Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Nani anajali jezi ya Taifa Stars kwa sasa?

Stars Matumaini.jpeg Nani anajali jezi ya Taifa Stars kwa sasa?

Tue, 6 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Rafiki yangu mmoja anaitwa Muhaji Junior aliposti katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram juzi akisema; “Yanga kama haichezi wikiendi hainogi kabisa.”

Nilitabasamu. Hakupenda kuwa mnafiki. Alitoa hisia zake za moyoni. Unaweza kudhani masihara lakini alikuwa anawakilisha hisia za watu wengi wa klabu yake.

Kwake Yanga ni tamu kuliko Taifa Stars ambayo ilitazamiwa kucheza baadae jioni yake. Ni hisia ambazo zimewabamba Watanzania kuhusu klabu zao kiasi kwamba kama kituo kimoja kingekuwa kinaonyesha mechi ya Yanga na Transit Camp halafu na kituo kingine kinaonyesha Stars na Uganda basi wangechagua Yanga na Transit Camp.

Kabla rafiki yangu hajasema alichokisema, marafiki zangu wengine walikuwa wakifuatilia pambano la Simba dhidi ya AS Arta Solar 7 lililokuwa unachezwa katika Uwanja wa zamani wa Taifa, sasa Uhuru maarufu kama shamba la Bibi.

Wengi wao walikuwa mashabiki wa Simba. Pambano la Taifa Stars halikuwa kipaumbele kwao.

Jioni likachezwa pambano la kufuzu kwenda Chan kati ya Taifa Stars dhidi ya Uganda pale Uganda. Stars wakachapwa mabao 3-0 na kutupwa nje ya michuano hiyo. Swali la msingi kubwa zaidi ni wapi lilipo tatizo la Taifa Stars.

Yataibuka maswali mengi. Mengine yatakuwa ya kinafiki zaidi.

Kitu cha kwanza kabla ya kujadili uwezo wa Taifa Stars tunapaswa kujadili ukweli mashabiki wa Tanzania hawana ‘mood’ na Stars. Wala hawakuwa na ‘mood’ na Taifa Stars. Katika siku za karibuni akili na mawazo yao yote yapo katika klabu zao mbili kubwa nchini Simba na Yanga. Ndio maana naamini kwamba Muhaji hakuwa mnafiki.

Kikosi cha Stars kilichoanza juzi kilikuwa kimesheheni wachezaji wengi wa Simba na Yanga. Ni Abdul Hamis ‘Sopu’ na Danny Lyanga ndio ambao hawakuwa wachezaji wa Simba na Yanga katika kikosi kilichoanza. Mashabiki walikuwa na kila sababu kuifuatilia Stars kwa karibu, lakini wala hawakufanya hivyo.

Katika mechi za karibuni wala hawafanyi hivyo. Huwa inatokea mara chache mashabiki kuwa na karibu hasa wanapopata matokeo mazuri.

Matokeo yake wachezaji hawaihofii jezi ya Stars. Wanakuwa bize na jezi za Simba na Yanga. Timu haina morali. Wachezaji hawana morali.

Kila mtu hana morali. Tukiachana na mambo ya uwezo wa timu, lakini kitu cha kwanza kwa Taifa kinapaswa kuwa morali. Kwa sasa haipo. Mara ya mwisho ilikuwepo wakati Stars walipoifunga Uganda mabao 3-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha tukaenda AFCON 2019.

Matokeo yake wachezaji wala hawana presha ya kuichezea Taifa Stars. Wala hawaoni kama ni jambo la hatari kupoteza mechi ukiwa katika jezi ya Stars. Presha ni kubwa ukipoteza mechi katika jezi ya Simba au Yanga kuliko jezi ya timu ya taifa. Kuna nyakati chache ambazo zimewahi kutokea jezi ya Stars ikawapa wachezaji wa Stars presha lakini sio nyakati hizi.

Tukiachana na suala hilo sasa hivi litaibuka suala la uwingi wa wachezaji wa kigeni nchini.

Mara nyingi suala hilo huwa linaibuka pale tu Taifa Stars wanapofanya vibaya. Kwangu mimi hii ni hoja mfu.

Kuziruhusu Simba, Yanga na Azam kusajili wachezaji 12 wa kigeni kila timu hakulinyimi Taifa muda wa kuendeleza wachezaji wake.

Tatizo hatuzalishi vipaji maridhawa. Klabu nyingine zimejaza wachezaji wa kizawa. Mbona hatuoni uhodari wao?

Labda pia inawezekana ubora wa kina Fei Toto na Jonas Mkude unachangiwa zaidi na na wachezaji wa kigeni pindi wanapocheza katika klabu zao. Kumbe wakikutana wenyewe kwa wenyewe wanakuwa wachezaji wa kawaida tu.

Labda mafanikio ya Simba kufika robo fainali ya michuano ya Afrika yalichangiwa zaidi na kina Luis Miquissone, Clatous Chama, Rally Bwalya, Joash Onyango na wachezaji wengine wa kigeni. Kumbe kama kikosi chao kingekuwa na wazawa watupu huenda wasingefika popote. Kama wangepangwa kina John Bocco, Hassan Dilunga, Ibrahim Ajibu, Miraj Athuman huenda wasingefika kokote.

Matokeo ya Stars yanachangiwa na mambo mawili. Hatuna wachezaji wazuri waliotengenezwa kishindani, pia hata waliopo hawana morali. Jaribu kuangalia mechi hizi mbili.

Sisi tulijaza wachezaji wa ndani wanaotesa katika soka letu huku wanaokosekana wakiwa ni watatu tu. Mbwana Samatta, Simon Msuva na Novatus Dismas.

Wenzetu walichezesha wachezaji wa ndani pia, lakini waliokosekana ni wengi. Wakati huo huo tunaamini kwamba tupo katika Ligi Bora ukanda huu kuliko Waganda.

Kumbe kinachong’arisha Ligi yetu ni hawa kina Fiston Mayele, Moses Phiri, Nelson Okwa na Prince Dube. Matumizi ya pesa yamekwenda juu na tunajishawishi kuamini kwamba Ligi yetu ni bora kumbe ubora unaletwa na wageni.

Lakini hapo hapo tunaweza kujiuliza namna ambavyo tumekuwa wepesi katika visingizio mbalimbali pindi timu inapoteza mechi. Mtu wa kwanza kutolewa mhanga alikuwa Kim Poulsen na benchi lake la ufundi.

Ilikuwa baada ya kichapo cha awali. Kumbe matatizo yetu mengi binafsi ya muundo wa soka letu tunaona tatizo ni kocha.

Walipokuja watu wengine kichapo kimekwenda juu zaidi. Tumefungwa zaidi. Na wao pia wakaona moja kati ya matatizo ya soka letu ni ukosefu wa John Bocco pale mbele.

Ukitazama jinsi pambano la kwanza lilivyokwenda unagundua tatizo halikuwa George Mpole wala John Bocco. Timu haikutengeneza nafasi na tukamuona Mpole tatizo.

Mpira wetu utaendelea kuwa wa viraka kwa muda mrefu, lakini ukweli ni kwamba hatuzalishi vipaji vya uhakika.

Waganda wanazalisha wachezaji wengi shule na wanakwenda katika mifumo sahihi ya soka.

Kikosi chao cha juzi kimesheheni wachezaji waliotokea timu ya vijana.

Sisi wachezaji wetu ni wale wale wa miaka nenda rudi. Nani mrithi sahihi wa Mohammed Hussein Tshabalala? Hatujui.

Kuna kitu hakipo sawa katika soka letu, lakini hatutaki kukiona. Leo ataondolewa kocha, kesho ataondolewa mshambuliaji lakini hakuna tunachokipata.

Zamani ingekuwa rahisi kwa mashabiki kudai kwamba Samatta hajitumi katika kikosi cha Taifa Stars. Leo hayupo na hatuna wa kumuangushia mzigo.

Katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 17 kilichofuzu michuano ya mataifa ya Afrika chini ya huo nchini Gabon miaka kadhaa iliyopita, ni Dickson Job pekee aliyeanza mechi hiyo. Nini kimetokea kwa wengine? Hatujui. Hakuna mwendelezo wa ubora.

Soka la Tanzania lipo zaidi katika ligi tu na linanogeshwa na wachezaji wa kigeni tunaowaimba kila siku. Kina Mayele, Chama, Ousmane Sakho, Khalid Aucho, Yannick Bangala na wengineo. Vinginevyo kiwango chetu cha wachezaji wa ndani kinatia mashaka.

Columnist: Mwanaspoti