Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Jinsi viungo vya binadamu vinavyoteketezwa

Viungopicc Mkurugenzi Tiba Taasisi ya MOI , Dk Samwel Swai

Tue, 14 Sep 2021 Chanzo: Mwananchi

Umewahi kujiuliza viungo vinavyokatwa kutokana na ajali au magonjwa ikiwemo miguu, mikono, matiti, kondo la nyuma la uzazi, na viungo vingine kutoka kwa binadamu baada ya upasuaji hupelekwa wapi?

Je? Unafahamu kwamba mgonjwa ana haki ya kupewa kiungo chake kama atahitaji ‘kwa ajili ya kukizika tu na si vinginevyo’ iwapo tu, hakikuwa na maambukizi yoyote?

Taasisi ya mifupa na mishipa ya fahamu Muhimbili (MOI) ni miongoni mwa hospitali zinazohudumia wagonjwa wengi wa ajali.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Tiba wa taasisi hiyo Dk Samwel Swai alisema MOI huzalisha kilogramu 300 za taka hatarishi kila siku.

Alisema taka hizo zinajumuisha vitu ambavyo vimetolewa katika mwili wa binadamu vikiwemo viungo kama mkono, mguu, vinginevyo ambavyo vyaweza kusababisha magonjwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine au vikiingia kwenye mazingira vinaweza kuchukuliwa na panya, ndege au wanyama wengine vikasambaza magonjwa.

Alitaja vitu vingine kuwa ni pamoja na kitu chochote kinachotumika kukata tishu ya binadamu, vifaa vya kufunga vidonda, vifaa vya kuchukuliwa damu, vifaa vya kukusanyia vipimo vya maabara ambavyo vina vinasaba vya watu kwamba vyote vimewekewa utaratibu mzuri namna ya kuviteketeza kwa kuchoma kupitia mashine hiyo.

Hata hivyo alisema mgonjwa anayekatwa viungo kuna taratibu ambazo huwa wanazifuata katika kuteketeza kwani lazima ashirikishwe kuhusu kiungo chake na iwapo hakina maambukizi huwa anapewa.

“Kabla hatujateketeza Lazima aridhie, mwingine anataka kuondoka na mguu au mkono wake kwenda kuuzika anapewa utaratibu upi anatakiwa kuufuata, wapo wanaoomba wanapewa wavichukue hivyo viungo au wanaitaka wakaizike wenyewe,” alisema Dk Swai na kuongeza kuwa kwa mwezi wanaweza kukata miguu na mikono minne mpaka sita.

Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano kwa umma Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema hospitali hiyo ina mashine maalum ya kuchomea taka ambayo imekuwa ikichoma viongo vya binadamu zikiwemo kondo la nyuma la uzazi.

“Muhimbili ni kubwa sana hapa tunazalisha zaidi ya tani 10 mpaka 11 za taka kwa siku na kati ya hizo tani moja na nusu ni taka hatarishi kwa siku na utaratibu wetu mwongozo unatutaka kuziteketeza kwa maana mpaka mgonjwa amekatwa mguu au mkono lazima kuna maambukizi yalitokea ndiyo maana jopo likakaa likaona matibabu sahihi ni kuondoa kiungo,” alisema Aligaesha.

Hata hivyo baadhi ya hospitali za jijini Dar es Salaam nyingi hazina mashine za kuchomea taka hatarishi kulingana na gharama kubwa.

Mkurugenzi wa mazingira na taka hatarishi kutoka Tindwa medical and health services (TMHS) Maimuna Salum alisema kampuni hiyo inahusika kuhudumia hospitali zote za jiji la Dar es Salaam na pia kuhudumia taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD), Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Kiwanda cha Tindwa kilichopo Kisanga, Kisarawe kimekuwa kikihudumia zaidi ya vituo 100 jijini kwa taka zote hatarishi ikiwemo sindano, bandeji, mtu amekatwa viungo, placenta zinaketezwa hapa ni zile taka ambazo huwezi kuzipeleka jalalani zina athari kwenye mazingira na huleta maambukizi.

Maimuna alisema taka hizo hatarishi huchomwa mpaka kugeuka jivu kwa nyuzi joto 1200 hadi 1400.

Alisema tangu mwaka 2008 Tindwa wamefanikiwa kuchoma taka hatarishi zaidi ya tani 2570 zikihusisha dawa na vifaa tiba vilivyokwisha muda wake na tani 80 za ngozi za wanaume waliotahiriwa walizopokea kutoka mikoa 11 kwa ajili ya kuteketeza.

Columnist: Mwananchi