Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Tunavyosubiri kumuona kocha Chuji viwanjani

Chuji Pic.png Athuman Idd ‘Chuji’

Wed, 27 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nilimuona Athuman Idd ‘Chuji’ akipewa cheti cha ukocha wiki iliyopita. Nilitabasamu. Nilikumbuka mbali. “Leo Chuji kocha?” maisha yanaenda kasi. Majuzi tu alikuwa anasimama katika eneo la Jonas Mkude anacheza soka. Leo amekuwa kocha?

Atakuwa kocha wa namna gani? Sijui. Kumbukumbu ya mwisho kabisa ya Chuji inayonijia kichwani ninapokumbuka suala la ukocha wake, ni ile picha ya zamani akizungumza kisela huku akifoka akiwa katika Basi la Taifa Stars iliporeja kutoka katika michuano ya CHAN iliyofanyika Ivory Coast.

Yeye na Haruna Moshi ‘Boban’ walijitenga katika timu baada ya kocha, Marcio Maximo kukasirishwa na vitendo vyao vya utovu wa nidhamu. Njia nzima wakiwa hewani walikuwa wamejitenga huku wakimrushia kocha maneno makali.

Walipofika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walikuwa wa kwanza kushuka na kuondoka zao bila ya kufuata utaratibu kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine. Ulikuwa mwanzo wa mwisho wake katika kikosi cha Maximo.

Kwa vyovyote ilivyo, Chuji alikuwa amesuguana na Maximo katika suala la nidhamu tu. Maximo alikuwa kocha imara katika suala la nidhamu. Ni kama ilivyo kwa makocha wengi wenye mafanikio duniani. Nidhamu ni kitu cha kwanza kabisa katika timu.

Inaanzia nidhamu ya kocha mwenyewe. Halafu inakuja nidhamu ya wachezaji na wafanyakazi wote katika timu. Naam, hapa ndipo tunaposubiri kuona rafiki yetu Chuji atakuwa kocha wa namna gani katika kuendeleza soka letu nchini.

Kabla hajaingia kwenye uwanja wa soka na kuanza kufundisha anapaswa kujutia kila kitendo cha nidhamu alichowahi kufanya akiwa kama mchezaji. Hata lile tukio la Maximo inabidi alipime upya kwa akili yake ya ukocha na kutuambia kama alikuwa sahihi au hapana. Atajisikia amani kama kuna mchezaji wake akimfanyia vile wakati huu yeye akiwa kocha?

Lakini pia atawavumilia wachezaji wenye utovu mkubwa wa nidhamu? Chuji rafiki yetu alikuwa mchezaji msela. Nadhani unaweza kuwa mchezaji msela lakini hauwezi kuwa kocha msela. Hapa ndipo tunaposubiri kuona kama atakuwa amebadilika.

Tukiachana na hili la ukocha na masuala ya nidhamu, kuna kitu kingine kinanifurahisha. Majuzi nilikuwa namwambia rafiki yangu mmoja kwamba natamani kuacha kushabikia soka. Maisha yake yanakwenda haraka na nimeshindwa kwenda nayo sambamba.

Nilimuona Wayne Rooney akiingia uwanjani akiwa na umri wa miaka 16. Lilikuwa pambano la timu yake Everton dhidi ya Arsenal. Akafunga bao na kuzungumzwa sana. Baadaye akatua Manchester United. Akawa staa mkubwa zaidi. Baadaye akaenda Everton, akaenda Marekani lakini sasa ni kocha.

Si ajabu nitajikuta nikiendelea kuwa shabiki wa soka wakati mwanae Kay atakapoanza kucheza Ligi Kuu ya England. Nyakati zinakwenda kasi kwa wanasoka. Na hapa hapa nimemkumbuka tena Chuji. Juzi juzi tu alikuwa staa wa Taifa leo ni kocha.

Ni fundisho kwa akina Mkude. Kwamba maisha ya soka yanakwenda haraka na wanapaswa kujipanga. Wanapaswa kujipanga kipesa zaidi ili wasiadhirike siku za usoni. Kuna baadhi ya wachezaji wa zamani nafahamu kwamba wameingia katika kazi ya ukocha sio kwa kupenda. Ni kwa kusaka riziki kwa sababu mtaani kumekuwa kugumu.

Maisha pia yamekwenda kasi kwa kina Chuji kwa sababu sasa hivi nadhani ndio wanaweza kutafakari zaidi fursa walizopoteza wakati wakiwa mastaa wakubwa. Kwa mfano, hauwezi kuamini kwamba wakati huu Chuji anapoamua kuwa kocha hakuwahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi yetu.

Kwa viungo wote wa sasa nchini hakuna anayemfikia Chuji. Labda hawa wa kigeni. Hawa wa ndani hakuna ambaye anaweza kumfikia Athuman. Alijua namna ya kumiliki mpira, kupiga chenga, kukokota kwa usahihi, lakini zaidi kupiga pasi ndefu ambazo viungo wa sasa zinawashinda.

Mchezaji wa namna hii alimalizia mpira wake kwenye Uwanja wa Taifa. hakuna aliyewahi kumuona nje ya mipaka yetu akijaribu bahati yake. Hapa ndipo soka la taifa letu lilipokwamia. Walau kina Novatus Dismas wanajaribu kutorudia makosa.

Lakini pia wakati mwingine unapomuwaza Chuji leo akiwa anajaribu kazi ya ukocha lazima tukumbuke namna alivyoondoka katika soka mapema. Ana umri wa miaka 34 kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia.

Tayari anaonekana kuwa mchezaji wa zamani. Lakini tukumbuke kwamba Februari mwaka huu Cristiano Ronaldo alitimiza miaka 37. Hapo hapo tujiulize, Zlatan Ibrahimovic ana miaka mingapi? Kuna wachezaji wangapi wenye umri wa miaka 34 wapo uwanjani?

Hata kama alidanganya umri bado kuna wachezaji wengi wa bara la Afrika wanadanganya umri lakini wanacheza kwa kipindi kirefu. Bado naamini kwamba huenda Chuji angekuwa uwanjani mpaka sasa kama angekuwa na nidhamu kubwa nje ya uwanja.

Lakini bado naamini kwamba kama angeondoka nchini angecheza soka kwa muda mrefu. Nje kunadumisha maisha ya mchezaji. Viwanja vizuri, afya inazingatiwa, mazoezi timilifu pamoja na mazingira mazuri kwa ujumla.

Naamini Mbwana Samatta anaweza kucheza soka hata akifikisha miaka 38. Amesogeza mbele siku zake za kucheza soka kwa kwenda kucheza nje ya nchi. Anaweza kutoka Ubelgiji akaenda Uarabuni, kisha akarudi Afrika kucheza walau Mpumalanga ya Afrika Kusini. Anaweza kurudi na kuwa kocha mchezaji wa Coastal Union. Ndivyo ambavyo wachezaji wa Afrika huwa wanafanya.

Chuji kama ilivyo kwa kina Boban, Shadrack Nsajigwa na wengineo, wamemaliza mpira mapema kwa sababu ya mazingira yetu. Naamini wangeweza kucheza kwa muda mrefu zaidi kama wangeenda kucheza nje ya nchi.

Kwa sasa hatuna cha kufanya bali tumempokea Chuji ambaye ni kocha wa mpira. Tunasubiri kwa hamu tumuone ambacho atatufanyia katika masuala ya ufundishaji lakini pia kuimarisha nidhamu za vijana wake. itachekesha kidogo lakini ndio mabadiliko ya nyakati.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz