Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Joao Felix, tuendelee kusubiri au tutawanyike maskani?

Joao Felix To Cfc Joao Felix

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwili wako una thamani gani? Haijulikani. Katika umri wa miaka 19 tu mwaka 2019, Joao Felix aliuzwa kwa kiasi cha Pauni 113 milioni. Pesa bwana! Leo tumeshtuka kusikia bei ya Declan Rice ni Pauni 105 milioni. Tulishtuka kusikia bei ya Antony Pauni 85 milioni licha ya kuwa na mguu mzuri wa kushoto uliombatana na kichwa kibovu.

Joao aliuzwa kiasi hicho ambacho hadi leo kama kuna mchezaji akinunuliwa tunaona ni kiwango kikubwa cha pesa. Atletico walimnunua kutoka Benfica kwa kiasi hicho cha pesa. Atletico? Ndiyo. Moja kati ya uamuzi mbovu katika soka.

Wote wawili walifanya uamuzi mbovu. Hakuna aliyemstahili mwenzake. Ndiyo maana hadi leo katika umri wa miaka 24 Joao anaonekana anatangatanga. Hana uelekeo. Sijui kwa nini aliamua kwenda Atletico au sijui kwa nini Atletico waliamua kumchukua.

Atletico hii hii ya Diego Simeone haikustahili kuwa na mchezaji kama yeye. Atletico ambayo haichezi mpira wa kuvutia. Simeone anacheza mpira mgumu kama wa Jose Mourinho. Nimewahi kwenda pale Wanda Metropolitano. Ni ‘Mungu mdogo’ pale Atletico Madrid.

Hata hivyo, staili yake sio ile ambayo itakufanya utamani kuitazama Atletico tena na tena. Anacheza mpira mgumu. Ulinzi mwingi. Kukabana kwingi. Anacheza kutokana na adui anavyocheza siyo kumlazimisha adui acheze kutokana na Atletico inavyocheza.

Wakubwa wote wakiwa nyumbani au ugenini huwa wanatawala soka licha ya kusaka pointi tatu. Atletico hali ni tofauti. Wanacheza mpira mgumu kwa nyakati zote. Kuna wachezaji wagumu ambao wangeweza kumfaa zaidi Simeone.

Kina Didier Drogba.

Lakini katika umri wa miaka 19, kinda mahiri na mlaini kama alivyo Joao, staili yake ya soka angefaa kucheza timu ambayo inaweka mpira chini na kuutandaza kwa umahiri mkubwa huku ikiwa haina hofu ya adui.

Timu kama Barcelona ile au Manchester City ya sasa. Timu kama Liverpool ya Jurgen Klopp au Arsenal ya Mikel Arteta. Badala yake Joao akajitumbukiza katika mikono ya Simeone. Nilijua hawataweza kwenda sawa na ndicho ambacho kilitokea.

Uhusiano wa Joao na Diego ulikuwa wa kusuasua. Atletico walilipa kiasi hicho cha pesa na kila mtu alikuwa na matumaini Joao alikuwa anakwenda kuiteka dunia ya soka baada ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kutuhangaisha kwa miaka mingi.

Ilikuwa inaonekana Joao angekwenda juu kidogo ya pale alipokuwepo mchezaji kama Eden Hazard. Haikuwa hivyo. Kila siku Joao alikuwa anakwenda chini. Alikuwa mchezaji wa kawaida tu.

Baadaye akatolewa katika mikopo miwili. Mkopo wa kwanza ni ule wa mwaka 2023 alipokwenda Chelsea. Mkopo wa pili ni ule alipokwenda zake Barcelona. Bahati mbaya aliikuta Barcelona ikiwa imeshatoweka. Afadhali angekutana na Barcelona ile ambayo Xavi Hernandez alikuwa mchezaji.

Lakini alikutana na Barcelona hii ambayo Xavi alikuwa kocha. Alikutana na majanga.

Sasa, miaka mitano tu baada ya kuuzwa kwa Pauni 113 milioni, leo Joao ameuzwa kwa kiasi cha Pauni 43 milioni kwenda Chelsea. Ni hasara juu ya hasara kwa Atletico. Hatujui hasa tatizo lilikuwa wapi kwa Joao. Kwa kuanzia nahisi tatizo lilikuwa pale alipochagua kwenda Atletico.

Lakini wakati mwingine unaweza kwenda kusikiliza upande wa pili ukaambiwa labda tatizo lilikuwa kwake. Joao ni Mreno, lakini baba yake alihamia Ureno akitokea Brazil. Wazazi wake wote wawili, Carlos na Carla ni walimu. Labda hawakumfundisha malezi mema na akaishia kuwa na tabia za wachezaji wa Kibrazili ambao tunawafahamu kwa namna ambavyo wanapenda starehe.

Na sasa, Joao ameanza upya. Hauwezi kuamini ana umri wa miaka 24. Umri bado upo upande wake. Swali ambalo linatusumbua wengi ambao tulishuhudia wakati ule Atletico wakilipa pesa nyingi kwenda Benfica ni kama Joao anaweza kufikia kile ambacho tuliwahi kuambiwa au kusikia kutoka kwake.

Anaweza kurekebisha mambo na kuwa mmoja kati ya wachezaji bora duniani? Mpira unashangaza sana. Wachezaji wengi wa aina yake huwa hawarudi tena kuwa tishio. Wachezaji ambao walitarajiwa kufanya mambo makubwa duniani kisha wakapotea. Inakuwa ngumu kurudi hata kama umri haujasogea.

Ni hawa kina Fernando Torres, Phillipe Coutinho na wengineo. Ukipotea basi umepotea. Ni wachache ambao walipotea, lakini wakarudi katika makali. Na kuna wachache ambao walitarajiwa kufanya mambo makubwa halafu wakaonekana wa kawaida, lakini baadaye wakafanya mambo makubwa.

Mfano ni Martin Odegaard. Alitokea Norway akiwa kinda wa miaka 16 mwenye jina kubwa. Akaenda Real Madrid, lakini akatulizwa na vipaji vya wachezaji wakubwa kiasi cha kuanza kuonekana mchezaji wa kawaida. Akaenda katika mikopo minne.

Alienda Heerenveen na Vitesse za Uholanzi, akarudi Hispania akatolewa kwa mkopo kwenda Real Sociedad, akarudi akatolewa kwa mkopo Arsenal. Baadaye alinunuliwa jumla na Arsenal na sasa ni miongoni mwa viungo bora duniani.

Ni suala la kusubiri kuona kama Joao atakuwa yule ambaye dunia ilimsubiri kwa hamu wakati anaondoka Libson kwenda Jiji la Madrid. Kinachotatiza ni namna ambavyo amekwenda katika timu ambayo imevurugika. Chelsea ya leo haieleweki. Hata wenyewe hawajielewi. Wana wachezaji zaidi ya 43.

Chelsea ya leo ambayo kila ikimuona mchezaji inamchukua. Labda Kocha Enzo Maresca anaweza kurudisha kipaji chake kiasi kwamba Atletico watajuta kwa kumuuza kiasi cha Pauni 43 milioni. Na sisi ambao tumekaa katika vibandaumiza tukiendelea kumsubiri arudi kama alivyokuwa Benfica tunajiuliza, tuendelee kusubiri au turudi maskani?

Columnist: Mwanaspoti