Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JPM na kiu ya uzalendo wa waandishi wa habari

Dbcc5e664ac52b9e74b2dff445fda148 JPM na kiu ya uzalendo wa waandishi wa habari

Wed, 3 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KAZI mama ya kila mwandishi wa habari duniani ni kuhabarisha umma juu ya mambo kadha wa kadha. Kwa nyakati tofauti waandishi wanaweza kuendesha propaganda ili tu kufanikisha lengo zuri au wakati mwingine baya.

Kwa muda sana, suala la waandishi wa habari na dhana ya uzalendo hapa nchini limekuwa likifumbiwa macho. Kwa nyakati tofauti uandishi nchini Tanzania umeonekana kuandika habari zilizoegemea upande mmoja bila kutafuta usahihi wake.

Ilifikia wakati katika nchi yetu, yeyote anayeitwa mwanasiasa anaweza akasimama jukwaani akiwa na madai dhidi ya watawala ambayo kayasikia vichochoroni, kwa maana kwamba hana ushahidi wowote, lakini chombo cha habari kikayaandika yalivyo, bila kuchunguza ukweli wake wala kutilia maanani kama yanachafua nchi au la.

Pengine inawezekana ni kutokana na tasnia yenyewe ilivyo kwamba ni kazi inayohitaji kuendana na muda hasa katika kuwasilisha habari kwa ajili ya uchapishaji au utangazaji.

Lakini je, ndo iwe sababu ya kuvunja miiko ya uandishi? Lakini pia kuna wakati uandishi wetu umekuwa ukijikitika zaidi kwnye habari zilizokaa kimbeambea badala ya kuhabarisha kwa kina masuala ya msingi kwa umma.

Je, inawezekana kukosekana kwa weledi katika tasnia ya uandishi ni kutokana na upungufu wa maadili kwa wahusika? Lakini kuna wakati tumeandika habari ambazo wapinzani wetu kibiashara wamezitumia kuchukua soko ambalo lilitakiwa kuja Tanzania! Nimesikia, kwa mfano, baadhi ya habari zetu huko nyuma za kuiandika vibaya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zilisababisha washindani wetu katika biashara ya bandari kushawishi wateja kwa kutumia taarifa zetu zinazoponda bandari yetu na wao kuneemeka.

Nina habari pia kwamba kwa kosa lile lile la kutochunguza, baadhi ya makosa yamekuwa hayafanywi na TPA, kwa mfano shehena ikipata matatizo ikiwa imeshachukuliwa na mawakala, bado uandishi wetu ulikuwa ukiisakama TPA na kuipaka matope kumbe wahusika ni wengine! Vivyo hivyo, nimesikia baadhi ya habari zetu tunazoandika kutuharibia kwenye utalii, kwa wawekezaji waliotaka kuja nchini na kadhalika.

Ni wazi kwamba tabia hii haipo kwa waandishi wote lakini kwa kiasi fulani hali ya kutotoa nafasi dawa kwa pande zote (balancing) katika uandishi waetu wa habari limekuwa tatizo sana.

Kimsingi, mbali na kutoa nafasi sawa, sina hakima kama kila tunachoandika tumekuwa tukijiuliza endapo kinaisaidi nchi yetu au kinaharibu. Pia tuangalie kama tunachoandika kinasaidia wananchi au kinatia hofu na kuleta athari mbaya. Je, ni cha kweli au cha kuzua? Niliguswa sana maneno ya Rais Magufuli aliyoyasema tarehe 25 Februali mwaka huu.

Ninanukuu: “Vyombo vya habari mnajitahidi kutoa habari, lakini mtangulize uzalendo na haki kwa yule anayeandikiwa habari, kumekuwa na uzushi sana mara fulani kafa (wakati siyo kweli) ni mambo ya ajabu… Lakini pia katika habari ambazo taifa letu linaandikwa vibaya watu wanashabikia, uzalendo umepungua… Tutangulize uzalendo wa nchi yetu.

Niwaombe watanzania wote tutangulize maslahi ya taifa, wajenga nchi ni sisi na wabomoa nchi ni sisi”. Katika utawala huu wa Rais Magufuli ambao unaielekeza nchi katika kujitegemea na kuruka viunzi vya mabeberu, vyombo vya habari vya kimataifa na hata vya baadhi ya waafrika wenzetu ambao ni washindani wetu kibiashara, vimekuwa vikiiandika vibaya nchi yetu.

Tena wakati mwingine vimekuwa vikibeza hatua kadhaa zinazochukuliwa na viongozi wetu wakubwa wa kitaifa. Hii inawezekana na nikutokana na baadhi ya wanasiasa kuisema vibaya nchi yetu na kuidhalilisha kwa maslahi yao binafsi au kwa kutumiwa na mabeberu.

Kama waandishi kazi yetu ya msingi ilipaswa kulisafisha taifa letu dhidi ya watu wa namna hiyo lakini badala yake tumeonekana kuacha watu hao wazidi kulichafua taifa letu kana kwamba wanafanya vyema! Maneno ya Rais Magufuli yalinikumbusha maneno ya Rais Uhuru Kinyata wa Kenye aliyewahi kusema: “Lakini yako ni kwenda kuharibu jina la nchi yetu huko nje na mambo ambayo haina.

Wazungu wamejaribu kutufunga kwa miaka sita wameshindwa. Wamesema hakuna kesi. Tosheka na haya. Na urudi tujenge Kenya yetu pamoja. Siyo kutuchafua kila saa. Tumechoka.

“Hawajui ya kwamba kujenga ni ngumu lakini kupasua (kubomoa) ni dakika moja. Lakini hawana shida kubomoa kwa kuwa watatengeneza njia wawe viongozi. Uongozi siyo kiti bajameni, uongozi ni vile unawatedea wananchi ambao wataka kuongoza.”

Dhana ya uzalendo ni pana sana na pengine inaweza kuwa ngumu kuielewa vyema. Lakini ifahamike kwamba mwandishi ana nguvu kubwa ya kusaidia katika kujenga na kukuza uzalendo kwa watanzania wenzake.

Badala ya kuruhusu watu wachafue nchi yetu inatupasa kama waandishi kuisafisha kila mara na kuizungumzia yaliyo mema na kufanya kila mmoja wa watanzania atambue ubora wa nchi yake.

Rais Magufuli alisema maneno mazito kwamba maendeleo ya nchi yetu na ujenzi wake uko mikononi mwa kila mtanzania sawa na Imani ya TANU na Azimio la Arusha. Ni wazi kwamba nchi yetu haiwezi kuendelea kwa kutegemea misaada hata siku moja kwa kuwa: “Hakuna nchi moja duniani ambayo iko tayari kutupa misaada au mikopo au kuja kujenga viwanda katika nchi yetu kutimiza shabaha zake zote za maendeleo.

Nchi zenye dhiki ni nyingi sana duniani. Na hata kama nchi zote zenye neema zingekubali kuzisaidia nchi zenye dhiki, bado ingekuwa msaada huo hautoshi.

Lakini nchi zenye neema hazitakubali. Hata katika nchi ile ile, matajiri huwa hawatoi fedha zao kwa hiari ili zisaidie Serikali kuondoa dhiki.” Maneno haya yakatiliwa mkazo na Hayati Baba wa Taifa aliposema: “Tutaijenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe.

Akipatikana mtu wa kutusaidia tutashukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya watanzania wote, ni kazi ya watanzania wenyewe. Si kazi ya mtu mwingine.” Suala la ujenzi wa nchi haliko mikononi mwa viongozi wakubwa tu bali kwa kila mtanzania mmoja mmoja.

Na watu wenye nafasi ya kufanikisha katika kuhamasisha maendeleo haya ni waandishi wa habari kwa kuuhabarisha umma ili kuunga mkono juhudi za serikali na kila mtu kubeba jukumu lake.

Nafikiri huu ni wakati mwafaka kwa kila mtanzania kutanguliza uzalendo katika kutimiza majukumu yetu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawamaliza nguvu mabeberu kwa kuwa hawataweza tena kupitisha propaganda zao chafu dhidi ya viongozi wetu na taifa letu.

Naamini kiu ya Rais Magufui ni kuona kila mtanzania kwa nafasi yake akiionea uchungu nchi yetu. Huu ndiyo wakati mwafaka wa kumuunga mkono Rais wetu katika jitihada zake za kuienga nchi na Mungu atubariki.

+255-71224-6001 [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz