Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Miaka 45 ya Hat-trick ya Kibadeni ni sifa au uzembe?

Kibaden Mputa Abdalah Kibadeni, Mchezaji wa zamani Simba SC

Tue, 22 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Tumeingia katika mwaka mwingine. Mwaka wa maadhimisho ya hat trick ya Abdalah Kibadeni. Wazee wa zamani walimuita Mfalme. Anabakia kuwa mchezaji wa mwisho kufunga mabao matatu ndani ya pambano moja la Simba na Yanga. Alifanya hivyo Julai 19, 1977.

Huu utakuwa mwaka wa 45 tangu Kibadeni atupie hat trick ile. Nilikuwa na miezi mitatu tu tangu nizaliwe. Mpaka leo hat trick ile inatukuzwa vilivyo. Wanaofanya hivyo hauwezi kuwalaumu kwa sababu kinabakia kuwa kitu pekee na cha kipekee katika pambano la watani.

Hata hivyo, zipo nyakati ambazo najiuliza. Ni sifa kuwa na hat trick ya zamani hivi? Jaribu kufumba macho na kujiuliza washambuliaji wangapi hatari wamepita katika klabu hizi tangu Kibadeni afanye vile? Wamepita wengi hatari ambao walikuwa na sifa zilizotukuka.

Wamepita kina Zamoyoni Mogella, Mohammed Hussein, Edward Chumilla, Amissi Tambwe, Makumbi Juma, Mbwana Samatta na wengineo wengi. Sasa hivi wapo kina Fiston Mayele, John Bocco, Meddie Kagere na wengineo ambao tunawaimba. Bado rekodi ya Kibadeni inasimama.

Mchezaji wa mwisho ambaye alikaribia kufikia rekodi ya Kibadeni ni Emmanuel Okwi. Siku ile ambayo Simba waliitandika Yanga mabao 5-0 pale Uwanja wa Taifa Okwi alikuwa amefunga mabao mawili, ikapatikana penalti lakini akamuachia Juma Kaseja. Ilikuwa nafasi pekee kwa Okwi kumfikia Kibadeni kama angepiga penalti na kuukwamisha mpira wavuni.

Pia kuna Hamis Kiiza ‘Diego’ katika ile mechi ya mabao 3-3 ya Simba na Yanga alifunga mabao mawili na alikuwa moto, lakini alitolewa na kumnyima kufikia rekod hiyo.

Kwanini rekodi inasimama kama ilivyo? Nadharia ni nyingi. Kwanza kabisa wakati mwingine hat trick ni bahati. Huwa inatokea tu mchezaji kuangukiwa na nafasi na akafunga zote. Hata hivyo, huwa haitokei mara nyingi. Lakini kama ikitokea basi ambaye anaangukiwa na hizo nafasi inabidi awe hatari kama Kibadeni alivyokuwa. Je, akina Mohammed Hussein walikuwa hawangukiwi na nafasi hizo? Tujiulize.

Lakini kuna nadharia ya ugumu wa pambano la Simba na Yanga. Linakuwa pambano lenye presha kubwa na washambuliaji bora ukamiwa. Ni kama ambavyo Simba walivyomkamia Mayele katika pambano la raundi ya kwanza la Ligi Kuu. Hakupumua. Joash Onyango na Enock Inonga walimpania hasa.

Lakini imekuwa hivyo enzi na enzi. Athuman Juma Chama ‘Jogoo’ alisifika kwa kumkaba vema Zamoyoni Mogella katika pambano la Simba na Yanga. Licha ya uhodari wa Mogella lakini takwimu zinaonyesha kwamba Mogella aliifunga Yanga mara moja tu.

Kuna picha moja ya zamani huwa inanivutia. Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ anaonekana akikunjana na George Masatu ambaye ni mmoja kati ya mabeki bora kuwahi kutokea nchini. Kulikuwa na bifu kali kati yao na nadhani ndio maana hat trick ilikuwa ngumu kwa Mmachinga dhidi ya Simba.

Nadharia ya ugumu wa pambano la Simba na Yanga inashindiliwa na ukweli kwamba timu yoyote kati ya hizi ikiwa dhaifu bado pambano linaweza kuwa gumu.

Mfano, washambuliaji wa Yanga walikuwa wapi kujipatia hat trick dhidi ya Simba wakati Simba walipokuwa dhaifu kiasi cha kukaribia kushuka daraja mwishoni mwa miaka ya themanini?

Lakini ndio kwanza Simba wakaichapa Yanga katika pambano la mwisho la msimu mwaka 1987. John Makelele akifunga bao la ushindi baada ya kipa wa Yanga, Sahau Kambi kufanya makosa katika lango lake. Yanga walikuwa imara haswa na Simba walikuwa dhaifu hasa..

Inawezekana upepo huu ndio ambao umewapitia kina Meddie Kagere hapa karibuni. Yanga walikuwa dhaifu huku wakiwa na Kindoki langoni lakini matokeo yakawa hayatabiriki. Simba licha ya kutamba Afrika lakini ikajikuta inapata matokeo mabovu dhidi ya Yanga. Fikiria akili yako ilikutuma nini katika pambano ambalo Bernard Morrison aliifunga Simba? Ungeweza kudhani Simba ingetoka na ushindi mnono.

Achilia mbali hilo, lakini nadhani washambuliaji wa hizi timu wanakosa utulivu na wanamezwa na hofu ya ukubwa wa pambano lenyewe. Unaweza kuliona hilo vema kwa sababu wachezaji wengi mahiri wanajikuta wakitolewa uwanjani na kuambiwa wamecheza kinazi.

Kinachotokea ni hofu tu kwa wachezaji wenyewe na wala sio kwamba wanacheza kinazi. Clatous Chama amewahi kutolewa na kuzomewa. Kwa Haruna Niyonzima kadhalika ilishatokea hali hiyo. Simon Msuva amewahi kutolewa na kuzomewa. Aliishia kulia tu. Hofu inakuwa kubwa wakati mwingine na mpira unawakataa.

Vyovyote ilivyo nimeanza kuona hat trick ya Kibadeni kama imeanza kuchosha hivi. Naona wakubwa barani Ulaya huwa wanatupiana hat trick bila ya shida. Zinafungwa hat trick nyingi katika mechi za watani wa jadi barani Ulaya, au zile ambazo zinahusisha timu kubwa.

Manchester United dhidi ya Liverpool kuna hat trick zimepigwa miaka ya karibuni na hasa nakumbuka ile ya Dimitar Berbatov. Ilikuwa Septemba 2010 tu na sio 1977. Ni kama ambavyo hat trick ya mwisho ya watani wa Manchester ilifungwa mwaka 1995 na Andrei Kanchelski. Haikuwa mwaka 1977.

Steven Gerrard aliipiga Hat trick Everton miaka 10 tu iliyopita. Lakini hata pambano la El Clasico limekuwa likitoa hat trick za kutosha licha ya ugumu wake. Inakuaje tunashindwa kumpiku Kibadeni aliyefanya hivyo miaka 45 iliyopita? Kuna kitu labda hakipo sawa.

Lakini kama wachezaji wenyewe wanashindwa basi huwa ninacheka pale mashabiki wa timu fulani pia wanapojiapiza kwamba wanakwenda kumchinja mnyama mabao mengi au kumkandamiza gongowazi mabao mengi, lakini tukienda uwanjani tunakuta hadithi tofauti.

Ebu watu wa Simba na Yanga pambaneni kidogo mvunje rekodi ya Kibadeni. Napata hisia kwamba sio jambo la sifa sana kwa rekodi hii kudumu miaka 45. Hat trick sio jambo jepesi, lakini sio jambo gumu. Natoa changamoto kwa kina Mayele na Kagere kabla hawajaondoka.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz