Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura

VOTE Jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KINYANGANYIRO cha kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, sasa kimepamba moto, ambapo takribani wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani, wanapita kila kona ya nchi kunadi sera zao.

Kampeni hizo zilianza rasmi Agosti 29, mwaka huu na zinatarajiwa kukamilika Oktoba 27, ambapo Oktoba 28 mwaka huu, ndio siku rasmi ya Watanzania kupiga kura na kuchagua viongozi watakaliongoza taifa hilo.

Katika uchaguzi huo ambao ni wa sita tangu Tanzania iliporejea kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992, mchuano wa wagombea umekuwa mkali, ambapo kila mmoja anajitahidi kuvutia wananchi kwa sera na ahadi atakazozitekeleza pindi akipatiwa nafasi.

Mchuano huo umeonekana wazi kutokana na namna Watanzania walivyo na mwamko mkubwa, si tu wa kufuatilia wagombea katika kampeni zao, lakini pia kujadili na kuchambua sera na ahadi zikiwemo ilani zao.

Tangu kampeni zianze, idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza katika mikutano hiyo ya kampeni, kiasi cha kufanya iwe vigumu kutabiri hasa nani atashinda kwenye uchaguzi huo kama tu kitatumika kigezo cha mgombea kujaza watu.

Pamoja na hali hiyo, lakini bado ukweli unabaki kuwa iko haja ya wananchi kuelemishwa kupitia kampeni hizo, juu ya umuhimu wa kujitokeza na kuonyesha ushabiki kwenye mikutano hiyo na pia kujitokeza kwa wingi huohuo kupiga kura siku ya uchaguzi.

Kihistoria Tanzania inaonesha kuwa haifanyi vizuri katika eneo la wananchi kutumia haki yao ya uraia ya kupigakura, kwani wengi wao hujitokeza kujiandikisha na kupata kitambulisho cha kupigia kura na kuishia hapo tu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya mwaka 2000, wapiga kura waliojiandikisha walikuwa zaidi ya milioni 10 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa milioni 8.51, sawa na asilimia 84.4.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa milioni 16.4, lakini waliopigakura walikuwa milioni 11.36, sawa na asilimia 69.3.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu hizo, katika uchaguzi wa mwaka 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha ilikuwa milioni 20.13, lakini waliopiga kura walikuwa milioni 8.62 tu, sawa na asilimia 42.84 ya wapiga kura waliojiandikisha.

Na mwaka 2015, kati ya watu zaidi ya milioni 23.16 walioandikishwa kupiga kura, waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni milioni 15.58 tu, sawa na asilimia 67.31. Kwa mujibu wa takwimu hizo, ni wazi kuwa bado Watanzania hawana mwamko wa kutumia haki ya kupigakura.

Wengi wamebaki na dhana ya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura, ili tu wapate vitambulisho watakavyovitumia kujipatia huduma mbalimbali. Ni vyema sasa kwa muda uliobaki wa kampeni, wagombea mbalimbali pia wautumie kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa wao kujitokeza kwa wingi kupigakura, kwani wingi wao kwenye mikutano bila kupigakura, hautasaidia kumpata mgombea wanayemtaka.

Columnist: habarileo.co.tz