NIMES, UFARANSA. KAPUMZIKE baba. Hicho ndicho wengi wanachoweza kusema kuhusu Jean-Pierre Adams aliyefariki duniani Jumatatu.
Beki huyo wa zamani wa Ufaransa ameumaliza mwendo akiwa na miaka 73, lakini miaka yote 39 iliyopita kabla ya umauti kumfika alikuwa amelala tu kitandani, hajitambui, yu mahututi. Lugha maarufu ya kimombo inayoweza kuelezea hali ya mchezaji huyo wa zamani wa Nice, Paris Saint-Germain na Nimes ni kwamba alikuwa kwenye hali ya mahututi “coma”
Mzaliwa huyo wa Senegal, alicheza zaidi ya mechi 140 timu ya Nice akipita pia PSG na Nimes, huku akiwa ameitumikia timu ya taifa ya Ufaransa mechi 22 kati ya 1972 na 1976. Nimes aliichezea mechi 84.
Maisha ya kwenye mahututi ya Adams
Utamnunulia zawadi gani mtu aliye kwenye coma kwa zaidi ya miaka 30? Hilo ni swali walilokuwa wakijiuliza familia ya Jean-Pierre kila mwaka ilipofika tarehe za matukio mbalimbali yaliyomhusu.
Jean-Pierre alikuwa kitandani, hajiwezi na hajitambui tangu mwaka 1982.
Miaka 39 iliyopita akiwa mwanasoka shupavu kabisa na mwenye nguvu, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 34 alikwenda kwenye hospitali moja huko Lyon kufanyiwa upasuaji wa goti. Lakini, alipotoka hospitalini hapo hakuwa anaweza kuzungumza, kutembea wala kutikisa hata mguu wake tena.
Mke wake, mrembo Bernadette amekuwa akimhudumia kwa kila kitu tangu wakati huo hadi kufikia sasa ikiwa ni zaidi ya miongo minne na hatimaye amemwaacha mpweke mkewe. Adams amekwenda zake.
“Hakuna aliyesahau kumpa zawadi Jean-Pierre. Iwe kwenye siku yake ya kuzaliwa, Krismasi au Siku ya Kinababa,” alisema Bernadette alipozungumza na CNN.
Jean-Pierre, ambaye alitimiza umri wa miaka 73, Machi 10, mwaka huu, alikuwa na uwezo wa kupumua mwenyewe. Hakuhitaji msaada wa mashine ya kupumulia. Aliwekwa kwenye chumba chake maalumu chenye vitanda vinavyofanana na vile vinavyopatikana hospitali.
“Tulimnunulia zawadi za fulana au pajama kwa sababu nimekuwa nikimbadilisha nguo akiwa kitandani. Alibadili nguo kila siku,” alisema mkewe alipofanyiwa mahojiano akiwa nyumbani kwake Nimes, kusini mwa Ufaransa – mahali ambako Bernadette amekuwa akimhudumia mumewe Jean-Pierre kwa mapenzi makubwa.
“Nilinunua vitu mbalimbali kupendezesha chumba chake kama mashuka mazuri na manukato. Alikuwa akivaa Paco Rabanne lakini baada ya nembo hiyo kusitishwa, nikawa namnunulia Sauvage ya Dior.”
Jean-Pierre, ambaye ni mzaliwa wa Senegal alicheza kwa mafanikio makubwa klabu za Nimes, Nice na Paris Saint-Germain.
Mapenzi na mrembo Bernadette
Jean-Pierre alizaliwa Senegal na mrembo Bernadette alizaliwa Ufaransa. Jean-Pierre alienda Ulaya na bibi yake kwenye mambo ya dini na kuandikishwa katika shule moja huko Ufaransa akiwa na umri wa miaka 10 tu. Baadaye aliasiwa na familia ya Kifaransa na hapo Usenegali wake ukaanza kufutika. Kwenye miaka ya 1960, kipindi hicho Jean-Pierre akiwa mwanasoka wa ridhaa tu alikutana na Bernadette disko.
“Sitaki kuficha kwamba kipindi kile nilipata wakati mgumu sana kutoka kwa familia yangu,” alisema Bernadette kuhusu uamuzi wake wa kuanzisha uhusiano na mtu mweusi. “Kipindi kile, mwanamume mweusi na mwanamke mzungu kuwa pamoja haikuwa kawaida. Baada ya hapo, mambo yalikuwa sawa, kila kitu ikawa Jean-Pierre, Jean-Pierre!”
Wawili hao walifunga ndoa Aprili 1969 na kufanikiwa kupata watoto wawili wa kiume, Laurent (alizaliwa 1969) na Frederic (1976).
Tatizo lilipoanzia
Jean-Pierre alikwenda kwenye hospitali ya Edouard Herriot huko Lyon kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya X-Ray. Akiwa hospitalini hapo, daktari mmoja ambaye alikuwa shabiki wa soka alimwona Jean-Pierre na kumwambia kwamba atamsaidia.
Baada ya hapo, ikapangwa tarehe ya kufanyiwa upasuaji ambayo ilikuwa Jumatano, Machi 17, 1982. Tarehe hiyo ilipofika kulikuwa na tatizo. Madaktari wa hospitali hiyo ya Lyon walikuwa kwenye mgomo, hivyo Jean-Pierre alikwenda kufanyiwa upasuaji na daktari mwanafunzi na tatizo lote lilianzia hapo.
Baada ya makosa makubwa yaliyofanywa na daktari aliyemfanyia upasuaji, Jean-Pierre alipata tatizo linalofahamika kitaalamu kama bronchospasm linalotokana na ubongo kukosa hewa ya oksijeni na hivyo kumsababisha aingie kwenye coma. Miaka ya tisini, daktari aliyemfanyia upasuaji alipewa adhabu ya kusimamishwa kazi mwezi mmoja ambayo ilibadilishwa na kuwa faini ya Dola 815. Mke wake ndiye aliyekuwa anahangaika kumhudumia mumewe muda wote.
Aliporudishwa nyumbani
Baada ya miezi 15 ya kuwa hospitali, serikali ya mtaa ilipendekeza Bernadette kumchukua mumewe na kurudi naye nyumbani kwake, akamhudumie wakiwa huko.
“Sidhani kama walifahamu namna ya kumhudumia, hivyo nilisema nitamchukua arudi nyumbani na nitamhudumia,” alisema Bernadette.
Tangu siku hiyo, Bernadette alikuwa akiamka mapema kwa ajili ya kumwaandaa mumewe ikiwa ni kwa kumpatia huduma mbalimbali, huku akisoma machapisho tofauti yanayofundisha namna ya kumhudumia mtu wa aina hiyo.
“Wakati mwingine sikupata kabisa usingizi usiku,” alisema Bernadette.
Mtu mweusi wa kwanza kuichezea Ufaransa
Wakati sasa timu ya taifa ya Ufaransa ikishuhudia mastaa kibao weusi wenye asili ya Afrika, Jean-Pierre ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuichezea Les Bleus akiwa mchezaji mweusi
tena kutoka barani Afrika. Juni 15, 1972, Adams alicheza mechi yake ya kwanza kwenye timu ya taifa ya Ufaransa katika mechi ambayo haikuwa rasmi dhidi ya Kikosi cha Waafrika kilichokuwa kimechaguliwa na Shirikisho la Soka la Afrika. Mechi yake ya kwanza ya kiushindani ilikuwa Oktoba 13, mwaka huo, Ufaransa iliposhinda bao 1–0 nyumbani dhidi ya Umoja wa Nchi za Kisovieti kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 1974. Mechi yake ya mwisho kuichezea Le Bleus ilikuwa Septemba 1, 1976, walipomenyana na Denmark kwenye mchezo wa kirafiki. Kipindi hicho akiwa kwenye beki ya Ufaransa alitengeneza kombinesheni na Marius Tresor iliyopachikwa jina la La garde noire (black guard).
Baada ya hapo, wakaibuka mastaa wengine wa Kiafrika kuichezea Ufaransa kama vile Marcel Desailly kutoka Ghana, Kylian Mbappe kutoka Cameroon na Algeria, Paul Pogba kutoka Guinea, N’Golo Kante kutoka Mali na wakali wengine kibao waliowahi kuitumikia Les Bleus katika mechi za kimataifa ikiwa asili yao ni Afrika.
Mkewe hakukata tamaa
Mrembo Bernadette amekuwa na mapenzi yasiyopimika kwa mumewe, ambapo aligoma kabisa suala la kumchoma sindano mumewe afe ili kuepukana na shughuli ya kumhudumia kila kitu. Mrembo huyo aliamini kwamba ipo siku mumewe angeamka kutoka kitandani kwa sababu alikuwa anapumua mwenyewe bila msaada wa mashine, anahisi harufu na anasikia.
Jean-Pierre ameacha wajukuu pia baada ya watoto wake wawili wa kiume nao kuzaa watoto wao. Bernadette hakujali kitu kwamba mumewe amelala tu kitandani muda wote, alilazimika kumgeuza mara kwa mara ili ngozi isinasie kwenye godoro.
Hayo ndo yalikuwa maisha ya Bernadette kwa mumewe Jean-Pierre Adams hadi hapo alipofariki dunia juzi Jumatatu.
Mwanafunzi aliyempa huduma Jean-Pierre hospitalini, aliwahi kusema: “Sikuwa na ufahamu wa kazi niliyotakiwa nifanye.”
Pumzika kwa amani Jean-Pierre Adams, beki wa mpira!