Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Kinachomsumbua Mukoko ni alama ya nyakati pale Yanga

Mukoko Pic Kinachomsumbua Mukoko ni alama ya nyakati pale Yanga

Tue, 25 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Katika miaka mitatu iliyopita Yanga imekuwa kama mtoto aliyetambaa, kisha akasimama, na sasa anatembea. Hiki ndicho kinachomsumbua mchezaji anaiyeitwa Tonombe Mukoko kwa sasa. Jina lake linahusishwa kuondoka Yanga.

Mukoko aliitoa Yanga katika kikosi kilichokuwa kinatambaa. Akaisimamisha. Lakini wamekuja watu wengine ambao wanaifanya Yanga itembee. Ni mabadiliko ya alama za nyakati. Hata yeye mwenyewe anaweza kupima.

Mkataba wake umebakiza miezi michache tu lakini watu wa Yanga hawashtuki. Kabla hata mkataba wake haujaisha walikuwa wamepanga kumpeleka TP Mazembe kwa uhamisho wa kubadilishana na winga Chico Ushindi.

Ukiona Yanga wamefikia hatua hii basi hawataki kuwa naye. Nadhani pia hataongezwa mkataba mwishoni mwa msimu. Unaweza kujiuliza imekuaje mchezaji bora wa msimu uliopita ghafla akawa hana nafasi katika msimu ujao ujue timu imekuwa zaidi.

Mukoko alionekana kuwa mchezaji muhimu kwa sababu aliingia katika kikosi dhaifu cha Yanga. Yeye na Zawadi Mauya waliisaidia Yanga kusimama kwa vile nafasi wanazocheza zilikuwa na wachezaji ambao hawakuisaidia sana timu.

Kabla yao kulikuwa na wachezaji kama Papy Tshishimbi ambaye alikuwa anasumbuliwa na majeraha mengi. Lakini pia siku zake za mwisho pale Jangwani alikuwa mchezaji wa kawaida tu. Tshishimbi aliingia kwa kasi Jangwani lakini baadaye akapoa.

Walikuwepo akina Abdulaziz Makame, Mohamed Issa ‘Mo Banka’ ambao licha ya vipaji vyao, lakini walikuwa wachezaji wa kawaida katika timu. Ghafla wakaibuka Mukoko na Mauya na moja kwa moja wakaenda kuchukua nafasi zao huku wakishirikiana na Fei Toto.

Hapo Yanga walikuwa wanaanza kusimama taratibu lakini ukweli ni kwamba bado kulikuwa na pengo kubwa kati yao na Simba ambao walikuwa na kikosi kinachotembea sio kutambaa wala kusimama. Kwa ujeuri zaidi Simba ikamuongeza Rally Bwalya katika kikosi ambacho tayari kilikuwa na kina Clatous Chama.

Yanga waliimarika chini ya Mukoko, lakini msimu huu walipokwenda sokoni wameibuka na wachezaji wazuri zaidi yake. Nilipowaona Khalid Aucho na Yannick Bangala wakicheza kwa mara ya kwanza nilijua kwamba Mukoko na Mauya wangepata wakati mgumu. Na hasa Mukoko.

Ukweli ni kwamba Mukoko ni mchezaji mgumu na anayejituma zaidi uwanjani. Tatizo ni kwamba umiliki wake wa mpira hauko vizuri. Mguso wake wa kwanza wa mpira sio mzuri kulinganisha na Aucho na Bangala. Mbaya zaidi ni kwamba Mauya ni mzuri zaidi katika umiliki wa mpira kuliko Mukoko. Tatizo la Mauya ni kwamba labda hajitumi sana uwanjani.

Kama ambavyo Mukoko na Mauya waliingia moja kwa moja katika kikosi cha kutokana na aina ya wachezaji waliowakuta basi ndivyo ambavyo Aucho na Bangala wameingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza kutokana na aina ya wachezaji waliowakuta.

Mauya amekuwa akicheza kutokana na kuwa mbele ya Mukoko kwa utulivu kwa mpira mguuni. Naambiwa kwamba kocha Nasreddine Nabi anamkubali zaidi. Hata hivyo bahati yake ya kuchezwa imechangiwa pia na uwezo wa Bangala kucheza nafasi nyingi tofauti, lakini pia majeraha ambayo yamekuwa yakiisumbua safu ya ulinzi ya Yanga.

Anapoumia beki yeyote wa kati wa Yanga, Bangala anarudi kucheza nyuma na kuwapisha Mauya na Aucho wacheze eneo la kiungo. Walipokosekana mabeki wote wa kulia wa Yanga, Djuma Shaban na Shomari Kibwana, basi Dickson Job amesogea kulia na Bangala amerudi kuwa mlinzi wa kati akicheza na Mwamunyeto.

Hata hivyo bado nafasi inakwenda kwa Mauya kucheza sambamba na Aucho. Na ni kweli kwamba Mauya ameitendea haki nafasi hiyo kwa kiasi kikubwa. Hii ina maana kwamba kwa sasa Mukoko anaangukia kuwa chaguo la nne katika orodha ya viungo wa chini achilia mbali Fei Toto anayejitanua peke yake pale mbele.

Tatizo kubwa zaidi kwa Mukoko limekuja baada ya Yanga kuamua kuongeza fundi mwingine katika eneo la kiungo. Salum Abubakar ‘Sure’ Boy ambaye naye ana utulivu mkubwa wa mpira mguuni kuliko Mukoko. Na hii inamaanisha kwamba Mukoko anakuwa chaguo la tano katika eneo la kiungo.

Haishangazi kuona watu wa Yanga wala hawashtuki kuona mkataba wa Mukoko umebakiza miezi mitano Yanga na hakuna anayejali. Umewahi kusikia mitandaoni watu wa Yanga wakiwa na hofu kwamba huenda Mukoko akaondoka klabuni kwao?

Umewahi kusoma mahala mashabiki wakisisitiza kwamba lazima waendelee kuwa na Mukoko? Umewahi kuona watu wa Yanga wakiwa na hofu kwamba huenda Mukoko ataenda Simba? wakati ule walikuwa na hofu wakati Simba walipoanzisha uvumi mitandaoni kwamba wanataka kuinasa saini yake.

Kumbe wakati ule ulikuwa wakati ule. Leo Yanga watakuw ana hofu zaidi ukiwaambia Simba wanamnyemelea Bangala au Aucho. Huu ndio ukweli. Hizi ndio alama za nyakati ambazo Mukoko analazimika kuzikubali. Kila kitabu na zama zake.

Naamini mwisho wa msimu huu Mukoko hatakuwa mchezaji wa Yanga. Lakini naamini pia kwamba endapo akisaini Simba au Azam bado mashabiki wa Yanga hawataulaumu uongozi wao ingawa ni kweli kwamba wanampenda mchezaji huyu. Ni kipenzi chao kikubwa.

Tatizo ni alama za nyakati. Sasa hivi Yanga inatembea yenyewe. Wachezaji upoteza umuhimu kikosini pindi wanapokuja wachezaji wengine muhimu zaidi. zipo nyakati ambazo Simba walikuwa wanamuona Shiza Kichuya kama staa mkubwa, lakini alipokuja Luis Miquissone wakajikuta wakitembea zaidi na kuachana na kina Kichuya.

Wakati mwingine huwa inatokea lakini kitu muhimu zaidi ni kuangalia maslahi ya timu. Ipo siku ambayo hata Aucho mwenyewe atapoteza umuhimu pindi atakapokuja mchezaji mkali zaidi yake. Labda kama hatakuja mkali zaidi yake ndipo ambapo ataendelea kuimbwa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz