Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LAMWEWE: Tunafahamu wakubwa wanaomtamani Amissi Tambwe

Tambwe Pic Straika wa DTB FC, Amiss Tambwe

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hapo mtaa wa chini Amissi Tambwe ana mabao 14. Ligi Daraja la Kwanza (Championship). Nadhani wengi tunaweza kuwajua wanaomtamani Tambwe kwa sasa. Ni klabu za Ligi Kuu. Wanajua kuna kazi ambayo Tambwe angeweza kuwafanyia lakini bahati mbaya walidharau hapo mwanzo.

DTB ni klabu ambayo iliamua kumrudisha Tambwe nchini. Yeyote ambaye alitoa wazo la kumrudisha Tambwe nchini alitumia akili kubwa ambayo baadhi ya viongozi wa klabu za Ligi Kuu walishindwa kuitumia licha ya kupewa madaraka makubwa katika nafasi ambazo wanazo.

Wote tunafahamu ubora wa Tambwe. Katika hali ya kawaida tunaweza kuamini kwamba Tambwe asingeweza kufunga mabao 14 mpaka sasa katika Ligi Kuu. Labda Ligi Kuu ni ngumu kuliko Ligi Daraja la Kwanza. Labda tutumie akili ya kawaida tu. Tupunguze nusu ya mabao ambayo Tambwe angefunga Ligi Kuu.

Tufanye kwamba Tambwe angefunga mabao saba tu Ligi Kuu mpaka sasa hivi. Kuna washambuliaji wangapi wa Ligi Kuu ambao wamefunga mabao saba katika Ligi Kuu mpaka sasa? Inawezekana kwamba hii ni hesabu ya kufikirika zaidi na labda tungefanya hesabu nyingine.

Hesabu zetu nyingine tungefanya kwamba Tambwe angeweza kufunga mabao matatu tu mpaka sasa katika Ligi Kuu. Kuna washambuliaji wengi tegemeo katika klabu zao hawajafunga mabao matatu mpaka wakati huu ambao tupo katika raundi ya 17 ya Ligi Kuu.

Tambwe angefunga kama kawaida katika ligi yetu. Kwanza kabisa washambuliaji wa aina yake Waingereza huwa wanawaita ‘poacher’. Ni wale ‘vibaka’ wanaokwapua pochi katika stendi. Wafungaji wepesi ambao hawana mambo mengi mbele ya lango. Wana mabao mengi lakini wapo wachache. Kina Ruud Van Nistelrooy, Pipo Inzaghi, Javier Hernandez ‘Chicharito’ na wengineo.

Kuna tatizo la upotevu wa nafasi katika Ligi Kuu. Sio kwamba nafasi za kufunga hazipo, hapana zipo. Wafungaji ni wazembe. Tambwe angezipata hizo nafasi angefunga kama kawaida. Huwa namuamini katika suala la kutumia nafasi chache zilizotokea.

Achilia klabu yake ya DTB ambayo ilimuamini na kumrudisha nchini nafahamu klabu ambazo zingekataa kumrudisha nchini kama zingepata nafasi hiyo. Kisa? Wangesema ni mzee. Huku kwetu huwa tunaangalia zaidi suala la umri kuliko ufanisi. Kuna wachezaji wengi wanaondolewa katika soka kwa kisingizio cha umri.

Kuna wachezaji wengi ambao walianza kucheza mpira wakiwa wadogo lakini kwa sababu wamecheza kwa muda mrefu huwa tunawaita wazee. Mchezaji aliyegoma kuitwa mzee ni Juma Kaseja. Kama angesikiliza maneno ya Waswahili basi zaidi ya miaka kumi sasa angekuwa amestaafu soka.

Mchezaji kama Kigi Makasi hatutaangalia ufanisi wake uwanjani. Tutamuona mzee kwa sababu amecheza muda mrefu. Haya ndio maisha yetu ya soka yalivyo. Tambwe amerudi kututia adabu na kutukumbusha kwamba kitu cha msingi uwanjani ni ufanisi sio umri.

Lakini tujiulize ni kwa ligi gani hasa ambayo inaweza kumzuia Tambwe kufunga? Ligi hii hii ambayo katika umri wake bado Serge Wawa Paschal anatawala mabeki? Ligi yetu bado ina wachezaji wengi wasio fiti. Jaribu kufikiria jinsi ambavyo Geita Gold wanawategemea Kelvin Yondani na Juma Nyosso katika safu ya ulinzi.

Mtu mmoja aliwahi kuniambia kwamba Polisi Tanzania wanaamini kwamba wanayumba kwa sababu walimpoteza Yondani katika safu ya ulinzi. Jiulize Yondani amecheza kwa miaka mingapi katika kiwango cha juu. Nafasi yake pale Polisi Tanzania itakuwa imechukuliwa na kijana lakini atakuwa amepwaya.

Mpira wa Tanzania umri sio tatizo sana. Vipi Agrey Morris katika safu ya ulinzi pale Azam. Hata kama akiondoka Azam sasa hivi lakini nazifahamu klabu nyingi ambazo Agrey anaweza kuzisaidia katika staili hii hii ambayo Yondani na Nyosso wanasaidia wenzao.

Lakini nilimkumbuka rafiki yangu Tambwe wakati Yanga walipomsajili mchezaji kama Yikpe. Yanga ndio walikuwa wametoka kumuacha Tambwe msimu mmoja uliopita. Lakini ni bora kuwa na Tambwe aliyezeeka kuliko kuwa na Yikpe aliye na miaka 24. Wote walikuja kuuona ukweli baadaye.

Nafahamu kuna klabu kadhaa za Ligi Kuu zinaweza kumtaka Tambwe mwishoni mwa msimu kwa sababu kuna moja ilijaribu kufanya hivyo katika dirisha dogo la Januari. Ni somo tosha ambalo inabidi wajifunze kwamba dunia ina uhaba mkubwa wa washambuliaji.

Hata kwa wakubwa wetu ni kwamba unaweza ukahalalisha kutokuwa na Tambwe kama utakuwa na Fiston Mayelle, Meddie Kagere na Prince Dube. Vinginevyo kama una akina Yikpe basi unastahili kuendelea kuwa na Tambwe. Unaweza pia hata kuendelea kuwa na Donald Ngoma.

Kuna klabu nyingi za Ligi Kuu ambazo Tambwe angetesa kama kawaida. Kuna washambuliaji wengi wa Ligi Kuu ambao ni vijana na mpaka leo hawana uwezo wa kufunga kama Tambwe anavyofanya. Hata ukiwapeleka Ligi ambayo Tambwe anacheza bado hawawezi kufunga kama yeye. Kuna washambuliaji wangapi mahiri vijana wapo katika Ligi yake na hawafungi kama yeye?

Kitu kingine ambacho Tambwe atakuwa nacho ni uzoefu. Wakati tunapowasimanga wachezaji wetu kwamba umri wao umekwenda huwa tunasahau kukumbuka kwamba umri pia unaendana na uzoefu. Mabao mengi ambayo Kagere huwa anafunga kwa sasa huwa yanaendana na uzoefu. Tunashindwa tu kuchunguza.

Columnist: Mwanaspoti