Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KWELI CHEMA HAKIDUMU

166f7fb10795db4d21bbe50093b1e928.jpeg KWELI CHEMA HAKIDUMU

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ilikuwa kwangu ngumu, kuamimi jambo hili

Kwamba rubani muhimu, Joni Pombe Magufuli

Keshaiaga kaumu, roho imeacha mwili

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Wallahi nilitamani, habari isiwe kweli

Mama Samia Hasani, aikanushie mbali

Kwamba ni mitandaoni, wamemlisha kauli

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Japo ni ngumu kumeza, nimesadiki ukweli

Kwamba yarabi muweza, keshalitwaa jabali

Tangu sasa hatoweza, kuwa na sisi kimwili

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Ghafla iso hiari, jembe meondoka kweli

Nafikiri sibashiri, takuwaje zetu hali

Alitujaza jeuri, nchi hii ni asali

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Neema tulishaona, zikitiririka tili

Na uchumi ukinona, ukisonga kwenda mbali

Kichwa kinauma sana, naona giza kwa mbali

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Ile kansa ufisadi, aliondoshea mbali

Wanyonge wakafaidi, kwa huduma mbalimbali

Akasimika miradi, ni muhimu kweli kweli

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Kwa nini tulikupenda, vile ni mtu mkweli

Wajua tulikupenda, vile ni mtu adili

Hakika tulikupenda, wanyonge yako madili

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Fununu zilipokuja, kwamba una ngumu hali

Wenye nia ya pamoja, tuliomba kwelikweli

Mungu akupe faraja, urejee njema hali

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Rabi ungetuuliza, tungekwambia ukweli

Kwako tungependekeza, mpe tisini kamili

Atuache twapendeza, tukijilia vidali

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Mwenyezi mlaze pema, John Pombe Magufuli

Ile siku ya kiama, mlipe kwa maadili

Ingawa ametuhama, tutamkumbuka kweli

Nenda baba Magufuli, kweli chema hakidumu.

Columnist: www.habarileo.co.tz