Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Uswahili wa Mwakinyo na Kiduku upo pia katika soka

Hassan Mwakinyo Bondia mtanzania, Hassan Mwakinyo

Tue, 5 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Watanzania tunajipenda. Tunajikubali. Basi tu umaskini unatuponza katika maeneo tofauti. Unaweza usilione hilo katika macho ya wazi lakini ukichunguza utagundua kwamba tunajikubali sana. Wakati mwingine hata katika mifano iliyo wazi. Tazama tunavyotaka pambano la Hassan Mwakinyo na Twaha Kiduku liwepo.

Hapo tunasumbuliwa na Utanzania tu. Nasikia wana uzito tofauti. Mmoja anapigana sana na mabondia wa nje, mwingine anapigana na mabondia wa ndani. Mwakinyo kajikita kwa mabondia wa nje, Kiduku kajikita kwa mabondia wa ndani.

Uzito tofauti unafanya pambano lao lisiwepo. Lakini zaidi ni kwamba Mwakinyo hataki kupigana. Hata watu wake wa karibu ambao nawafahamu hawataki apigane? Wanataka Mwakinyo ajikite zaidi katika ngumi za kimataifa na sio hizi za ushindani wa ndani. Mwakinyo mwenyewe anajiona kuwa, Mbwana Samatta wa ngumi au Diamond Platinumz wa ngumi.

Hata hivyo, sidhani kama kauli zake zitabadili chochote. Watanzania watashinikiza pambano hili litokee. Kila siku watapiga kelele. Ataziba masikio kwa pamba lakini Watanzania watataka litokee. Watamtukana, watamponda, watamkejeli kwa muda mrefu kwa sababu hataki kupigana na Kiduku.

Watanzania tuna hili jambo. Tunajipenda. Hata katika soka huku tunajipenda sana. Kwa mfano, mchezaji akishindwa kucheza nje kwa sababu zisizoeleweka bado tunasimama nyuma yake. Wapinzani wa timu yako wanaweza kumponda lakini ile timu ambayo amekwenda watamshangilia bila ya kujali kama amerudi nyuma.

Ni kama Haruna Moshi ‘Boban’ aliporudi. Simba walishangilia, Yanga wakaponda. Ni kama Farid Mussa Maliki aliporudi. Yanga walishangilia, Simba wakaponda. Hatuwezi hoja mezani na kuangalia maslahi ya taifa hili ambalo lina wanasoka wachache wanaocheza nje ya nchi.

Wale wanaoshangilia hoja zao ni kama vile “Hata Bongo kuna pesa”. Mwingine atasema “Ni maamuzi yake mwenyewe mwacheni”. Furaha yao ni kuona tu kuwa mchezaji husika anacheza katika klabu yao. Hakuna muda wa kuweka hoja mezani na kutazama maslahi ya taifa. Tunatazama maslahi ya klabu.

Hata sasa hivi najua kwamba wapo ambao udenda unawatoka kwa Simon Msuva. Ukisikia tu kwamba Msuva kasaini Yanga au Simba kuna upande utalipuka kwa furaha. Hakuna ambacho watamlaumu Msuva zaidi ya kukipanga kikosi na kuonyesha namna ambavyo watamzamisha mtani pindi wakikutana.

Huyu Msuva ameimarika zaidi tangu alipokwenda kucheza Morocco. Nadhani tangu amekwenda Morocco ameifungia Taifa Stars mabao mengi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote akiwepo kaka yake, Mbwana Samatta. Amenufaika na soka la ushindani akiwa Morocco. Hata hivyo kama Msuva akisaini hapa, nani atajali?

Kuna ambao wanaweza hata kufurahi kama Kelvin John akirudi na kucheza timu yetu. Tutaamini kwamba tutakuwa katika nafasi nzuri ya kumchapa mtani wa jadi lakini pia kuchukua ubingwa. Hapa ndipo kwa kiasi kikubwa akili ya shabiki wa Tanzania imewekeza.

Ushindani wetu wa ndani umewekwa mbele kuliko ushindani wa nje. Bahati nzuri kuna mastaa ambao wamenufaika na ushindani wetu wa ndani. Mastaa wa kigeni. Hawa ni ambao wanaonekana wamefeli nje lakini wamerudi kuchota dola zetu. Miongoni mwao ni kama Clatous Chama. Binafsi sioni kama Chotta ameifelisha nchi yake kwa kurudi Tanzania.

Tunachosahau ni kwamba Chama ni Mzambia. Baada ya kutoka Morocco hajarudi kwao Zambia. Amekuja Tanzania kuendelea kuichezea timu ambayo inafika mbali katika michuano ya Afrika kuliko timu kubwa za Zambia, ZESCO na ZANACO.

Lakini kumbuka kwamba Chama bado anachotaka dola zetu kwa kiasi kikubwa na anakwenda kutumia kwao. Si ajabu akawa mchezaji anayeingiza pesa nyingi kuliko mastaa wote wanaocheza katika Ligi Kuu ya Zambia. Hauwezi kumlaumu sana yeye kuwa hapa hata kama ukisema alifeli Morocco.

Mwingine ni huyu rafiki yetu, Heritier Makambo. Watu wa Yanga walishangilia aliporudi tena nchini lakini bado ameendelea kuwa faida kwa nchi yake na familia yake. Anachukua dola zetu anapeleka kwao Congo. Alipofeli alikokwenda bado hakurudi kwao. Amerudia dola zake pale Jangwani.

Upinzani wetu wa sisi kwa sisi umezidi kuimarika kiasi kwamba sasa tupo katika hizi ngumi za Mwakinyo na Kiduku. Kuna rafiki yangu mmoja anaitwa, Ildephonce Amlima aliwahi kuniambia kitu cha maana kidogo. Kuhusu namna ya kushambulia lango kwa pamoja.

Wakati huo Amlima alikuwa staa mkubwa wa timu ya Bandari Mtwara iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu ya Bara ingawa wakati huo ilikuwa inaitwa Ligi Daraja la Kwanza. Upande mwingine kulikuwa na mshambuliaji mahiri wa klabu ya Africana Newala, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ambaye baadaye alitamba na Yanga.

Utanzania wa wakati huo uliwakabili watu wa Mtwara ambao muda mwingi walikuwa wakibishana nani zaidi kati ya Amlima au Mmachinga ambaye klabu yake ilikuwa daraja la pili ambayo kwa sasa ni kama daraja la kwanza. Niliwahi kuwa katika mkumbo wa kumuuliza nani alikuwa zaidi yao.

Amlima alinijibu katika busara kuu. Aliniambia “Watu hawapaswi kubishana nani ni zaidi kati yetu. Watu wajiulize mimi na Mohammed tukicheza timu moja itakuaje”. Ni jibu la busara ambalo sijawahi kulisahau. Imepita miaka 30 sasa hivi lakini sijawahi kusahau. Ni kitu hiki hiki ambacho watu walipaswa kukishinikiza katika suala la Mwakinyo na Kiduku. Labda wote wangekuwa bize kujitangaza kimataifa. Labda wakati mwingine wote wangekuwa wanaweka kambi moja wakati wakijiandaa na mapambano dhidi ya wageni?

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz