Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Onyango anajiuliza maswali ambayo hata sisi tunajiuliza

Onyango Tz Web Beki wa kati wa Simba, Joash Onyango

Tue, 30 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Uvumi ni mwingi kuhusu Joash Onyango. Kwamba anataka kuondoka zake Msimbazi na kutokomea kwingineko baada ya Kocha wa Simba, Zoran Maki kumuacha akilipasha moto benchi la timu hiyo. Unaweza kusadiki uvumi huo ni wa kweli kwa sababu Onyango hakuzoea hivyo.

Hadi sasa Joash itakuwa hajui ni kitu gani kimempiga usoni. Itakuwa ni kitu kizito chenye ncha kali. Kwa misimu yote amekuwa beki wa kati namba moja. Ametengeneza kombinesheni na Kennedy Juma. Halafu akadumu muda mrefu na Sergi Wawa Paschal.

Alipoingia Mcongo mwenye makeke, Enock Inonga ilibidi Wawa aanze kusugua benchi huku Onyango akicheza sambamba na Inonga. Maisha yalikuwa mazuri kwake. Haikuwa bahati mbaya Onyango aliendelea kuwa beki namba moja wa Simba.

Watu wa Yanga walijaribu kumvunja nguvu Onyango kwa kumuita Mzee. Mara kadhaa niliwauliza ni mzee gani anayeweza kuwa na kasi kama ya Onyango? Mzee gani anayeweza kuusoma mchezo kwa umakini mkubwa na kulihami lango lake?

Ni mzee gani anayeweza kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani juu na chini? Hata katika pambano ambalo Inonga alimsindikiza nje ya uwanja Fiston Mayele alikuwa ni Onyango ndiye aliyemdhibiti vilivyo Mayele lakini Inonga akaenda kujichukulia sifa za bure mbele ya kamera za Azam TV kwa kumsindikiza nje Mayele alipokuwa akitolewa.

Lakini ghafla amekuja beki anayeitwa Mohammed Ouattara. Beki wa kimataifa wa Burkina Faso. Haikujulikana kama beki huyo amekuja nchini kwa ajili ya kuwa msaidizi wa Onyango na Inonga, au amekuja nchini kwa ajili ya kuanza kucheza moja kwa moja na kuchukua nafasi moja ya Onyango au Inonga.

Na sasa tumejua kwamba kumbe alikuja nchini kuchukua nafasi ya Onyango. Nilichopenda kutoka kwa Kocha wa Simba, Zoran Maki ni kwamba hakutaka kuwa mnafiki. Hakutaka kubadili mfumo wake kwa ajili ya kumridhisha beki wa tatu wa kimataifa katika kikosi chake.

Hakutaka kwenda katika mfumo wa kutumia mabeki watatu kwa ajili ya kuwaridhisha mabeki wake watatu wa kimataifa kutoka Congo, Kenya na Burkina Faso. Ameamua kwenda na Inonga na Ouattara. Hii ina maana imegharimu nafasi ya mmoja kati ya wachezaji muhimu katika historia ya Simba miaka ya karibuni.

Kitakachokuwa kinamshangaza Onyango ni kile kile ambacho kinatushangaza sisi. Ametupwa nje huku kiwango chake kikiwa kile kile ambacho tunakifahamu. Ametupwa nje ya kikosi bila ya kufanya makosa uwanjani. Labda alifanya makosa katika mechi za kirafiki za Misri ambazo hatukuziona wakati Simba ilipokuwa inafanya maandalizi ya msimu mpya.

Vinginevyo katika macho ya wengi ukiwauliza mashabiki wa soka bila ya kujali itikadi zao, ni beki gani bora kati ya Onyango na Inonga nadhani wengi watakwambia ni Onyango. Ingawa hachezi na jukwaa lakini amekuwa na sifa nyingi zaidi uwanjani kutokana na uimara wake.

Kama hali ikiendelea hivi basi Onyango atakuwa na maswali mengi kichwani. Lini nafasi yake itakuja? Januari mwakani anatimiza miaka 30. Wachezaji wa umri wake huwa hawapendi kukaa benchi. Ukimtazama katika benchi unamuona wazi hana furaha. Hii ni tabia ya kishindani ambayo wanayo wanasoka wengi wa kimataifa kasoro wanasoka wa Tanzania.

Lakini hapohapo kumbuka kwamba mapema mwanzoni mwa msimu Onyango alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba. Maisha yakiendelea hivi ina maana hatavumilia kabisa kukaa benchi.

Ni kweli ameomba kusitishiwa mkataba wake kwa sasa? Sina uhakika isipokuwa utakuwa mtego mkubwa kwake na klabu yake.

Simba hawataweza kukubali kirahisi kwa sababu wanajua kwamba beki yeyote kati ya Quattara au Inonga akipata matatizo basi Onyango ni chaguo sahihi la kuziba pengo lake na si Kennedy Juma. Wanawezaje kumruhusu kuondoka?

Lakini hili ndio tatizo ambalo Simba wamejitengenezea wao wenyewe. Kuwa na mabeki watatu wa kimataifa wa kigeni. Kama wangekuwa na wawili tu kisha Kennedy Juma anatumika kama wa akiba kusingekuwa na tatizo sana kwa sababu Kennedy angekubali hali hii lakini sio Onyango.

Pale Yanga wamejikuta wakifanikiwa kwa ujanja ujanja wao wa kuwa na Yannick Bangala kama msaidizi wa mabeki wa kati. Kati ya Bakari Mwamnyeto na Dickson Job mmoja akipata tatizo basi Bangala anacheza. Lakini hata kama hiyo ingekuwa nafasi rasmi ya Bangala basi mmoja ambaye anakaa nje asingejisikia kama Joash anavyojisikia kwa sasa.

Kwa upande wake mwenyewe kama akiamua kuvunja mkataba basi Simba haitamlipa pesa nyingi. Atakuwa ameamua kuvunja mkataba mwenyewe. Labda timu ambayo anaweza kwenda itakuwa imemuahidi pesa nyingi kama akivunja mkataba wake. Kitu ambacho nahisi kinaweza kutokea.

Kwa ninavyomtazama Onyango ni wazi kwamba ana uwezo wa kucheza timu mbili kubwa nchini kando ya Simba ambazo ni Yanga na Azam FC. Tofauti na akina Saidoo Ntibanzokonza ambao wakubwa hawakukimbizana nao baada ya kumaliza mikataba yao, Onyango ni mchezaji ambaye Yanga na Azam wanaweza kumpitia kama upepo kama Simba wakiachana naye.

Na Simba nao sio wajinga. Wanajua kwamba hilo linaweza kutokea na hii ni sababu nyingine ambayo inaweza kusababisha wasiuchane mkataba wa Onyango. Na kwa namna ambavyo Zoran amewachanganya kwa mambo mengi huenda wasikubali kuwapoteza wachezaji wengi kwa sababu yake.

Onyango anaingia katika kundi la mastaa wa Simba ambao inadaiwa hawakubaliki na Zoran lakini kumbe wanakubalika kwa uongozi. Nadhani hawataweza kukubali kuwapoteza wachezaji hawa wakati muda wa Zoran klabuni unaweza kuwa mchache kuliko muda wa wachezaji wenyewe.

Columnist: Mwanaspoti