Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI Rwanda

Cd5c5d6a651ac83c77147b2a6d662d57 KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI Rwanda

Wed, 7 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

LEO dunia inaadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda ambapo zaidi ya watu 800,000, wengi wao wakiwa kutoka kabila la Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa kikatili mwaka 1994.

Mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalianza siku moja baada ya ndege iliyokuwa imembeba Rais wa Rwanda, Juvenal Habyarimana kudunguliwa mjini Kigali, Aprili 6, 1994 na kumuua kiongozi huyo kutoka kabila la Wahutu pamoja na Rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira, na kila mtu aliyekuwa katika ndege hiyo alipoteza maisha.

Baada ya kifo cha Rais Habyarimana kikatiba Waziri Mkuu wa Rwanda, Agathe Uwilingiyimana alipaswa kuchukua nafasi ya urais lakini aliuawa na wanajeshi tarehe 7 Aprili kwa sababu alitazamiwa kuwa na siasa ya wastani, si kali.

Waziri Theodore Sindikubwabo aliteuliwa na kamati ya kijeshi kuwa rais mpya akaapishwa tarehe 9 Aprili.

Watutsi walio wachache walishutumiwa kwa kuidungua ndege hiyo na hatimaye Wahutu wenye misimamo mikali wakaanzisha mauaji makubwa na ya kutisha dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani, ndani ya siku 100 tu, huku wakisaidiwa na jeshi, polisi pamoja na wanamgambo. Walilenga kumaliza kanisa kizazi cha Watutsi (ethnic cleansing).

Huko nyuma Rais Paul Kagame alituhumiwa na Jean-Lousi Bruguiere, mmoja wa majaji maarufu wa Ufaransa kuwa alishiriki katika mauaji hayo ya halaiki ya wananchi wa nchi hiyo na mauaji ya Habyarimana.

Hatua hiyo ilisababisha serikali ya Rwanda nayo kuwatuhumu viongozi wa Ufaransa kuwa walishiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Kwa utaratibu huo Kamisheni Huru ya Kitaifa ambayo iliamuriwa na serikali ya Rwanda ikusanye nyaraka na ushahidi unaothibitisha nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya Rwanda, ilitayarisha nyaraka zilizofichua jinsi Ufaransa ilivyoshiriki katika mauaji hayo, ambayo yalipewa jina la “Jinai za Watenda Jinai”.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamisheni hiyo, duru za juu za kisiasa, za kidiplomasia na za kijeshi za Ufaransa ziliratibu na kutekeleza mauaji hayo ya kimbari.

Vilevile ripoti hiyo ilisema kwamba, Ufaransa ilishiriki katika kutoa mafunzo kwa wanajeshi na waasi wa Kihutu, kutoa silaha na suhula za kijeshi, kusaidia kwa siri mauaji, ubakaji na mateso katika ardhi ya Rwanda. Tuhuma hizo zilivuruga kabisa uhusiano kati ya Ufaransa na Rwanda.

Japokuwa miaka 27 imepita lakini yaliyotokea yameacha mabaki na majeraha. Ni tukio ambalo halitasahulika nchini Rwanda, karibu kila mmoja aliguswa na mkasa huu.

Hadi sasa nchi ya Rwanda bado inajaribu kupata ahueni kutokana na makovu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, na pia bado inapambana kujenga upya uchumi wake ambapo kahawa na chai ni miongoni mwa mazao makuu yanayoipatia fedha za kigeni.

Benki ya Dunia inasifu maendeleo ya nchi hiyo na inasema yamesaidia kupunguza umasikini na ukosefu wa usawa miongoni mwa jamii.

Aprili 7 ndiyo siku ya kumbukumbu ya mauaji hayo ambapo kila mwaka Rais wa Rwanda, Paul Kagame huwasha mwenge wa kumbukumbu katika Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari kwenye mji mkuu wa Kigali. Kumbuku hii hufanyika katika eneo linaloaminika kuwa zaidi ya waathirika 250,000 walizikwa hapo.

Siku hii ndiyo mwanzo wa maadhimisho ya kumbukumbu hizi na ambazo zinakuwa na matukio kadhaa yanayodumu kwa siku 100 zijazo, na ambazo zilitengwa kwa makusudi ya maombolezo ya nchi nzima.

Ikiwa leo dunia inaadhimisha kumbukumbu ya mauaji haya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kupitia ujumbe wake anasema kuwa siku hii inawaenzi wale wote waliouawa, wengi wakiwa Watutsi pamoja na Wahutu wenye msimamo wa wastani na watu wengine ambao waliyapinga mauaji ya kimbari.

Guterres anasema: “Na tunapata msukumo kutoka kwenye uwezo wa wale walionusurika kwa kuwa na maridhiano na urejeaji katika maisha ya kawaida. Hatupaswi kamwe kuruhusu ukatili kama huo kutokea tena.”

Aidha Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anasema kuwa wanadamu wanapaswa kusema hapana dhidi ya kauli za chuki na ubaguzi, na kukataa kujitenga, utaifa na uwekaji wa mipaka.

Anasema kwa kutambua tu kwamba sisi sote ni familia moja ya wanadamu ndani ya sayari moja ndipo tutaweza kuzimudu changamoto nyingi za ulimwengu ambazo zinatukabili – kutoka kwa Covid-19 hadi mabadiliko ya tabianchi.

“Tangu mauaji ya kimbari, Rwanda imeonesha kuwa inawezekana kunyanyuka kutoka katika majivu, kupona na kujenga upya jamii imara na iliyo endelevu zaidi. Tunapoangalia mbele kuongeza kasi ya juhudi za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, wacha tuchukue funzo kutoka katika somo linaloendelea la Rwanda,” anasema Guterres.

Maadhimisho ya mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka 27 ya mauaji hayo ambapo mwaka jana maadhimisho hayakufanyika kutokana na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona.

Imeelezwa kuwa katika miaka ya nyuma kumbukumbu hizo zilikuwa zinasababisha machungu na maumivu makali kwa baadhi ya watu, huku wengi wao wakiangua vilio au hata kuzimia katikati ya mkesha huo wa kumbukumbu.

Bado imekuwa vigumu kwa waathirika kadhaa kusamehe, kutokana na miili ya wapendwa wao kutojulikana ilipo na pia wauaji wengi kuwa huru.

Hii ni wazi kwamba wengi wanaendelea kuishi na kuhisi matokeo ya mauaji ya kimbari ambapo unakuta baadhi ya watu wametengwa na familia zao au labda hata hawana familia, japokuwa kuna mikakati ya kina ya upatanisho.

Wahalifu, waathirika, hata ambao hawakuwa wamezaliwa wakati huo, kwa pamoja wote wanakabiliwa na matukio hayo sawa, maana yamebeba historia ya nchi na yameigusa jamii na kuacha majeraha makubwa.

Licha ya hayo mauaji haya yalisababisha hata kukaibuka wimbi la wakimbizi zaidi ya milioni tatu kukimbilia katika nchi za jirani kusalimisha maisha yao na zaidi ya watu 120,000 kuwekwa gerezani wakisubiri kesi zao ziweze kusikilizwa na hatimaye kutolewa uamuzi.

Hata hivyo, Kanisa Katoliki bado limeendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa upatanisho, haki na amani kwa kutumia Tume za Haki na Amani. Kama ilivyo kwa nchi jirani ya Burundi, Kanisa pia linaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuwa chombo cha upatanisho, haki na amani.

Hii ni dhamana endelevu inayopaswa kusimikwa katika miundo ya dhamiri nyofu, uwekezaji katika maisha ya vijana kwa njia ya elimu na fursa za ajira ili waweze kujitegemea pamoja na kuhamasisha mwingiliano wa vijana katika nchi mbalimbali ili kujenga umoja na mshikamano.

Ni lazima katika nchi kuwafikiria vijana wa sasa na endelevu ili kweli waweze kudumisha utu, kwa kupinga vikali tabia za kibaguzi, kikabila na hali halisi ya utamaduni wa nchi husika.

Hata hivyo katika kipindi cha miaka 27 baada ya mauaji haya Rwanda imebadilika. Kwa sasa Rais Paul Kagame ndiye kiongozi anayesifiwa kwa kusimamia maendeleo ya haraka ya kiuchumi baada ya mauaji kumalizika.

Mafanikio yake yamempatia umaarufu kama kiongozi wa kuigwa katika bara la Afrika, hata kama bado kuna baadhi ya watu wanapinga misimamo yake mingine, lakini kwa hakika Rwanda kwa sasa ni moja ya nchi zinazoongoza hata katika ngazi ya teknolojia ya habari na sera ya uwekezaji ya maendeleo ya kidijitali.

Mwaka 2017 Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliitaja nchi ya Rwanda kama moja ya mifano ya mafanikio ya maendeleo katika intaneti barani Afrika.

Wakati wa Kongamano la Kiuchumi Duniani lililofanyika mjini Davos, nchini Uswisi, kuanzia tarehe 17 - 20 Januari 2017, Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Irina Bokova aliitaja Rwanda kama moja ya mifano ya mafanikio katika maendeleo ya intaneti duniani.

Kiongozi huyo alitolea wito nchi nyingi ambazo bado zina kiwango cha chini kwa matumizi ya intaneti kuiga mfano wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa kuungana na kuboresha mazingira ya maisha ya watu bilioni 3.9 ambao bado hawajafikia hatua hii.

Vilevile ushiriki wa wanawake katika uamuzi kwa ngazi zote za serikali umeiweka pazuri nchi ya Rwanda kama inavyothibitishwa Bi Emma Rubagumya, Mbunge na Mjumbe wa Kamati ya Masuala ya Jinsia katika Bunge la Rwanda.

“Sisi kama wanawake tunapokuwa wengi katika ngazi za kufanya uamuzi, inakuwa rahisi kwetu kwamba kila uamuzi unaofanywa serikalini basi huwa wanawake wameweka mchango wao ambao unatoka kwenye kujua matatizo hasa yanayowakabili wanawake,” anasema Rubagumya.

0685 666964 au [email protected]

Columnist: www.habarileo.co.tz