Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Novatus ameliheshimisha eneo la kina Hamis Gaga

Nova Pic Novatus ameliheshimisha eneo la kina Hamis Gaga

Tue, 5 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Zamani niliwahi kuandika mahali kwamba mchezaji wa kwanza wa Tanzania kutamba Ulaya atakuwa anatokea katika eneo la ushambuliaji. Zilikuwa ni hesabu nyepesi. Hakuna eneo ambalo ni rahisi kuhesabu namba za mchezaji kama ushambuliaji.

Unahesabu tu mabao aliyofunga halafu unajua kwamba ni mfungaji hatari. Unaweza pia kuhesabu namba za msaada wake katika mabao (asisti), lakini lengo kuu la mchezaji kuwa mshambuliaji ni kufunga. Yawe mabao mazuri au ya kawaida. Unaweza kufunga hata kwa kutumia tumbo lakini tutahesabu.

Na duniani hakuna mfungaji mbaya. Hakuna mfungaji wa mabao rahisi wala magumu. Haya mabao ambayo tunayaona rahisi yanatokana na mchezaji kukaa katika nafasi yake katika wakati sahihi (positioning). Sio kila mshambuliaji anaweza.

Ilikuwa rahisi kwa Wazungu kumchukua Mbwana Samatta kwa sababu waliangalia namba zake akiwa na TP Mazembe. Hawakuhitaji sana kujua kuhusu utaifa wake. Utaifa haufungi mabao. Hivyo Genk wakajibebea Samatta kama nilivyofikiria awali.

Lakini pia kwa sasa wana Kelvin John. Huyu naye wamemchukua kwa sababu ya namba zake. Tangu akiwa katika timu za vijana, Kelvin amekuwa mfungaji mzuri. Ilikuwa rahisi tu kuangalia mabao yake na kisha kumchukua.

Lakini ukitazama pia kwa umakini mkubwa mastaa wengi wa siku za karibuni ambao wamekuwa wakitoka nchini kwenda nje ni washambuliaji. Kina Habib Kyombo, Eliud Ambokile, Eliuter Mpepo na wengineo. Wazungu wanasaka sana washambuliaji.

Kabla ya huyu Novatus Dismas ambaye amejiunga na klabu ya Ligi Kuu ya Ubelgiji Zulte Weregem, ni Himid Mao tu ndiye ambaye ni kiungo anayecheza soka la kulipwa nje ya mipaka yetu. Inaonekana ni eneo gumu.

Kwa kwenda kucheza soka katika klabu ya Ligi Kuu ya Ubelgiji, Novatus ametuheshimisha kwa mambo mawili. Kwanza ameendelea kutuheshimisha katika soka la Ubelgiji. Anakuwa staa wa tatu kutoka Tanzania kucheza katika Ligi Kuu ya Ubelgiji baada ya Samatta na Kelvin.

Walau ameendeleza kijiwe chetu. Hawa watatu wanafungua njia hata kwa mastaa wengine wa Tanzania kuaminika zaidi nchini humo. Kabla yao usingeweza kumuamini mchezaji wa Tanzania kwa sababu wazungu akili zao zipo kwa wachezaji wa Ivory Coast, Nigeria, Cameroon na kwingineko ambako wana historia ndefu ya soka.

Lakini, Nova ameiheshimisha nafasi yenyewe ya kiungo. Sijui sana kuhusu Sunday Manara ambaye naye anatajwa alicheza kwa mafanikio soka la Ulaya. Anatajwa kwamba alikuwa kiungo mshambuliaji. Hizo zilikuwa zama za zamani.

Katika zama za sasa Nova ametuwakilisha katika eneo hilo nyeti katika soka. Ni eneo ambalo kwa miaka mingi lilikuwa likitoa mafundi. Kwa sisi watu wa zamani kidogo tunawakumbuka kina Athuman China, Method Mogella, Issa Athuman, Hamis Gaga, Dadi Athumani, Steven Mussa, Octavian Mrope na wengi wengineo.

Wakati mwingine huwa tunatazama soka na kujiambia katika nafsi; “Kama angekuwepo zama hizi basi Gaga angecheza soka la kulipwa Ulaya”. Hizi ni kauli za kawaida katika vijiwe vyetu. Lakini sasa kuna wachezaji ambao wana zama zao.

Wachezaji hawa ni kama hawa kina Nova, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu na wengineo. Kwa sababu tupo katika dunia ya uwazi ingekuwa ujinga kama baada ya miaka kadhaa tungeanza kuambiana; “Ingekuwa zama hizi basi Novatus angecheza Ulaya.” Isingekuwa sahihi. Wakati ni sasa.

Nova amefanya kweli zaidi kwa sababu pia ametokea Ulaya kwenda katika klabu nyingine ya Ulaya. Ina maana ameonwa akiwa na klabu ya Ulaya na kisha akapata usajili wa kwenda juu zaidi. Ligi Kuu ya Israel ipo chini kulinganisha Ligi Kuu ya Ubelgiji. Inamaanisha kwamba amefanya kazi nzuri Israel. Hakwenda kuongeza idadi ya wachezaji amekwenda kushindana.

Katika umri wa miaka 19, Nova amekwenda Ulaya wakati sahihi zaidi. Tutalijadili hili siku nyingine, lakini ukweli ni kwamba anaweza kufika mbali kwa sababu amejisogeza katika Ligi inayozalisha vipaji vya kwenda ligi kubwa zaidi akiwa na umri mdogo.

Kina Yaya Toure, Victor Wanyama, Cheikh Kouyate na wengineo walipita katika ligi hii na kwenda katika ligi kubwa zaidi kwa sababu kuna maskauti wengi ambao wamekuwa wakiitolea macho. Kwa ninavyomfahamu Nova sidhani kama anaweza kutuangusha.

Ana sura ya kitoto, lakini amekomaa kiakili na kimwili. Anacheza soka la shoka na hapana shaka anatuwakilisha vizuri katika eneo la kiungo ambalo kwa miaka mingi, hasa zamani, lilikuwa linatoa wachezaji wa aina mbili kwa wakati mmoja. Wachezaji wenye umaridadi wakiwa na mpira lakini pia wanacheza soka la shoka. Hawa ndio kina Athuman China.

Achilia mbali suala la nafasi yake, lakini tuendelee tu kujikumbusha kwamba wakati huu wenzetu wakitegemea wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya mipaka yao ili wapate mafanikio, sisi hatuna budi kufuata njia hiyo.

Siamini kama wachezaji wetu wazawa wanaocheza nyumbani wanaweza kutusogeza popote pale katika timu ya taifa. Tunahitaji hawa kina Nova waweze kupenya huku na kule kwa ajili ya kutuletea maarifa yao katika kikosi cha taifa. Hakuna njia nyingine ya mkato zaidi ya hii.

Lakini pia Nova ameendelea kuonyesha kwamba inawezekana kwa wachezaji wetu kutamba Ulaya. Kama tulihisi kwamba kwa Samatta ilikuwa ngekewa, au kwamba kwa Kelvin ilitokana na kubebwa na Samatta, basi hapa kwa Nova tumepata mfano mwingine tofauti.

Kupitia kwake ambaye amekwenda katika klabu nyingine ya Ubelgiji bila ya kuwa na uhusiano na kina Samatta imeonekana wazi kwamba kuna uwezekano wa kujibeba mwenyewe ukafanya makubwa.

Columnist: Mwanaspoti