Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Macho manne sakata la Aziz Ki

Aziz Ki Yanga Dar Macho manne sakata la Aziz Ki

Tue, 19 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Afadhali habari ya mchezaji anayeitwa Stephane Aziz Ki imefika mwisho. Ilianza kama masihara halafu mwisho ikakamata nchi. Ungeweza kudhani dunia ina mchezaji mmoja tu mahiri anayeitwa Stephane Aziz Ki. Unaweza kudhani yupo katika kiwango cha kina Lionel Messi.

Hata hivyo, unasemehe kwa sababu tupo katika nchi ambayo mitandao ya kijamii imeshika kasi. Mashabiki nao wameanza kuwa waandishi wa habari. Watanzania wanakesha mitandaoni na labda ndio maana Yanga walimtangaza Aziz Ki usiku wa manane. Wanajua homa yetu.

Sakata lake limenitafakarisha mambo mengi. Aziz Ki alicheza vyema mechi mbili za ASEC Mimosas dhidi ya Simba. Alifunga mabao mazuri. Alionyesha kipawa maridhawa. Simba na Yanga zote zikaingia katika mbio za kumtaka. Kuna mahala Yanga waliwazidi Simba ujanja.

Rais mpya wa Yanga, Injinia Hersi Said alisafiri hadi Morocco kwenda kumtazama Aziz KI akicheza dhidi ya Berkane. Akafanya naye mazungumzo mazuri. Akajenga urafiki na mchezaji. Wakati huo ilionekana kama vile Simba walikuwa bize na mchezaji anayeitwa Victorien Adebayor wa US Gendarmerie.

Urafiki wa Injinia Hersi na Aziz KI ulikuwa kiini kikubwa cha staa huyo wa Burkina Faso kusajili Yanga, huku wakisaidiwa na staa mwingine wa Burkina Faso waliyenaye kikosini, Yacouba Songne. Baadaye Simba walipomkosa Adebayor wakarudisha nguvu kwa Aziz Ki, lakini walikuwa wamechelewa. Tayari Hersi alikuwa amekutana na mchezaji huyo pamoja na mama yake Dubai na wakamaliza dili.

Ambacho Simba na kundi kubwa la mashabiki wa Yanga walikosa uhakika kuwa Yanga wameinasa saini ya Aziz Ki ni ukweli mchezaji huyo bado alikuwa ana mkataba na ASEC Mimosas na isingekuwa rahisi kwa Yanga kutangaza mapema wameinasa saini yake. Wangeweza kushtakiwa na Fifa kwa kumsaini mchezaji ambaye alikuwa na mkataba na timu yake.

Ambacho hakinishangazi ni namna ambavyo klabu zetu zimeendelea kuingia vitani kwa mchezaji ambaye wamemwona kwa sababu amecheza vyema dhidi ya mmoja wao. Kama ASEC isingekuwepo katika kundi la Simba ni wazi leo Aziz Ki asingekuwepo nchini. Kumbe ni mchezaji mzuri tu. Mfumo wetu wa kuskauti wachezaji upo chini.

Kina Jose Luis Miquissone walipatikana kwa namna hii. Kama Simba wasingecheza na UD Songo si ajabu Miquissone tusingemwona nchini. Ni nadra kupata wachezaji wazuri kwa mfumo ambao Yanga waliutumia kumpata Morrison au Simba walivyotumia kumpata Pape Ousmane Sakho.

Kinachonishangaza ni namna ambavyo baadhi ya kundi kubwa la mashabiki wa Simba limeanza kunyongea kabla ya ligi kuanza. Kuna mambo mawili hapa. Angalia jinsi Simba walivyoupokea usajili wa Habib Kyombo klabuni mwao. Wengi waliuponda kwa sababu Yanga walikuwa wametoka kumtangaza staa wa zamani wa Newcastle United, Gael Bigirimana.

Kabla ya hapo Yanga walikuwa wametoka kumtangaza Lazarious Kambole ambaye anatokea Kaizer Chiefs. Kisaikolojia Yanga wakajikuta imara na kuanza kuzomea usajili wa Simba. Bahati mbaya Simba hawakuwa imara na wakajikuta wakikebehi uhamisho wao wenyewe.

Haikushangaza ndani ya saa 24 zijazo Simba wakalazimika kumtangaza kiungo wa Nigeria, Victor Akpan kwa ajili ya kuwapoza mashabiki wao ambao wanaamini Kyombo hakuwa mchezaji wa maana. Binafsi naamini Kyombo atawashangaza mashabiki wa Simba msimu ujao.

Jaribu pia kuangalia. Ukimtazama mchezaji kama Augustine Okrah ni wazi anaonekana kuwa fundi. Namba zake hazidanganyi. Ukitazama video zake zinakuonyesha Simba wamelamba dume. Inawezekana ni kama tu ambavyo Yanga wamelamba dume kwa Aziz Ki. Tatizo ni Simba hawajawahi kumuona mchezaji wao uwanjani.

Hii ina maana Yanga waliendelea kuusubiri kwa hamu uhamisho wa Aziz Ki huku wakiwakebehi Simba. Hata Simba nao waliendelea kuusubiri kwa hamu uhamisho wa Aziz Ki kwenda Yanga kwa sababu hawakuamini mpaka dakika ya mwisho Aziz anakwenda Yanga. Haishangazi kuona uhamisho wa Aziz Ki umefunika zaidi kuliko wa Okrah wakati kumbe Okrah anaweza kuwa mchezaji mzuri kuliko Aziz Ki.

Baada ya kila kitu, jambo la msingi ni Yanga wamepata mchezaji wa maana na Simba wanaendelea kupata wachezaji wa maana. Hata hivyo, ni nadra kwa Simba na Yanga kung’ara kwa pamoja. Kuna uwezekano dhana hii ikaondoka msimu ujao wakati wote watakapokuwa wanashiriki michuano ya kimataifa?

Yanga kwa sababu ina wachezaji ambao ninawafahamu zaidi naona imeanza kunitisha zaidi. Aziz Ki anaungana na Bernard Morrison na Fiston Mayele katika safu ya ushambuliaji pale Jangwani. Wote wanaonekana tishio na ni wachezaji wenye maarifa mengi katika kushambulia. Lakini nyuma yao Feisal Salum bado yupo.

Mabeki wa kushambulia ambao wataisaidia safu hii ya ushambuliaji ni Djuma Shaban upande wa kulia wakati Joyce Lomalisa atatokea kushoto. Hawa ni Wacongo wawili wanaosifika kwa kushambulia. Maeneo mengine tayari Yanga ina wachezaji bora kama Bigirimana, Khalid Aucho, Yannick Bangala, Sure Boy na wengineo.

Hata hivyo, wana mtihani kweli kweli wa kufika mbali katika hatua zinazofuata za michuano ya CAF. Watu wanataka kuona baada ya mikwara yote hii ya kina Aziz Ki timu yao inaweza kwenda mbali kiasi gani kama ambavyo Simba imekuwa ikifanya katika miaka ya karibuni.

Ni mtihani kwa viongozi wa Yanga kuona kama wamekomaa kwa mbinu za nje ya uwanja. Lakini ni mtihani kwa Kocha Nasreddine Nabi kuona kama anaweza kuiongoza Yanga katika mechi za kimataifa na kufika mbali. Huu unaweza kuwa msimu wake wa mwisho Yanga kama wakitolewa mapema.

Msimu uliopita ungeweza kumsamehe Nabi kwa timu kuondolewa mapema kwa sababu maandalizi ya timu yalivurugika Morocco, pia wachezaji kama Mayele na Aucho walikosa vibali vya kushiriki michuano ya CAF. msimu huu hakuna visingizio kwa Nabi wala viongozi.

Tutarudi hapa kuizungumzia Simba pindi ikikamilisha uhamisho wake. Kwa sasa Simba wanaonekana kuwa na hofu ambayo haijulikani inapotokea.

Labda wanahitaji kushinda pambano lao la kwanza la kufungua msimu dhidi ya Yanga. Huenda upepo ukabadilika haraka.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz