapa Simba tofauti na hiyo ya wenzangu waliopita hapa binafsi nitafanya vizuri na kuisaidia timu katika mashindano yote.”

MECHI TATU

Kyombo anasema kuna mechi tatu ambazo hataweza kuzisahau katika maisha yake ya soka kutokana na mambo ambayo yalitokea ndani yake ambayo yalimuhusu.

“Mechi ya kwanza ni ile ya Simba ambayo niliumia goti hadi kushindwa kucheza nje baada ya kukaa miaka miwili bila ya kucheza mpira, kuna mechi niliwafunga Yanga mabao mawili pale Kirumba Mwanza na ya mwisho ni ile fainali ya ASFC dhidi ya Simba,” anasema Kyombo na kuongeza;

“Naikumbuka fainali dhidi ya Simba kutokana tulikuwa katika kiwango bora kuliko wapinzani na wachezaji wa Mbao tuliamini tunakwenda kuchukua ubingwa ila makosa madogo tu yalibadili mchezo na matokeo.”

Columnist: Mwanaspoti