Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Lusajo anajaribu kutuuzia mbuzi katika gunia

Lusajo Pic Lusajo anajaribu kutuuzia mbuzi katika gunia

Tue, 1 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mshambuliaji wetu, Reliants Lusajo hadi sasa anaongoza orodha ya ufungaji, akitupia kambani mabao katika msimamo wa Ligi Kuu ya Bara. Ana mabao 10 na anaonekana kuwa moto msimu huu.

‘Wetu’ namaanisha kwamba ni Mtanzania mwenzetu na sio mgeni. Mchezaji ambaye mara nyingi amekuwa akifanya hivyo ni John Bocco wa Simba. Tumemzoea. Alishafanya hivyo tangu akiwa na Azam FC na sasa ameendelea akiwa na Simba. Anapata huduma nyingi akiwa Simba na inawezekana ni miongoni mwa sababu za yeye kufanya vizuri.

Lakini sasa tunaelekea raundi ya pili na mfungaji kinara ni Lusajo. Idadi ya mabao ambayo amefunga wazungu huwa wanayaita ‘double figure’. Kuna wachezaji wetu huwa wanayafunga, lakini juu yake kunakuwa na wachezaji wa kigeni ambao wanatuburuza. Lusajo amekuwa kinara wa aina yake hasa ukizingatia kwamba anacheza Namungo.

Na sasa imeanza minong’ono mingi kuhusu Lusajo. Inadaiwa kwamba wakubwa wanamtaka. Hapo hapo unawaza. Ni kweli Lusajo ana haki ya kwenda kwa wakubwa kwa sababu washambuliaji wa wakubwa hawafanyi vizuri msimu huu achilia mbali Fiston Mayele anayeendelea kutetema mara nyingi msimu huu.

John Bocco hana bao katika Ligi Kuu hadi sasa. Heritier Makambo hana bao katika Ligi Kuu hadi sasa. Chris Mugalu hana bao hadi sasa katika Ligi Kuu. Lusajo ni jibu sahihi kwao au ni mchezaji wa msimu mmoja (one season wonders) ambaye hatahimili makali akienda kwa wakubwa au ni mchezaji halisi anayestahili?

Wakubwa wanaweza kumnyofoa Mugalu au Makambo au Bocco halafu wakamuamini Lusajo? Ni swali ambalo mashabiki wameanza kujiuliza kimya kimya baada ya kuona Lusajo anawakimbiza mastaa wa timu kubwa katika orodha ya vinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Sio tu kwamba amekuwa akifunga, lakini amekuwa akicheza vizuri na haonekani kubahatisha. Anawatawala mabeki na amekuwa akifunga mabao ambayo sio ya kubahatisha. Anaonekana kuwa mshambuliaji asilia hasa na hata katika timu ya taifa ameanza kuwa na mchango. Kumbuka jinsi alivyofanya kazi nzuri kutengeneza bao la Simon Msuva katika pambano la kufuzu fainali za Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na DR Congo pale Lubumbashi. Wanapokoseka kina Mbwana Samatta huwa tunalaza matumaini kwake kwamba atatubeba vema katika safu ya ushambuliaji.

Kuna mambo mawili. Kwanza kabisa kila anayefanya vema anastahili zawadi au tuzo. Kwa mwanasoka, unapofanya vizuri unastahili mkataba mnono ama ulipo au unapotarajiwa kwenda. Kazi yao ya soka ni ya maisha mafupi sana. Kama Lusajo angekuwa mdogo wangu, halafu anawekewa Shilingi 50 Milioni 50 mezani na wakubwa ningemshauri aende zake. Hajawahi kukamata pesa hizo maishani. Labda kama ana biashara nyingine nje ya uwanja. Huwa tunawalaumu wazawa wanaokwenda Simba na Yanga bila ya kuangalia habari ya maisha binafsi. Kama hakuna timu ya nje iliyoweka kiasi hicho mezani halafu Simba, Yanga au Azam wanaweka kiasi hicho hakuna unachoweza kufanya zaidi ya kupinda mgongo na kusaini karatasi zilizopo mbele yako.

Suala la kucheza au kutocheza litajulikana mbele ya safari. Tatizo ni kwamba kuna pengo kubwa kati ya Namungo na wakubwa. Mpira wetu hauna nafasi ya kuzalisha wachezaji kama kina, Harry Kane ambao wanaweza kucheza Tottenham Hotspurs kwa muda mrefu bila ya kwenda Real Madrid, Man City, Chelsea au Manchester United. Hata hivyo upande wa pili wa nje ya Lusajo unatutisha kidogo. Kuna Wachezaji wengi ambao tuliwashauri kama yeye lakini walipofika Simba au Yanga hawakuendelea kuwa wale wale tena. Hawa ni kina Adam Salamba, Waziri Junior, Charles Ilamfya na wengineo. Hata Yusuph Mhilu ndio ameanza kujitutumua sasa hivi.

Nini kinatokea? Mambo ni mengi. Wengine wanakosa kujiamini kutokana na presha ya ukubwa wa klabu. Wengine pia wanakosa kuaminiwa kwa sababu ya uwepo wa mastaa wengi klabuni. Kwa sasa ni rahisi kumthamini Lusajo akiwa na Namungo kuliko akiwa na Simba au Yanga.

Pale Namungo wenzake wanamuamini. Wamemzunguka na wanajua kwamba ni staa wao ambaye anawabeba. Akikosea hakuna wa kumlaumu sana. Mipira mingi atapelekewa yeye. Nje pia hakuna mashabiki wengi wa kumlaumu na kumkejeli, achilia mbali kumtukana.

Ukienda kwa wakubwa unajikuta katika rundo la mastaa na inaondoa umuhimu wako. Sio lazima kwamba kila mpira upasiwe wewe. Ukikosea unatukanwa na mashabiki hasa kama bado haujatengeneza himaya kwa mashabiki. Kunakuwa na tofauti kati ya kukosea kwa Mayele na kukosea kwa Lusajo. Haya ndio maisha ya timu kubwa.

Wengi wanashindwa kuhimili presha hii. Matokeo yake wanajikuta wakiingia hofu ya kucheza. Lakini zaidi ni kwamba klabu zenyewe haziwapi muda wa kuzoea mazingira yenyewe. Ndani ya msimu mmoja tu unaweza kutolewa kwa mkopo. Kama John Bocco huu ungekuwa msimu wake wa kwanza Simba nadhani angetolewa kwa mkopo mahala. Akienda timu kubwa ataweza kuhimili presha au ndio yatakuwa yale yale ya akina Salamba? Hapa ndipo linapokuja suala la kumuuzia mwanadamu mbuzi katika gunia. Unasikia sauti ya mbuzi akiwa katika gunia. Unamnunua bila ya kufungua gunia. Unakwenda nyumbani na kufungua gunia unakuta kiumbe mwingine au unamkuta Mbuzi mdogo asiyestahili bei husika.

Ni matumaini yangu kwamba Lusajo ataendelea kufanya vema. Lakini kama habari ni kwenda katika timu kubwa basi bado tuendelee kusubiri kidogo. Aliwahi kucheza Yanga ya vijana lakini hadithi ya leo ni tofauti na ya zamani. Leo Yanga watahitaji mchezaji aliyekamili kimwili na kiakili aingie katika timu moja kwa moja.

Lakini hatuwezi kujua. Huenda pia tukawa tumempata mrithi wa John Bocco katika soka letu la ndani. Katika miaka ya karibuni kuna wachezaji wengi wa nafasi tofauti ambao wanatamba katika timu kubwa lakini katika eneo la ushambuliaji anayetamba ni Bocco tu. Labda Lusajo anaweza kuwa mrithi sahihi wa Bocco. Hatuwezi kujua.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz