Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Jezi, biashara tamu kwa mapacha wa Kariakoo

WACHEZAJ JICHO LA MWEWE: Jezi, biashara tamu kwa mapacha wa Kariakoo

Tue, 7 Sep 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

ILIKUWA wiki nyingine ya kusisimua kwa wale mapacha wawili wa Kariakoo. Simba na Yanga. Wameanza nyingine siku hizi. Ligi ya kushindanisha jezi zao. Nani ana jezi nzuri kuliko mwingine. Simba walikuwa wametoa jezi yao na Yanga wakajaa mitandaoni kukosoa.

Vyovyote ilivyo sifa nyingi ziende kwa hawa mapacha wawili. Hatimaye wamefanikiwa kuingia katika biashara nyingine ambayo itadhihirisha ukubwa wao. Zamani biashara hii haikuwepo na bado timu hizi zilijiita kubwa. Hapana walikuwa wanakosea. Wao walikuwa wakongwe tu sio wakubwa.

Timu kubwa Ulaya huwa zinajiendesha kwa mambo matano makubwa. Kwanza ni wadhamini hasa yule mdhamini mkuu anayekaa kifuani. Pili ni mauzo ya haki za televisheni. Tatu ni mauzo ya haki za matangazo. Yanga na Simba wanafaidika kupitia mkataba wa Azam ambao unasimamiwa na TFF. Lakini Yanga wana mkataba wao binafsi wa mabilioni na hawa watu wa Azam.

Vitu vingine viwili ni mauzo ya wachezaji kama ambavyo tumeona kina, Clatous Chama, Luis Miquissone na Tuisila Kisinda walivyoondoka kwa pesa ndefu. Lakini kitu kingine ni mauzo ya jezi na vifaa mbalimbali vinavyoambatana na rangi au nembo ya klabu. Hili la mwisho naona limekuja katika mabadiliko makubwa.

Mabosi wa zamani wa klabu hizi hawakutumia hii fursa lakini leo Yanga na Simba zimewapa watu tenda ya kutengeneza na kusambaza jezi huku klabu zikiingiza mabilioni ya pesa. Hongera nyingi kwao kwa sababu viongozi wa zamani tuliwashauri kuhusu hii fursa lakini waliziba masikio.

Zamani mashabiki wa Yanga walikuwa wanavaa jezi za Brazil, Mamelodi Sundowns au Norwich City kuwakilisha rangi za klabu yao. Ilikuwa aibu. Tatizo klabu ilikuwa haina jezi na si kwamba mashabiki walikuwa hawana pesa. Leo shabiki wa Yanga atakayevaa jezi ya Brazil nadhani ataionea aibu jezi yake.

Huku upande wa Mnyama mashabiki walikuwa wanavaa jezi za Liverpool, Manchester United au Arsenal kwa ajili ya kuwakilisha rangi za klabu zao. Ukweli ni kwamba kwa sasa tabia hiyo inaweza kubakia kuwa historia kwa sababu jezi zipo na zinajulikana.

Ubora wa jezi? Hii ni hatua nyingine ya kufikiriwa katika siku za usoni. Ukweli ni kwamba ubora wa jezi zetu ni tofauti na ule wa jezi za nje. Kitambaa cha jezi zetu bado hakipo katika ubora sawa na jezi za wakubwa wa Ulaya. Nadhani kwa sababu kwa sasa tunastahili hali hii kiuchumi.

Kama jezi ikitengenezwa katika ubora uliopitiliza nadhani itastahili kuuzwa kuanzia Sh 90,000 na kuendelea. Nani atamudu? Watamudu watu wachache na kutakuwa na kilio kubwa kutoka kwa sisi watu maskini. Kitambaa chetu kutoka China kimeangalia hali halisi ya uchumi wa watu.

Hata jezi za klabu mbalimbali kubwa za Ulaya zinazouzwa hapa nchini zimetengezwa na kitambaa ambacho kinamudu uchumi wa Mtanzania. Haishangazi kuona jezi ya Manchester United inauzwa Shilingi 35,000 za Kitanzania wakati Ulaya jezi ni ghali na uuzwa kuanzia dola 70 na kuendelea.

Kilio cha ubora wa jezi lazima kiambatane na ukweli kwamba mfuko wa Mtanzania wa kawaida hautamudu kununua jezi halisi ya Yanga au Simba ambayo itakuwa imetengenezwa na kitambaa kile kile kilichotumika kutengeneza jezi halisi ya Manchester United.

Nini kitafuata kwa Simba na Yanga? Ni kweli kwamba wameambukiza klabu nyingine kuwa na jezi zao na kufanya biashara lakini ni wazi kwamba pengo kati ya Simba na Yanga na wengineo litaendelea kuwa kubwa. Pengo kati ya Yanga na Coastal Union linazidi kuimarika. Pengo kati ya Simba na Biashara United ya Musoma linazidi kuimarika.

Sijui tutafanya nini kupunguza makali ya pengo hili katika siku za usoni ili tuwe na ligi yenye ushindani zaidi tofauti na hali ilivyo sasa.

Kitu cha kusikitisha zaidi ni kwamba hata mashabiki wa mikoani wa klabu hizi ni mashabiki wa Simba na Yanga.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz