Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Mayele alivyoamua ugomvi wa Misri na Kigamboni

N3 Data JICHO LA MWEWE: Mayele alivyoamua ugomvi wa Misri na Kigamboni

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakati kibao kikimuita Fiston Kalala Mayele aende katika benchi, safari hii Henock Inonga hakuweza kumsindikiza na kujigamba kuwa amemdhibiti kama alivyowahi kufanya katika pambano la kwanza la pambano la kwanza la Ligi Kuu msimu uliopita.

Pambano hilo Inonga alionekana akimsindikiza Mayele na kutoa ishara kwamba yeye ndiye aliyekuwa amemdhibiti. Mashabiki wa Simba walishangilia vilivyo tukio hilo. Juzi, Mayele alionekana kutetema mbele ya Inonga wakati beki huyo akielekea vyumbani. Mayele aliibuka mshindi.

Mabao yake mawili yaliamua pambano la juzi katika mechi ambayo Simba walicheza kipindi cha kwanza halafu Yanga wakaimaliza katika kipindi cha pili. Binafsi yalikuwa ni matokeo yaliyonishtua kidogo. Kabla ya mechi dalili zilianza kuonyesha kwamba Simba wangeweza kuibuka washindi.

Simba walijaa uwanjani. Kulikuwa na sababu kadhaa. Kwanza kabisa walianza maandalizi yao mapema kabla ya Yanga. Wakati wakiwa Misri wakianza mazoezi, wachezaji wa Yanga walikuwa sebuleni, kila mmoja katika familia yake wakicheza na watoto. Na zaidi ni kwamba Yanga walipoanza mazoezi yao siku 10 baadaye, Simba walikuwa Misri na wao walitarajiwa kuanza mazoezi yao Morogoro.

Baadaye wakaamua kuanza kambi yao nyumbani kwao Kigamboni. Lakini kikubwa ambacho kiliwafanya Yanga wasije kwa wingi uwanjani huku Simba wakijitokeza kwa wingi ni matokeo yao ya wikiendi iliyopita wakati wakitambulisha vikosi vyao.

Yanga walichapwa 2-0 na Vipers ya Uganda huku wakionekana wakiwa hawako sawa sana. Simba wakashinda 2-0 dhidi ya St George ya Ethiopia. Ishara ilikuwa ni kuwa tunaona kile ambacho kimefanyika Pre-Season. Binafsi niliamini kwamba yalikuwa matokeo halisi kwa sababu hii hii ya namna ya maandalizi yao ya mwanzo wa msimu yalivyokuwa.

Hata bao la Pape Ousmane Sakho lilipofungwa ilionekana kama vile utabiri wa mashabiki ungetimia. Lilikuwa bao maridadi shukrani kwa mwamuzi wa pembeni. Haikuwa offside. Hata kama ingekuwa offside bado tusingemlaumu sana. Mstari alipokuwepo Sakho na watu wa mwisho wa Yanga ulikuwa umekaribiana mno.

Simba walionekana kutawala vema kipindi cha kwanza kiasi cha kuamini kwamba walikuwa wametangulia maandalizi. Halafu ghafla mechi ikaanza kwenda katika kila upande lakini Simba walimaliza kipindi cha kwanza wakionekana kuwa sawa zaidi. Kocha wa Yanga, Mohammed Nabi alionekana kujaza viungo wengi huku kocha wa Simba pia akionekana hivyo hivyo.

Kipindi cha pili Yanga hawakuchelewa kupata bao la kusawazisha. Alikuwa ni Fiston. Pasi aliyopenyezewa na Aziz Ki ilikuwa ya dhahabu hasa. Asingeweza kumkosa Beno Kalolanya. Katika mechi zote tatu zilizopita ambazo Mayele hakuziona nyavu za Simba ni kwa sababu hakupata nafasi kama ile.

Baadaye akafunga bao lake la pili wakati mechi ikiwa imefika jioni. Hili ni bao lake halisi, hasa kwa namna ambavyo aliwazuga walinzi watatu wa Simba kabla hajamalizia kwa mguu wa kushoto. Alikuwa amekamilisha ‘hat trick’ yake dhidi ya Simba tangu afike nchini. Lilikuwa bao lake la tatu dhidi ya Simba tangu afike nchini.

Mwisho wa mechi Yanga walitawazwa kuwa washindi wa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo, zote wakiwafunga mahasimu wao Simba. Mechi iliacha majibu machache.

Kwanza ni namna ambavyo Simba waliamua kuwaacha nje wachezaji wake wote wageni isipokuwa mlinzi, Mohamed Ouatarra. Labda waliona kwamba mechi ingekuwa ngumu kwao na walipaswa kuisoma wakiwa nje.

Kwamba kwanza walipaswa kujua ugumu wa Derby wakiwa nje ili kipindi cha pili waje wakijua umuhimu wa mechi. Yanga wao walianza na Aziz Ki tu. Hauwezi kujua kwanini walichukua uamuzi huo. Vyovyote ilivyo haikuathiri kiwango chao uwanjani.

Swali jingine ambalo lilijibiwa katika mechi hii ni ukweli kwamba Aziz Ki alistahili kugombaniwa na timu zote hizi mbili katika dirisha hili la uhamisho wa wasajili. Ni fundi hasa wa mpira. Anajua kukaa na mpira, kutambuka wapinzani na kisha kupiga pasi za mwisho. Mguu wake wa kushoto ni wa dhahabu.

Alichofanya uwanjani kimemshushia presha kutoka kwa mashabiki wa timu zote mbili ambao walikuwa wanasubiri kwa hamu kuona kama anastahili kelele zote ambazo zilikuwa zinapigwa kwake na mitandao ya jamii kuhusu uhamisho wake. Anabakia kuwa mchezaji aliyezungumzwa zaidi katika dirisha hili linalofungwa Agosti 31.

Mwamuzi Heri Sasii naye alikuwa na maswali ya kujibu. Aliitendea vema jioni yake ya juzi. Uamuzi wake katika matukio mengi ulikuwa sahihi kasoro zikiwa ni chache. Inonga anajazwa na jazba za pambano na huenda alistahili kadi nyekundu kwa undava aliomfanyia Sure Boy.

Hata Sure Boy naye angeweza kupewa kadi nyekundu kwa namna alivyojibu mapigo. Hata hivyo, Heri Sasii aliamua kuiweka mechi katika uwiano kwa kutotoa kadi hizo. Siku hizi kitu cha msingi ni kuangalia kanuni na sheria na kutojali zaidi kuhusu ubinadamu.

Bernard Morrison alistahili kupewa penalti, lakini Heri Sasii aliiweka mfukoni kwa sababu Yanga walikuwa wanaongoza mabao mawili na mechi ilikuwa imefika jioni. Kama Yanga wangekuwa wamefungwa angeweza kutoa. Ni kosa la mwamuzi. Unaweza kutoa penalti hata tano katika mechi moja, na wakati mwingine dhidi ya upande mmoja.

Lakini hapo hapo Heri Sasii hakuitendea haki Simba ambayo ilikuwa inasaka kusawazisha bao. Katika dakika nne za majeruhi ambazo aliongeza, Morrison alileta mzaha mwingi wa kupoteza muda.

Hata hivyo, Heri Sasii hakufidia dakika zile katika muda wa nyongeza. Kwanini? Ukweli ni kwamba waamuzi wa kimataifa huwa wanafidia kama kuna mtu kapoteza muda katika dakika za nyongeza.

Mwisho wa yote lilikuwa pambano zuri la soka. Shukrani kwa Simba na Yanga. Lilikuwa pambano ambalo lilikidhi matarajio ya mashabiki. Katika picha kubwa timu zote mbili zilipata pambano zuri kwa kujiandaa na mechi za kimataifa zaidi. Kwa ndani ni wazi kwamba Simba na Yanga zimeimarika zaidi.

Pole kwa Simba kwa sababu najua namna ambavyo wanajisikia. Katika miaka ya karibuni wamekuwa wateja wazuri wa Yanga. Sijui kitu gani kinatokea kwao lakini tangu Yanga wakiwa na timu ya kawaida hadi leo wana timu nzuri wanaonekana kuitawala Simba kisaikolojia hasa ndani ya uwanjani.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz