Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Kutoka Misri, Azam wameng'ata meno kwa hasira

Azammmmmm Benchi la Ufundi Azam FC msimu ujao

Tue, 9 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ghafla akajitokeza Yusuf Bakhresa, mmoja kati ya matajiri wa Azam FC na kuanza kununua wachezaji mastaa kikosini. Ilikwenda mbali zaidi kwa Yusuf mwenyewe kuonekana katika picha wakati Azam ikisaini wachezaji. Yaani mchezaji anasaini, Yusuf yupo kando halafu Mtendaji wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ naye anakuwa kando.

Mara nyingi watu wa familia ya Bakhresa huwa hawapendi picha zao kuonekana hadharani achilia mbali mitandaoni. Mzee mwenyewe, Said Salim Bakhresa watu wamekuja kuijua sura yake baadae sana. Walisikia jina mara nyingi lakini hawakujua anafanana vipi.

Kwa Yusuf kuonekana hadharani katika mitandao katika staili ile wengi tulifahamu ilikuwa imebeba ujumbe kwamba safari hii Azam hawataki masikhara tena.

Safari hii kina Bakhresa hawataki masikhara na wamekwenda mbele wenyewe kuonyesha wanaudhamiria msimu mpya kwa hasira.

Matokeo yake imeleta vifaa vipya vya maana kama Tape Edinho, Kipre Junior, Cleophas Mkandala, Isah Ndala, James Akaminko, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Nathaniel Chilambo, Ali Ahamada na Malickou Ndoye

Niliamua kusafiri mpaka Misri ambapo Azam imeweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya. Ukweli ni kwamba dhamira ya maandalizi yao ya usajili vimeendana na dhamira ya kambi yao iliyopo hapa Misri. Azam ina kila kitu. Inaonekana kuwa na jambo lake msimu ujao.

Imefikia katika hoteli nzuri ya kifahari katika mji mdogo unaoitwa El Gouna. Huu mjini upo ndani ya mkoa unaoitwa Urghada. El Gouna ni mji wa kifahari hasa ambao umetengwa kwa ajili ya watu wenye fedha. Kuna hoteli nyingi za kifahari na ni mji ambao umepangiliwa vema. Watalii wengi kutoka pande mbalimbali za dunia hasa Ulaya na Marekani wamefurika katika hoteli hizi.

Azam imeweka kambi katika moja kati ya hoteli hizi za kifahari. Hoteli yao inaitwa Cook. Imechukua vyumba 25 na chumba kimoja kinalipiwa dola 157 za Marekani kwa siku moja. Hizi ni sawa na shilingi za Tanzania 365,000. Imekaa hapa kwa wiki mbili na unaweza kuona ni kiasi gani cha pesa imetumia kwa uwepo wake hapa.

Uwanja wa mazoezi ni mmoja kati ya viwanja vinavyotumiwa na Klabu ya Gouna ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Misri. Gouna ni timu ambayo straika wa Azam, Idris Mbombo alikuwa anaichezea kabla ya kutua Azam. Ina maana katika kitongoji hiki cha Gouna, Mbombo ndiye mtu pekee mwenyeji katika msafara wa Azam.

Uwanja huu ambao Azam inafanyia mazoezi unaweza kuwa topiki ya siku nyingine lakini kifupi tu unatafakarisha. Wamisri wapo Jangwani. Nchi yao ni kavu lakini viwanja vyao vyote ni vya hali ya juu. Uwanja laini, wenye nyasi nzuri kama za viwanja vya Ulaya. Wenzetu wapo makini na maisha yao ya michezo.

Lakini Azam imepata wasaa mkubwa wa kutumia gym na mabwawa ya kuogelea pamoja na huduma mbalimbali ambazo klabu halisi ya mpira wa miguu inapaswa kupata. Zaidi pia ilipata muda mzuri wa kujiandaa.

Na baada ya mazoezi haya kukamilika, Kocha wa Azam, Abdihamid Moallin anakaa katika presha kubwa na benchi lake la ufundi ambalo lina kila mtu na limekamilika. Nilichojua huu unaweza kuwa msimu ambao utaamua hatima yake baada ya kumaliza fungate lake na Azam msimu uliopita.

Nilichokisoma kutoka kwa matajiri wa Azam na mabosi waliopo hapa wanaamini kuwa hiki kinaweza kuwa kikosi bora cha Azam tangu kiliposambaratika kile cha kina Kipre Tchetche, Kipre Balou, John Bocco, Himid Mao, Shomari Kapombe na wengineo.

Mabosi wanataka Azam irudie makali yale na kutwaa ubingwa msimu ujao huu unaoanza bila ya kujali Simba na Yanga zimesajili kina nani. Wana haki hiyo. Presha ipo kwa Moallin kutoa matokeo bora. Kitu cha kwanza ambacho kitamuuma katika kichwa chake ni namna ya kupanga kikosi bora kinachoanza.

Azam imerundika mastaa katika kila eneo. Katika kila nafasi kuna wachezaji bora. Kwa mfano katika eneo la ushambuliaji kuna washambuliaji wanne. Hiki ni kitu nadra katika soka la kisasa. Kuna Idris Mbombo, Prince Dube, Rodgers Kola na mzawa wetu Shaban Chilunda.

Bahati mbaya kama utaharibu katikati hauwezi kupelekwa pembeni kwa sababu na huko Azam imesheheni. Pembeni Abdul Suleiman ‘Sopu’, Ayoub Lyanga, Idd Seleman ‘Nado’, Ismail Aziz Kader, Tepsie Evans, lakini zaidi kuna Kipre Junior ambaye ametamba katika Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita na alikuwepo katika kikosi cha msimu kama ilivyo kwa Aziz Ki wa Yanga.

Huo ni mfano tu wa namna Azam ilivyosheheni. Lakini katika kila eneo imesheheni vivyo hivyo ukipata nafasi ya kuanza katika kikosi cha sasa cha Azam inabidi uitendee vema nafasi yako. Vinginevyo itakuwa vigumu kwa mchezaji kuirudisha nafasi yake kwa haraka.

Wachezaji walionivutia machoni ni wengi lakini kiungo, Tape Edinho atawashangaza wengi. Ana kipaji kikubwa ambacho kitafunika majina la wachezaji wanaojiona wakubwa ambao wamenunuliwa na Simba na Yanga katika dirisha hili la uhamisho.

Najua namna ambavyo magazeti yamekuwa yakiwafuatilia kwa karibu wachezaji wapya wa Simba na Yanga kuliko wa timu nyingine.

Lakini kuna huyu Kipre Junior. Anakuja kurithi jina la Kipre pale Azam. Ana kipaji kikubwa na uwezo wake wa kukokota mipira ni wa kipekee. Itakuwa majanga kwa mabeki wengi wa ligi kuweza kukabiliana naye mara kwa mara. Tusubiri na kuona.

Lakini hatuwezi kusubiri na kuona kwa wachezaji hawa tu. Inabidi tusubiri na kuona kutoka kwa timu nzima. Wachezaji wa Azam inabidi wajipe presha wenyewe. Presha ya kupata matokeo katika kila mechi. Kule Simba na Yanga wachezaji wanapewa presha zaidi na mashabiki. Azam haina mashabiki wa kutosha kama Simba na Yanga. Inabidi wajipe wenyewe.

Hauwezi kusema haiwezekani wakati kina John Bocco waliwahi kufanya hivyo na kuipa timu yao ubingwa wa Ligi Kuu.

Baada ya hapo wamewahi pia kutwaa mataji mengine. Kwanini ionekane kama haiwezekani? Inawezekana. Ubora upo. Nimeuona kwa macho yangu hapa Misri. Kila kitu kilichofanywa na matajiri kimeashiria kama vile wameng’ata meno kwa hasira.

Columnist: Mwanaspoti