Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Kuna sababu lukuki za Yanga hii kunyanyua makwapa msimu huu

Ubingwa Ligi Kuu Yangaaa Yanga wakiwa na Kombe la Ubingwa 2021/2022

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nchi nzima juzi jioni zilijaa picha za Yanga wakiwa wanashangilia mbele ya kombe lao. Imepita miaka mitano sasa tangu walipofanya hivyo. Kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Huwa inatokea mara chache kwa Yanga au Simba kukaa kipindi kirefu cha namna hii.

Kuna sababu za msingi za Yanga kuchukua ubingwa huu mbele ya rafiki zao Simba. Awali haikutabirika kama Simba wangepotea mapema hivi. Haji Manara akiwa Simba aliwahi kutabiri kwamba Simba ingechukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara kumi mfululizo.

Ungeweza kudhania masihara, lakini wakati mwingine ungeweza kuhisi lilikuwa jambo linalowezekana. Kwa mfano wakati ule Yanga wana David Molinga katika safu ya ushambuliaji halafu Simba wana Chris Mugalu, John Bocco na Meddie Kagere. Jaribu kufikiria kwamba huyo huyo Molinga alikuwa anawaringia Yanga.

Ungeweza kudhani lingekuwa jambo la kweli kwa sababu wakati fulani Aishi Manula akisaidiana na Beno Kalolanya kama ilivyo sasa, Yanga walikuwa na kipa anaitwa Kindoki. Msaidizi wake alikuwa Ramadhan Kabwili. Ungeweza kudhani kwamba lilikuwa jambo la masihara kudhani Simba ingechukua kwa miaka kumi mfululizo. Lakini kama hali kwa Yanga ingebaki ile ile basi hakuna ambalo lingeshindikana.

Juzi kulikuwa na hitimisho la hadithi hii Mbeya. Yanga wamenyanyua kombe. Zipi zinaweza kuwa sababu za ndani ya uwanja? Nje ya uwanja najua kunaweza kuwa sababu zake lakini ndani ya uwanja Yanga pia walitibu matatizo yao ya msingi ambayo yameipa hadhi ya ubingwa.

Inawezekana watani wao Simba wangeweza kuwa bora kwa mara nyingine msimu huu na wakatwaa ubingwa kwa mara nyingine, lakini naamini kwamba Yanga walikuwa na ubora wa kukimbizana na Simba mpaka wikiendi ya mwisho ya kufungwa na ligi tofauti na misimu minne iliyopita.

Tatizo la kwanza ambalo Yanga walitibu ni kupatia usajili wa wachezaji wengi wazuri. Inachosha kurudiarudia, lakini wamesajili vizuri kwa kuwachukua Fiston Mayele, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Sure Boy, Djuma Shaban na wengineo.

Lilikuwa kundi ambalo limewapa ubora, pia imewapa machaguo. Kwamba mchezaji ambaye angeweza kukosekana halafu likawa pigo kubwa ni Mayele tu. Mastaa wengine wamekosekana lakini timu ilikuwa katika mwendo mdundo. Yanga ni kati ya timu zilizoathiriwa na majeraha msimu huu.

Eneo la katikati la Yanga walikuwa na Aucho, Saido Ntibazonkiza, Fei Toto, Yannick Bangala, Zawadi Mauya, halafu akaja Sure Boy. Watatu wowote ambao wangeanza bado eneo lilikuwa bora. Hawakuwahi kuwa na kitu kama hivi kwa misimu mingi sasa.

Wakati mwingine walisaidiana matatizo ya uwanjani. Kibwana Shomari mara nyingi amecheza kama beki wa kushoto. Dickson Job mara kadhaa amecheza kama beki wa kulia. Farid Mussa mara kadhaa amecheza kama beki wa kushoto. Walicheza nafasi hizi kwa ufasaha kwa sababu ya ubora wao.

Tatizo la pili ambalo Yanga walitibu ni kutokukosea kusajili katika nafasi ya ushambuliaji. Ni kweli kwamba usajili ni bahati nasibu, lakini Yanga walikosea mara nyingi katika madirisha waliyopita. Walikosea halafu wakakosea, halafu wakakosea tena na tena. Kuanzia kwa kina Yikpe, David Molinga, Michael Sarpong Yanga walionekana wanakosea.

Walipofika kwa mtu kama Fiston Mayele ikaonekana kama vile Yanga wametibu moja kati ya matatizo makubwa yaliyokuwa yanawakabili. Ni ngumu kwa soka la dunia hii kutwaa ubingwa bila ya kuwa na mshambuliaji tegemeo. Ameweza Pep Guardiola tu na kikosi chake cha Manchester City msimu huu. Vinginevyo ni ngumu.

Unaweza kuwa na mshambuliaji anayefunga mabao mengi bila ya timu yake kutwaa ubingwa. Ni kama vile Harry Kane wa Tottenham. Ni kama vile George Mpole na Geita Gold yake. Lakini ni ngumu kwa timu zetu kutwaa ubingwa bila ya kuwa na mshambuliaji wa uhakika.

Lakini pia ujio wa kipa, Djigui Diarra uliwahakikishia Yanga kwamba lango lao lipo salama. Kipa wa mwisho wa uhakika kidogo katika lango la Yanga alikuwa Beno Kalolanya. Vinginevyo Yanga walikuwa katika mawimbi makubwa langoni mwao hapo awali. Hakukuwa na kipa.mwenye mamlaka langoni kama huyu Diarra.

Ghafla Yanga wakajikuta imara katika kila idara. Ushambuliaji, kiungo, ulinzi na katika nafasi ya goli. Mara nyingi timu zote zinazotwaa ubingwa huwa zinakamilika katika kila idara. Sijaona idara yoyote Yanga ambayo haikuwa imekamilika.

Mathalani Simba msimu huu iliangushwa zaidi na safu yao ya ushambuliaji. Kagere, Mugalu na Bocco hawakufunga mabao ya kutosha walipopata nafasi. Kwa Yanga sio Mayele tu, hata Fei Toto na Saido walifanya kazi nzuri katika kuongeza idadi ya mabao.

Kitu kingine ambacho Yanga walipatia ni kutomuondoa kocha wao, Nasreddine Nabi baada ya kutolewa katika michuano ya Afrika pale Nigeria dhidi ya timu iliyoitwa Rivers United. Yanga walipoteza mechi zote mbili dhidi ya timu hiyo changa ya Nigeria.

Lingekuwa jambo rahisi tu kumtupia mzigo Nabi. Imekuwa hivyo kwa klabu zetu kubwa zinapotolewa katika michuano ya Afrika au kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi. Kocha anakuwa muathirika. Hata hivyo, hapa Yanga walikuwa wametumia akili kwa sababu kocha mwingine mpya angeanza upya.

Yanga walikuwa wametolewa na Rivers sio kwa sababu ya Nabi. Ukweli ni kwamba walikuwa na maandalizi mabovu kuelekea mechi hizo mbili kwa sababu ya kambi yao ya maandalizi ya mwanzo wa msimu kushambuliwa na Uviko-19 nchini Morocco. Hadi sasa naamini kwamba Yanga akicheza leo na Rivers basi Wanigeria hao watapoteza.

Hali hayo yakitokea, wapinzani wao Simba walikuwa na msimu mgumu kuanzia nyumbani hadi ugenini. Lakini pia kuondoka kwa Clatous Chama aliyekwenda Morocco na Jose Louis Miquissone aliyekwenda Misri kuliwanufaisha kwa kiasi kikubwa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz