Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Mapacha walivyotoka pacha Lupaso kwa Mkapa

Dabi Pic Data Beki wa Simba, Achieng akimiliki mpira mbele ya Mayele

Tue, 14 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hatukutazamia iwe hivyo lakini katika mechi ambayo tunamtafuta mchezaji bora wa mechi kupitia safu za ulinzi za timu zote mbili, ni wazi kwamba hautashangazwa kusikia pambano lenyewe la watani lilimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

Watani waliondoka uwanjani bila ya kutupatia walau bao moja la kuanzisha kelele mjini hapa. Kisa cha kutotupatia mabao? Mbili zilikuwa sahihi kwa makocha wa pande zote. Hasa katika maeneo ya ulinzi.

Sababu nyingine ni ukweli kwamba wachezaji wetu walihitaji nafasi nyingi kufunga. Kwa mfano, labda Khalid Aucho alihitaji nafasi nyingine kufunga kwa kichwa kona murua aliyopoteza kipindi cha kwanza. Labda Fiston Mayele alihitaji nafasi nyingine kufunga baada ya kupoteza nafasi yake pindi shuti la Fei Toto lilipombabatiza mlinzi mmoja wa Simba na mpira kumwangukia yeye.

Labda John Bocco alihitaji nafasi nyingine wakati mpira ulipomrudia kufuatia kipa Djigui Diarra kupangua shuti kali la Sadio Kanoute. Wote wawili, Mayele na Bocco hawakuwa wameotea pindi mipira ilipowafikia. Walipoteza tu umakini wa kutumia vyema nafasi chache zilizojitokeza katika nafasi hiyo.

Vinginevyo katika maeneo ya ulinzi timu zote zilifunga vyema milango yao. Simba walikuwa na nidhamu ya hali ya juu. Katikati walisimama vyema, Josh Onyango ambaye alimdhibiti vyema Fiston Mayele.

Yanga walikuwa wanapiga pasi nyingi eneo la ulinzi na kiungo na baada ya hapo wanapiga mipira mirefu iliyowaacha Mayele na Onyango wakipambana. Ni mara moja tu Mayele alimzidi ujanja Onyango. Akampitisha tobo na kutokea upande wa pili. Onyango akamzuia kwa mikono na kupewa kadi ya kwanza ya njano. Mara nyingine zote Onyango aliibuka shujaa. Kama angepitwa Mayele alikuwa anakwenda kutazamana na kipa.

Kilichonishangaza ni wakati Mayele anatolewa nje. Henock Inonga alikwenda naye mpaka nje na kutoa ishara kwamba alikuwa amemdhibiti vya kutosha. Haikuwa kweli. Sifa zilipaswa kwenda kwa Babu Onyango ambaye binafsi naamini alikuwa mchezaji bora wa pambano la juzi. Vinginevyo katika kipindi cha kwanza kocha wa Simba alikuwa amekipanga kikosi chake kijeuri. Alitaka kasi zaidi kikosini na kujikuta akiwa amewapanga Hassan Dilunga, Kibu Dennis na Bernard Morrison nyuma ya mshambuliaji pekee Meddie Kagere. Rally Bwalya aliwekwa nje kwa sababu ana ufundi mwingi lakini sio mwepesi.

Kulikuwa na nafasi iliyokuwa inatafutwa kati ya viungo wa Yanga, Aucho na Yannick Bangala na walinzi wao Dickson Job na Bakari Mwamunyeto. Ilipatikana mara chache nafasi hiyo kutokana na utundu wa Morrison lakini Job akaishia kumchezea rafu. Dilunga alikuwa kimya muda mwingi licha ya kuibuka shujaa katika pambano dhidi ya Red Arrows.

Kipindi cha pili akaingia Bwalya ambaye alikwenda kuchukua nafasi ya Morrison eneo la katikati halafu Morrison akaenda kupimana ubavu na Kibwana Shomari. Ilikuwa vita nzuri na ya kusisimua. Dakika hii angeshinda huyu dakika iliyofuata angeshinda mwingine. Ilikuwa ni tofauti wakati Kibu alipokuwepo uwanjani. Upande wa pili achilia mbali kesi ya Mayele na Onyango kulikuwa na kesi nyingine mbili. Upande wa kulia wa Yanga, Jesus Moloko na Mohamed Hussein Tshabalala walidhibitiana. Moloko alikuwa na kasi kulisaka lango la Simba akamkuta Tshabalala akiwa imara. Lakini Tshabalala alijikuta akikosa muda wa kwenda kuishambulia Yanga kama ilivyo kawaida yake.

Upande mwingine ulinishangaza. Saido Ntibanzokonza alikuwa na kipindi cha kwanza cha ovyo. Alidhibitiwa kwa urahisi na Shomari Kapombe. Aliporudi kipindi cha pili alikuwa wa moto hasa. Ni yeye ndiye aliyelazimisha mashambulizi mechi kuelekea lango la Simba. Ni yeye ndiye alimpeleka majaribuni Aishi Manula kwa shuti kali ambalo liliporudi lilimkuta Mayele ameotea. Eneo la kiungo kulikuwa na Vita ya Fei Toto na Jonas Mkude. Fei alikuwa na jukumu la kumpita Jonas na kufanya mipango. Jonas alijikuta akicheza faulo mara nyingi zaidi. Wakati yeye akiwa katika hali hiyo, pacha wake wa juzi, Kanoute alikuwa aking’ara kwa kazi uwanjani. Alikaba vyema na kusambaza mipira vizuri.

Mwamuzi Herry Sasii hakuwa na wakati mgumu juzi. Ilimsaidia. Kwanza kabisa wachezaji hawakuchezeana rafu mbaya za ovyo. Waamuzi husaidiwa kazi zao vizuri na wachezaji. Wachezaji hawakuwa na jazba na walionyeshana ufundi zaidi. Hakukuwa na rafu ambayo Sasii angelazimika kujiuliza kutoa kadi nyekundu. Hakukuwa na utata wowote unaohusu bao la kukataliwa au kukubali. Lakini pia hakukuwa na utata wa suala linalohusu penalti. Ni tofauti na waamuzi waliokutana na visanga vya penalti ya Kelvin Yondani dhidi ya Meddie Kagere au ile ya Josh Onyango dhidi ya Tuisila Kisinda. Sasii alijikuta katika mechi laini ambayo inaweza kumpatia mechi nyingine ya Simba na Yanga siku za usoni.

Mwishoni pambano lilimalizika kwa suluhu. Ni suluhu ambayo inashusha pumzi kwa mashabiki wa pande zote mbili. Kila shabiki atakwambia ni afadhali ya suluhu kuliko kufungwa. Ni suluhu tu, hasa hii ambayo mwamuzi alichezesha vizuri ndio ambayo inatoa nafuu mtaani kesho.

Lakini nafuu zaidi ilipatikana kwa wachezaji wenyewe. Ungeweza kuona wachezaji wa pande zote mbili wakihisi nafuu katika sura zao. Bora sare kuliko kufungwa. Lakini hapohapo ndipo ungegundua kuwa kumbe Yanga na Simba ni kama timu moja. Wachezaji kuna mahala walikuwa pamoja au kukutana pamoja. Kagere na Aucho waliongea sana. Kisa? Walicheza Gor Mahia pamoja. Kanoute na Diarra waliongea. Kisa? Wanatoka taifa moja la Mali na walicheza pamoja kikosi cha timu ya taifa ya vijana cha Mali. Bahati iliyoje kwao kutoka Afrika Magharibi na kukutana Tanzania. Inatokea mara chache.

Rikizi Siwa, kocha wa makipa wa Yanga aliongea sana na Onyango. Wote wawili ni Wakenya. Wanajuana zamani. Rafiki yangu, Emmanuel Jurgen Malima anapenda kuuita Uwanja wa Mkapa kwa jina la alikotoka, Lupaso. Nami nauita hivyohivyo. Lupaso. Hakukuwa na mbabe juzi katika dimba la Lupaso. Mapacha walitoa sare pacha. Mpaka wakati ujao tena.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz