Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Saluti kwa Kibu Denis na Shomari Kibwana

Kibu Pic Vs Kibwana Kibu Denis na Kibwana Shomari

Tue, 7 Jun 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nilikuwepo Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba, wakati magari mawili ya wagonjwa yalipoingia uwanjani kuwatoa Shomari Kibwana na Kibu Dennis kuwapeleka hospitali ya Bugando. Walipasuka vibaya wakati kila mmoja alipokuwa akiitetea timu yake pambano la watani Simba na Yanga.

Shomari alikuwa anauondoa mpira kwa kichwa cha kuparaza, kibu alikuwa anataka kupiga kichwa cha mkandamizo na kama angeupata mpira basi lingeweza kuwa bao la kusawazisha kwa Simba. Hata hivyo aliishia kukigonga kichwa cha Shomari badala ya mpira. Kila mtu akapasuka.

Siku mbili baadae walikuwa wakifanya mazoezi katika kikosi cha timu ya taifa. Na juzi walikuwa uwanjani wakilitetea taifa katika pambano la kuwania kufuzu Afcon mwakani dhidi ya Niger katika ardhi ya Benin. Usione kitu cha kawaida sana.

Nawajua wachezaji wengi ambao wangekacha pambano hilo hasa baada ya kuumia namna ile. Wameshonwa nyuzi nyingi lakini wamerudi mazoezini na wamecheza mechi. Nawafahamu wachezaji ambao wangekacha mechi inayofuata baada ya kuumia vile. Sio tu wangekacha mechi ya timu ya taifa bali pia ya timu zao ambazo zinawalipa mishahara.

Kuna wachezaji wetu huwa wanadanganyika kwamba wana vipaji vikubwa na hawafanyi juhudi. Kando ya kipaji mchezo wa soka unahitaji juhudi kubwa. Wachanganue vema Kibwana na Kibu. Hiki walichokifanya ndio kielelezo cha namna ambavyo wanaumaliza msimu wao vema.

Yanga wametoka kumuongezea mkataba Kibwana. Ni mchezaji wa kwanza kuongezewa mkataba kabla ya kina Bakar Mwamunyeto na Zawadi Mauya. Kwanini? Kwa sababu amejitokeza kuwa mchezaji muhimu katika kikosi chao. Anajituma sana. Ilidhaniwa kwamba ujio wa Djuma Shaban ungemuondoa kikosini.

Matokeo yake Kocha Nasreddine Nabi akamhamishia upande wa kushoto na bado anapiga kazi. Ni mchezaji asilia wa Yanga. Katika sehemu ya kuweka mguu yeye anaweza kuweka hata kichwa. Yanga ina bahati na wachezaji wa namna hii tangu zamani.

Sio mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini mapungufu yake yamezibwa na tabia yake ya kujituma. Wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa wamejikuta wakipata wakati mgumu kukabiliana naye kwa sababu ya tabia yake ya kujituma uwanjani. Mwisho wa siku mchezo wa soka unahitaji jambo hili.

Sijui ni kitu gani kinamsukuma Shomari kuwa kama alivyo. Sijui kama ndivyo alivyozaliwa. Sijui kama anaukimbia umaskini wa familia yake. Sijui kama ndivyo ilivyo hulka ya watu wa kwao. Sijui. Ninachojua ni kwamba huenda akawa mchezaji anayejituma zaidi katika kikosi cha Yanga kwa sasa na watu wa Yanga wanampenda kwa hilo.

Kwa upande wa Kibu, anamaliza msimu akiwa mchezaji muhimu zaidi Simba. Ni mchezaji ambaye kuna watu hawamkubali. Hata hivyo kila siku anaendelea kuwa mchezaji muhimu kwa sababu tu ya kujituma. Sio mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini amefidia mapungufu yake kwa sababu ya tabia ya kujituma. Simba ipo katika msimu ambao mashabiki na viongozi wanauona mbovu.

Mabosi wa timu walijaribu hadi kumrudisha Clatous Chama katika kikosi lakini, Kibu ameendelea kuwa mchezaji muhimu zaidi klabuni licha ya kiwango chake kuwagawanya mashabiki na mabosi wa timu hiyo.

Kwa sasa unaweza pia kumuamini Kibu mbele ya Pape Sakho. Unaweza kumuamini Kibu mbele ya akina Chris Mugalu na wengineo. Inawezekana wanamzidi maarifa lakini Kibu anahusika katika matukio mengi zaidi kwa sababu anajituma zaidi.

Kuna kitu inaonekana kinamkimbiza nyuma yake. Kitu ambacho kinamtia msukumo. Ameishi katika maisha ya ukimbizi kwa muda mrefu. Naambiwa ameishi sana katika kambi za wakimbizi. Soka ndio mchezo ambao umemuondoa katika hizo kambi na kumleta katika hoteli nzuri anazoishi na timu yake ya Simba na timu ya taifa.

Mtu kama huyu hawezi kuangalia nyuma. Atafanya kila analoweza asirudi katika maisha yale. Sisi tuna wachezaji ambao wanauringia mchezo wa soka kwa sababu ya kutegemea nyumba za urithi. Wengine wanauringia kwa sababu wanaambiwa wana vipaji vikubwa na mashabiki. Hawaoni sababu ya kuwa na juhudi kwa sababu wanaambiwa na mashabiki kwamba mpira ni kama baiskeli. Ukiweza kuendesha hauwezi kusahau.

Bahati mbaya hakuna kazi fupi kama ya mchezo wa soka. Ukiwa na miaka 30 tu unaanza kuitwa mzee. Baadaye kidogo unaondoka katika soka huku katika maisha ya kawaida ukiwa kijana mbichi. Ni hapo ndipo unapoanza kugundua makali ya maisha na namna ulivyozembea katika uwekezaji wakati unacheza.

Ni hapo ndipo unapogundua kwamba mchezo wa soka ulikuwa ni kazi muhimu ambayo ulipaswa kujitolea kwa nguvu zako zote kama ambavyo kina Kibwana wanafanya kwa sasa. Bahati mbaya kwa wakati huo ndipo unapojua kwamba wachezaji wengi huwa hakuna wanachoweza kufanya nje ya soka kwa sababu hawakwenda shule.

Siku hizi nimeanza kuwaona hadi wachezaji ambao hawakuwa na nidhamu wakati wanacheza soka nao wanajitumbukiza katika kazi ya ukocha. Wanatafuta sehemu ya kushikia kwa sababu wamegundua hakuna wanachoweza kufanya nje ya soka. Zamani wakati wanaringa walidhani umri usingewakumba. Walidhani wangecheza soka kwa umri mrefu zaidi. Hata hivyo umri ni ukuta. Leo wanatapatapa na nadhani wanajuta kwa kushindwa kupambana wakiwa na nguvu na kuwekeza zaidi wakati wanacheza soka.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz