Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Kizunguzungu cha Akpan na kocha Zoran

Akpan Pic Data Kizunguzungu cha Akpan na kocha Zoran

Wed, 24 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simulizi ya Victor Akpan inachekesha kidogo. Inaanzia namna ambavyo Simba ilipompora kutoka katika kucha za Azam ambao pia walikuwa wanamtaka staa huyo kutoka Coastal Union.

Niamini mimi kwamba Simba ilifanya umafia mzuri kwa Azam.

Tayari mchezaji alikuwa anaelekea zake Azam. Akafika hadi Chamazi akiwa na viongozi wa Coastal. Mabosi wa Coastal walikuwa wanataka pesa ya mauzo yake. Azam haikuweza kumaliza shughuli yao na Akpan Chamazi. Wakapanga kwenda kumalizia mjini.

Kina Akpan akiwa wanaelekea mjini Simba wakaingilia kati. Wakaliteka dili kimafia na kumsainisha. Dili lake limeigharimu Simba kiasi cha Sh200 milioni. Hiyo ni pesa kwa mchezaji mwenyewe lakini ni pesa kwa Coastal.

Ilionekana Simba walikuwa wanasaka mtu wa kuchukua nafasi ya Thadeo Lwanga. Kwa viongozi wa Simba kwao lilikuwa dili sahihi kwa mujibu wa macho yao. Walikuwa wamemuona Akpan vizuri katika mechi za Coastal na walikuwa wamejiridhisha na kiwango chake.

Haikuwa mara ya kwanza kwa Simba kumsajili mchezaji wa kigeni ambaye anacheza hapahapa nchini. Waliwahi kufanya hivyo kwa Asante Kwasi na Bernard Morrison.

Kasheshe ilianzia katika kambi yao nchini Misri ambapo Kocha Zoran Maki alidai mchezaji huyo hakuwa katika mipango yake. Sio Akpan tu, nasikia aliwataja wengi hadi Nassor Kapama. Hawa ni wageni ambao mashabiki wa Simba hawajawahi hata kuwaona wakiwa katika jezi ya timu yao.

Namzungumzia zaidi Akpan kwa sababu timu imetumia pesa nyingi kumnasa. Swali la kwanza, mchezaji haingii katika mfumo wa kocha au kiwango chake hakiridhishi? Akpan ni kiungo anayetoka katika boksi la timu yake kwenda katika boksi la adui. Inawezekana Mzamiru Yassin ni bora kuliko Akpan?

Makocha wana maoni tofauti lakini binafsi niliamini Simba walikuwa sahihi kumchukua Akpan. Nimemuangalia katika mechi za Coastal hasa dhidi ya timu kubwa na alionekana kuwa mchezaji hasa.

Alikuwa na nguvu na akili ya mpira. Lakini zaidi alikuwa mchezaji mshindani uwanjani.

Nini kinatokea? Simba wameingia naye mkataba ambao inabidi alipwe pesa nyingi kila mwezi. Kuna klabu nyingine ambazo zinaweza kumtaka lakini je, zitaweza kumlipa mshahara ambao Simba wamempa?

Sidhani hata kama marafiki zangu Coastal wanaweza kumudu wakirudishiwa mchezaji wao. Tunarudi katika mfumo wa usajili. Ni kweli siku hizi katika soka la kisasa viongozi ndio ambao wanasajili wachezaji?

Mkurugenzi wa ufundi ndiye ambaye anasajili wachezaji. Kocha anapewa wachezaji tu. Nadhani kulikuwa na sababu nyingi za Simba kumnasa Kocha Zoran kabla ya kuanza kuwanasa wachezaji.

Labda angepewa mikanda ya Akpan na kumkataa kabla klabu haijaingia hasara ya mamilioni ya fedha. Lakini hata asili ya mkataba wa Zoran na Simba inanipa shaka namna ambavyo kocha huyu anawezaje kuwa na mamlaka makubwa ya kuwaingiza Simba hasara.

Yeye mwenyewe ana mkataba wa mwaka mmoja tu. Kazi yake ipo hatarini kama Simba watatolewa mapema katika michuano ya kimataifa. Vipi akija kocha nwingine ambaye atamkubali Akpan katika klabu yake anayocheza kwa mkopo? Ina maana Akpan anaweza kurudi kikosini na maisha yakaendelea.

Ukirudi kwa Akpan mwenyewe nadhani atakuwa amechanganyikiwa. Sawa amepata pesa lakini tayari kocha amemshusha hadhi yake.

Unadhani Azam wanaweza kumhutaji tena hata kama Simba wakiwa tayari kumpeleka kwa mkopo klabuni hapo? Lakini hapohapo Azam watajihisi wamedharauliwa na mchezaji mwenyewe. Hawawezi kumuhitaji tena.

Vyovyote ilivyo Simba imeshaingia hasara ya kwanza kwa Akpan. Wamelazimika kwenda sokoni kumchukua kiungo mwingine kutoka Nigeria ambaye atatua muda wowote nchini akitokea Nigeria. Ina maana kama Zoran angemkubali Akpan basi staa huyo asingechukuliwa.

Kwa upande wa ndugu yetu Kapama nadhani atakuwa anajisikia vibaya. Namna ambavyo ndoto za wachezaji wetu wa ndani ni kucheza Simba na Yanga, halafu unafika Simba, unasaini, lakini kabla haujaonyesha uwezo wako kocha anakukataa. Ni afadhali kwa wale ambao wamepita miaka ya karibuni na wakavaa jezi kisha wakakataliwa baadaye na mashabiki au viongozi.

Hawa ni kina Yusuf Mhilu, Abdulsamad Kassim na wengineo. Waliwahi walifikia ndoto zao hata kama walicheza kwa dakika chache uwanjani. Kapama atakuwa amevunjika moyo na hasa ukizingatia kocha pia atakuwa amemshusha hadhi kiasi kwamba klabu nyingine kubwa zitapiga chenga kumchukua.

Lakini bado anayo nafasi ya kumuumbua Zorani kama akienda kwingineko na kuonyesha kiwango cha juu hasa katika mechi dhidi ya timu kubwa ikiwemo Simba yenyewe. Wakati mwingine historia za wachezaji wakubwa zinaanzia katika kukataliwa kama hivi.

Wapo wengine waliokataliwa hata kwa vimo vyao. Mwishowe, kwa maamuzi magumu ambayo Zoran amechukua, njia pekee ya kupata mkataba mwingine Simba ni labda kuifikisha Simba nusu fainali ya michuano ya Afrika.

Vinginevyo Simba haitavumilia hasara ambayo atakuwa amewapa katika matukio haya ya akina Akpan. Mara nyingi maamuzi magumu ya makocha huwa yanapewa sapoti na mafanikio yake.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz