Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Matola, mbuzi wa kafara asiye na hatia

Seleman Matola Malawi Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola

Wed, 14 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mashabiki wa Simba walikuwa wanaimba kwamba hawamtaki kocha wao wa muda aliyesimamia pambano la Simba dhidi ya KMC mapema wiki iliyopita, Seleman Matola. Ilianza kama mzaha katika miaka ya karibuni, ila sasa baadhi ya mashabiki wanaonekana kuvunja daraja la uhusiano baina yao na Matola.

Swali la kwanza. “Kwanini yeye huwa hang’olewi?” Mashabiki wamekuwa wakistaajabu kwanini Matola amekuwa kocha msaidizi wa kudumu katika timu hiyo. Kwamba makocha wanakuja na kuondoka, lakini Matola amekuwa msaidizi wa kudumu.

Anaweza kuja kocha mzungu na msaidizi wake, lakini Matola naye atakuwa msaidizi wa kocha huyo. Makocha wanapofukuzwa benchi zima la ufundi nalo linafukuzwa. Hata hivyo, Matola anafanikiwa kubaki na kuishika timu kwa muda mpaka atakapokuja kocha mwingine.

Ni kama tu alivyoishika timu kwa muda baada ya kuondoka kwa Zoran Maki. Akaisimamia timu kwa mechi moja halafu akamkabidhi Juma Mgunda. Haya ndio yamekuwa maisha yake katika klabu ya Simba na amekuwa akiifanya hii kazi kwa uaminifu mkubwa.

Kwanini mashabiki safari hii wanataka na yeye aondoke? Ni ngumu kuelewa. Zamani walikuwa wanadhani kwamba labda Matola alikuwa anawafanyia fitina makocha wanaokuja ili waondoke na kisha nafasi apewe yeye. Hata hivyo, siamini kwamba ni kweli kwa sababu Matola mwenyewe hana sifa ya kuwa kocha mkuu kwa sasa. Kuna vyeti anakosa.

Inakuwa ngumu kuamini kwamba anafanya hivyo ili apewe timu na viongozi. Haiingii akilini. Lakini majuzi kilichonishangaza wakati mashabiki wakimzomea na kumtaka aondoke wengine walikuwa wanadai kwamba timu ilikuwa imecheza kiwango kibovu kwa sababu yake.

Ukweli ni kwamba mashabiki wa Simba walikuwa hawajaridhishwa na kiwango cha timu yao tangu mwanzo wa msimu. Ni lini waliwahi kuikubali Simba ya Zoran? Sidhani. Sana sana walichokuwa wanasikia ni kwamba kocha alikuwa anawavuruga. Mara leo hamtaki Victor Akpan, kesho hamtaki Nassor Kapama, keshokutwa hamkubali Joash Onyango.

Ni kweli Simba haikucheza vizuri dhidi ya KMC, lakini Matola alikuwa ametoka kukabidhiwa timu saa 24 tu zilizopita baada ya Zoran kuondoka. Walitegemea abadilishe kitu gani cha ajabu? Kilichotokea ni kwamba mashabiki walikuwa wamepata mpenyo wa kupenyeza hisia zao juu yake.

Ni hisia ambazo wanazo kwa muda mrefu. Kinachoshangaza ni kwamba waliamua kumfanya mbuzi wa kafara bila ya kutafakari baadhi ya mambo. Kwa mfano, wakati Simba ikifika robo fainali ya michuano ya Afrika, Matola alikuwa msaidizi wa wazungu. Mbona hili hawalioni?

Ninachofahamu ni kwamba Matola yuko pale kwa ajili ya kulinda maslahi ya upande wa viongozi dhidi ya benchi la ufundi. Ni kosa la muda mrefu sasa limendelea kufanyika, lakini huo ndio ukweli na ndio utamaduni wa soka la Afrika.

Nafahamu kwamba mabosi wa Simba wanamhitaji mtu ambaye atafikisha hisia zao kwa urahisi kwa benchi la ufundi. Hii ndio kazi ya kwanza ambayo inamuweka Matola katika benchi la Simba. Wakati mwingine inasaidia wakati mwingine haisadii.

Kuna makocha ambao wana vichwa vigumu na mabosi wa Simba wanaona kuna umuhimu wa kuwawekea mtu kama Matola kwa ajili ya kumkontroo pale ambapo anazidisha kufanya mambo ambayo huenda hayana maslahi kwa klabu.

Pale Manchester United kuna utaratibu wa kocha wa kigeni kuwekewa msaidizi mmoja ambaye anaifahamu klabu vilivyo. Kwa mfano kwa sasa katika benchi la Erik Ten Hag amewekwa Steve McLaren ambaye wote tunamkumbuka kwamba aliwahi kuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson.

Kazi nyingine ambayo inamuweka Matola katika benchi la Simba ni kurahisisha mawasiliano ya lugha ya Kiswahili kati ya wachezaji na kocha husika. Kuna wachezaji wetu wazawa ambao hawafahamu lugha ya Kiingereza vema. Matola anatumika kurahisisha ujumbe kwa wachezaji kutoka kwa kocha.

Hata hivyo, kwa sasa mashabiki wa Simba hawataki kuelewa yote haya na wanataka Matola aondoke na mabenchi ya ufundi ambayo yamekuwa yakiondolewa kila uchao katika klabu ya Simba. lilikuwa suala la muda tu kabla ya hali hii kufikia.

Mioyo ya mashabiki imekuwa ikisaka mchawi. Msimu uliopita Simba haikuambulia taji lolote kubwa nchini zaidi ya kutwaa taji la Mapinduzi Januari mwaka jana pale Unguja. Baada ya hapo wakawa na msimu mbovu ikiwemo kutolewa katika michuano ya Shirikisho.

Msimu huu umeanza vibaya kwao kwa kufungwa na mtani wao wa jadi Yanga. Hawataki kuangalia msimamo wa ligi ulivyo. Licha ya kuongoza ligi (kabla ya mechi za jana), lakini kipigo cha Yanga kimewauma. Ni kipigo cha pili mfululizo baada ya Fei Toto kuwazamisha Mwanza katika fainali za Shirikisho.

Kipigo cha pambano la Ngao ya Jamii kinawauma watu wa Simba na lilikuwa suala la muda tu kabla ya kuanza kumsaka mchawi. Bahati nzuri mashabiki wa soka siku hizi wanawaheshimu viongozi wao tofauti na hali ilivyokuwa zamani.

Wapo ambao walihojiwa siku ile wakaonyeshwa kutoridhishwa na mtendaji wa klabu, Barbara Gonzalez, lakini wengi zaidi waliamua kumtoa Matola kuwa mbuzi wa kafara. Kwao lilikuwa jambo rahisi kumtoa kafara Matola kuliko uongozi. Kwao lilikuwa jambo rahisi kumtoa kafara Matola kuliko wachezaji. Ni kwa sababu timu ilicheza vibaya muda mchache tu baada ya Zoran kuondoka.

Kwa vile wengi pia walikuwa hawaridhiki na kiwango cha timu yao chini ya Zoran ni wazi kwamba waliunga mkono uamuzi wa uongozi kuachana na Zoran. Kama wangekuwa wameridhika na uwezo wa Zoran nadhani siku ile wangeugeukia uongozi na kuutukana. Kwa vile waliridhika na uamuzi wa uongozi ndio maana hasira zao wakazihamishia kwa Matola.

Ushauri wangu binafsi kwa Matola ni kumuomba tu apumzike kwa muda katika nafasi hiyo. Hii ni kwa sababu tayari mioyo ya mashabiki imeamua kumtoa kafara. Timu ikishinda kama ilivyoshinda juzi pale Malawi mashabiki watakaa kimya. Timu ikifungwa wataibuka naye. Utakuwa ni mchezo wa kumsaka mchawi kila timu inapofanya vibaya na jibu lao litakuwa rahisi tu, “Mchawi wetu Matola”.

Heshima pekee kwa Matola itarudi pale ambapo atajiweka kando halafu timu itafanya vibaya. Pale ndipo mashabiki watakapokumbuka kwamba adui yao sio Matola. Wataanza kusaka sababu nyingine. Muda si mrefu atarudi tena klabuni huku mashabiki wakiwa wameshika adabu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz