Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Mwanza ni rafiki wa Yanga adui mkubwa wa Mnyama

Sure Boy Kati Kati Mchezo ulimalizika kwa Yanga kushinda 1-0

Tue, 31 May 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mwanza haijawahi kuwaacha Simba salama pindi wanapocheza na Yanga. Haijawahi. Ilitokea mwaka 1974 wakati baba yake, Haji Manara, Sunday Manara ‘Computer’ alipoongoza vita ya kumuua mnyama katika Uwanja wa Nyamagana. Mnyama alikufa 2-1.

Ikatokea mwaka 2010 wakati Jerry Tegete alipofunga bao la kiufundi akiunyanyua mpira vema juu ya nywele za kipa, Juma Kaseja na mpira kutinga wavuni. Lilibaki bao hilo hilo kwa dakika zote 90 za mchezo huo uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba. Sitaki kusimulia pambano mapambano yao ya Kombe la Hedex ama lile pambano la kirafiki ambapo Simba ilipigwa 3-0, Kirumba.

Juzi tena, Mwanza haijamuacha salama Mnyama. Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika dakika ya 26 alikokota mpira kuanzia katikati ya uwanja. Viungo na mabeki wa Simba walishindwa kumdhibiti haraka. Akili zao zilikuwa kwa Fiston Mayele na Heritier Makambo ambao walikuwa wanafungua nafasi.

Fei akaachia shuti kali ambalo si tu kwamba Beno Kalolanya hakuliona, hapana, hata Peter Schmeichel asingeweza kuliona. David De Gea asingeweza kuliona pia. 1-0. Kwanini wachezaji wa Simba hawakumfuata mtu aliye na mpira? Inashangaza kidogo. Mpira ukaisha hivyo hivyo na kuhitimisha msimu mbovu wa Simba.

Ndani ya uwanja kuna mambo machache ya kusimulia. Achilia mbali bao la Fei, lakini kipindi cha kwanza Yanga waliwakamata vema Simba katika eneo la kiungo. Yanga walijaza viungo wanne ikiwa sio kawaida yao. Yannick Bangala, Fei Toto, Khalid Aucho na Salum Abubakar ‘Sure Boy’. Kocha Mohammed Nabi alifanikiwa katika alichokitaka.

Halafu mbele huwa inatokea mara chache kwa Nabi kuwaanzisha kwa pamoja, Mayele na Makambo lakini alifanya hivyo. Sababu ni rahisi tu. Hali ya uwanja kwanza haikuwa nzuri sana na kocha alitaka Makambo na Mayele wapigiwe mipira mirefu ya juu.

Lakini, Mayele amekuwa akidhibitiwa kwa urahisi na mabeki wa Simba, Joash Onyango na Henock Inonga ‘Varane’. Nabi aliamua kuwaongezea mshambuliaji ili agawanye majukumu yao. Kwa kiasi fulani Yanga walionekana kuwa tishio wakati ikiwasaka washambuliaji wao.

Yanga walionekana kwenda katika lango la Simba kwa kasi na kujiamini zaidi kwa sababu walikuwa wanatawala eneo la kiungo ambalo Sadio Kanoute, Thadeo Lwanga na Mzamiru walionekana kuelemewa. Mwishowe waliishia kucheza rafu mara kwa mara.

Hawakuweza kuwatafuta vema washambuliaji wao. Ilimlazimu Chris Mugalu kushuka chini kuja kucheza na viungo wake. Kibu Dennis ambaye kwa siku za karibuni ameibuka kuwa mchezaji muhimu zaidi Simba hakuwa na siku nzuri juzi.

Kipindi cha pili kuanzia dakika ya 70 Simba walibadilika na kuanza kuielemea Yanga. Hata hivyo krosi zao na kona zao za mara kwa mara ama ziliiishia katika mikono ya Djigui Diarra au katika vichwa vya Bangala, Bakari Mwamunyeto na Dickson Job. Hakukuwa na ubunifu mkubwa wakati wakilikaribia lango la Yanga.

Hatari za Simba juzi zilikuja zaidi katika mipira mirefu. Hii sio Simba ambayo tunaifahamu. Simba ambayo miezi 24 ilikuwa inatamba na mastaa wanaojua kuweka mpira chini. Simba ambayo iliziangusha Al Ahly, Vita, TP Mazembe na wengineo katika uwanja wa Taifa.

Subiri kwanza. Simba iliwakosa wachezaji muhimu katika pambano hili. Jukwaani nilikuwa nimekaa na Shomari Kapombe na John Bocco ambao kama wangekuwa fiti wangecheza. Lakini Clatous Chama alikuwa kwao Lusaka, Zambia. Jonas Mkude alikuwa Dar es Salaam akiutazama mpira katika televisheni. Aishi Manula alikuwa katika benchi akiwa amefunga plasta katika kidole chake.

Bernard Morrison walishaagana naye na hatufahamu kama alikuwa Dar es Salaam au Accra. Tunachofahamu ni kwamba hakuwepo Mwanza, naye alishaagana na timu huku ikiwa imebakiza mechi saba za Ligi. Ilichekesha kidogo kwa mchezaji muhimu kama yeye.

Ni ngumu kuweka hili kama kisingizio au hapana. Hata mastaa hawa wanapokuwepo Simba ya msimu huu bado imeonekana kusuasua na hatujui ambacho kinaweza kufuata baada ya pambano la juzi. Inaonekana kuna fagio litatembea Msimbazi.

Kabla ya mechi juzi Yanga ndio ambao walikuwa wanatamba zaidi kwamba wangeibuka na ushindi na ndicho kilichotokea. Timu yao imeimarika zaidi huku Simba wakionekana kuterereka zaidi. Baada ya kutolewa katika robo fainali ya michuano ya Shirikisho Afrika, morali imeshuka zaidi na kuna migogoro ya chini kwa chini. Nini kinafuata kwao? Kitu cha kwanza sijui kama wataendelea kuwa na kocha Pablo Franco. Soka la Tanzania, hasa katika timu kubwa, kocha anakuwa mhanga wa kwanza kama mna msimu mbovu. Imetokea mara chache kwa kocha kupona baada ya msimu mbovu kama huu wa Simba.

Watakapotathmini kikosi chao wanapaswa kuja na jibu kama tatizo ni kocha au wachezaji au uongozi. Hata kama wakiamua kuwa tatizo ni kocha bado kocha mpya ajaye atalazimika kukifumua kikosi upya. Kuna maeneo mengi ambayo Simba watalazimika kujisaka upya.

Kuna wachezaji wamechoka baada ya kucheza vema kwa misimu mitano mfululizo. Nadhani Simba inaweza kuachana pia na washambuliaji wawili au mmoja kutoka katika kundi la John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu. Itakuwa mara yao ya kwanza kusaka mshambuliaji mpya wa uhakika baada ya kuvuma kwa hao jamaa.

Kwa Yanga tuendelee kusubiri na kuona jinsi ambavyo msimu utaisha. Ni rahisi kuiongelea Simba kwa sasa kwa sababu mashabiki wake wanataka kujua mambo mengi kuhusu timu yao Yanga. Ni msimu unaowaumiza kwa kiasi kikubwa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz