Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Mambo mawili Mayele anayotufunulia sasa

Mayelee Tetema Mambo mawili Mayele anayotufunulia sasa

Tue, 12 Apr 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mabao ya Fiston Mayele yanasisimua. Hajafunga mabao mengi kuliko kina John Bocco na wengineo. Labda kwa sababu pia hajacheza miaka mingi nchini. Lakini mabao yake machache aliyofunga yamekuwa ya kusisimua.

Staili yake ya kushangilia pia imekuwa gumzo nchi nzima. Ameleta kitu kipya msimu huu.

Baada ya kila kitu mabao yake yameleta vitu tofauti ambavyo wengine tunajifanya hatuvioni wala hatutaki kuzungumzia. Inaanzia katika klabu yake yenyewe na taifa zima kwa jumla yake. Kuna mambo mengi yapo nyuma ya pazia lakini tunayakalia kimya.

Kwa mfano, mabao ya Mayele yamesababisha watu wa Yanga wapunguze chuki kwa TFF. Misimu mitatu yote iliyopita Yanga walikuwa wanalia na TFF na Bodi ya Ligi wanaipendelea Simba. Mayele amekuja kufunga mdomo huo kiurahisi kabisa.

Kwa kuanzia Yanga hawakuwa na timu nzuri kuliko watani wao. Lakini duniani timu zote kubwa na nzuri huwa zina mshambuliaji anayejua kucheka na nyavu. Mshambuliaji atakayeleta tofauti ndani ya klabu yake na katika msimamo wa Ligi Kuu. Ndicho ambacho Yanga walikuwa wanakosa.

Hivi Yikpe alifunga mabao mangapi na yakawa yanakataliwa na waamuzi? Baadaye alikuja mtu anayeitwa David Molinga ‘Falcao’. Yanga walikuwa wanajifariji tu lakini hakuna mshambuliaji wa kisasa anayeweza kuwa na kilo zile kisha akasumbua mabeki. Hakuna. Alikuwa anafunga kwa sababu Yanga lazima ifunge mabao kwa namna yoyote ile.

Jaribu kufikiri namna Molinga alivyoonekana mshambuliaji muhimu Yanga kiasi, akaanza kuringa. Ilitokana na ukosefu wa mastaa kikosini. Wakati huo huo Simba walikuwa na Meddie Kagere na John Bocco. Bado Yanga walikuwa wanaamini walikuwa wanaonewa na TFF.

Baadaye akaja Michael Sarpong. Alifunga mabao mangapi yaliyokataliwa mpaka Yanga wakatengeneza hoja walikuwa wanaonewa na TFF? Alikuwa na umbo zuri, lakini hatukuwahi kujua ubora wake ulikuwa wapi hasa. Atakumbukwa zaidi kwa kutuliza katika ile penalti yake dhidi ya watani baada ya Tuisila Kisinda kuchezewa rafu na Joash Onyango.

Kuna washambuliaji wamepita hapa katikati ni vigumu kudai Yanga walikuwa wanaonewa. Sio tu washambuliaji, lakini kuna vikosi vimepita hapa Yanga ni ngumu kuhalalisha Yanga walikuwa wanaonewa sana na waamuzi au TFF.

Tangu walipompoteza Heritier Makambo aliyekwenda AC Horoya ya Guinea, Yanga haikupata mshambuliaji wa maana ambaye angeweza kuuweka mpira katika wavu achilia mbali kikosi ambacho kingeweza kuweka shinikizo kwa waamuzi wawe upande wao.

Shukrani kwao kwa kujitokeza watu wa GSM ambao walau wamepambana kurudisha heshima ya Yanga na kuwanunua watu kama kina Mayele na wengineo ambao wana hadhi ya Yanga. Lakini walau sasa unaweza kuumiza kichwa kama ukiamua kupanga kikosi cha pamoja cha mastaa wa Yanga na Simba.

Hauwezi kupanga kikosi hicho kwa sasa ukawaacha nje mastaa kama Mayele, Khalid Aucho, Yannick Bangala na wengineo. Bado wakati ulipokuwa unaamini hakuna mchezaji wa Yanga anayeweza kuingia katika kikosi cha kwanza cha watani wao bado Yanga walilalamika wanaonewa.

Mchezaji kama huyu Mayele ametufunulia tu Yanga haikuwa na timu ya maana ambayo ingemfanya mtani akune kichwa. Haikuwa na timu ya maana ambayo ingeitoa TFF katika lawama. Huu ni ukweli ambao kwa sasa hauzungumzwi na watu wa Yanga. Pia kuna kitu Mayele ametufunulia. Mpira wetu una safari ndefu. Jaribu kufikiria ambavyo nchi nzima inamuimba. Kila shabiki anamuota. Lakini Mayele hayupo katika kikosi cha DR Congo. Majuzi Wacongo walikuwa wanajaribu kufuzu kwenda Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Mayele alikuwa Kigamboni katika kambi ya Yanga.

Hatujui kama Wacongo wanafahamu wana mtu wao hatari anayeimbwa na nchi nzima. Hatujui. Tangu afike nchini Mayele hajawahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa. Umewahi kuwaza kama Mayele angekuwa Mtanzania? Angekuwa na nafasi ya kudumu katika kikosi chetu.

Lakini umewahi kuwaza kama kuna Mtanzania angekuwa anaongoza kwa kufunga mabao katika Ligi fulani yoyote nyingine duniani. Lazima tungepiga kelele aitwe. Wacongo wana kina Mayele wangapi? Hapa ndipo tuone uhalali wa kipigo walichotupa katika uwanja wa Taifa katika mchakato wa kufuzu kombe la dunia.

Kuna Wacongo wanaotamba Congo na hatuwajui. Ni kama tulivyokuwa hatumjui Mayele. Pia kuna Wacongo wanaotamba Afrika katika klabu mbalimbali kubwa na ndogo. Na kuna Wacongo wanaotamba Ulaya kama kina Cedric Bukambu na wengineo. Halafu kuna Wacongo ambao wamezaliwa nje ya nchi yao na kukulia ughaibuni. Hapa kuna Wacongo wa aina mbili. Kuna waliozaliwa na wazazi wa Kicongo na kuna wengine ambao mzazi mmoja ni Mcongo na mwingine sio Mcongo. Wengine ndio kina Romelu Lukaku wanaoamua kucheza nje.

Kufikia hapa Congo inakuwa na idadi kubwa ya wachezaji kiasi cha kumsahau Mayele. Kuna kazi ya kufanya kuweza kupambana na taifa kama hili. Haishangazi kuona wachezaji wanaomfukuzia Mayele kwa ufungaji wote wameitwa timu ya taifa. Kina George Mpole wa Geita Gold na Reliant Lusajo wa Namungo.

Sio tu Mayele ambaye anakosekana katika kikosi cha Congo. Wachezaji wote wa Congo wanaocheza Yanga wangeweza kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars na wakacheza bila ya tabu. Lakini kwao wamekosekana na bado mambo yanasonga. Kuna umuhimu wa kuzalisha wachezaji wengi hapa nchini. Bwawa limepungua samaki kwa kiasi kikubwa. Wenzetu mabwawa yao yamejaa samaki na wana uwezo mkubwa wa kuwavua na kisha wengi wakapotelea majini bila ya kuwatia hofu.

Columnist: Mwanaspoti