Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Ikabaki kuwa mechi ya Inonga na Kibwana

Inonga Pic Data Beki wa Simba Mkongo Henock Inonga

Wed, 4 May 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mipira miwili hafifu kuelekea kwa Djigui Diarra kutoka kwa wachezaji wa Simba ndio yalikuwa mashambulizi pekee yaliyolenga lango juzi jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kwa Yanga hakukuwa na mpira wowote ambao ulilenga lango. Inakupata tafsiri ya jumla ya pambano la watani juzi.

Ni mechi ambayo hautaweza kuirudia tena katika televisheni yako kama watu wa Azam watairudia kuionyesha katika TV yao. Hakuna matukio mengi ya kusisimua labda tu kama unatafuta tukio moja maalumu ambalo ulilikosa. Vinginevyo hakukuwa na matukio mengi.

Kwanini? Tahadhari ilikuwa kubwa kwa pande zote mbili. Kama ilivyokuwa katika pambano lililopita, walinzi wawili wa kati wa Simba, Enock Inonga na Josh Onyango walikuwa makini kuhakikisha mshambuliaji tishio zaidi kwa sasa katika Ligi yetu, Fiston Mayele hatetemeki. Na kweli hakutetemeka.

Lakini walikuwa wapi washambuliaji wengine wa Yanga nikimaanisha mawinga na viungo washambuliaji? Walikuwepo wapi washambuliaji wa Simba wakiongozwa na Chris Mugalu? Na wao walipaswa kufanya jambo. Hawakufanya. Hakukuwa na ubunifu wowote mkubwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya uwanja.

Clatous Chama alicheza dakika 45 tu kisha akatolewa. Kwa mara nyingine tena Chama alikuwa na mechi mbovu dhidi ya Yanga. Sijui huwa ana matatizo gani katika pambano la watani. Mechi pekee ambayo Chama aling’ara dhidi ya watani ilikuwa ni katika ushindi wa mabao 4-1 pambano la FA miaka miwili iliyopita

Vinginevyo Chama alikuwa na mechi nyingine mbovu. Hakuwa msaada kwa timu yake pale ilipomuhitaji. Chama anahitajika zaidi na Simba kucheza karibu na boksi la adui na kufanya mambo yatokee. Hakufanya hivyo. Hakuwa na maamuzi makubwa na hakuonekana pia kuwa fiti. Nilidhani wakati wenzake wanacheza mechi za Shirikisho yeye alikuwa anapata mapumziko ya kutosha.

Na katika pambano ambalo anatoka Chama kisha anaingia Rally Bwalya ni wazi kwamba hautegemei mabadiliko makubwa ya kiuchezaji. Bwalya huyu huyu alishindwa kuziba pengo la Chama wakati ameenda Morocco angewezaje kufanya maajabu katika dakika 45 za kipindi cha pili juzi?

Ousmane Sakho ameendelea kuwa mchezaji ambaye hana mwendelezo wa ubora kama ilivyo kwa Bernard Morrison. Leo wanakuwa katika fomu kesho wanakuwa ovyo. Sakho hakuwa na mchango wowote uwanjani. Yule Sakho wa michuano ya Mapinduzi sijui amekwenda wapi? Kabla ya mechi alikuwa miongoni mwa mastaa ambao tulitazamia wangeweza kufanya jambo. Na yeye pia, kama ilivyo kwa Morrison benchi lilimuita.

Kilichokuwa kinatokea Simba ndicho ambacho kimetokea Yanga. Feisal Salum nyuma yake kulikuwa na mafundi wawili, Yannick Bangala na Khalid Aucho. Alipewa leseni ya kuwa kiungo mchezeshaji na afanye analotaka lakini hakuwa na maajabu.

Kama ilivyokuwa yeye ndivyo ilivyokuwa kwa Saido Ntibanzokonza. Wote hawakuwa na maajabu na kwa kiasi kikubwa walichangia Mayele asiwe na maajabu. Hawakumpa huduma zinazotakiwa. Ilishangaza kuona Farid Mussa alicheleweshwa kuingia uwanjani mpaka dakika ya 79.

Upande wa Jesus Moloko nao ulikuwa hivyo hivyo. Sawa, alisababisha Mohammed Hussein Tshabalala asipande mara kwa mara lakini bado hakuwa na madhara makubwa. Na aliyeingia nafasi yake, Dennis Nkane naye alikuwa kinda ambaye hakuwa na uzoefu wa mechi yenyewe. Hakuleta maajabu uwanjani na kama anataka kuwa kama Mrisho Ngassa basi bado ana safari ndefu.

Mwisho wa siku ilikuwa ni mechi ambayo Aishi Manula na Diarra hawakutoka jasho sana. Hakuna ambaye aliokoa mchomo wowote wa hatari. Hakuna ambaye baada ya mechi angeweza kulala na viatu. Hakuna. Kama unaweza kusema Mayele hakuwa tishio unajaribu kujiuliza Mugalu alikuwa na tishio gani?.

Mwisho wa siku ikabaki kuwa mechi ya Shomari Kibwana na Enock Inonga. Katika mechi kubwa ya watani wa jadi ukiona wanasifiwa zaidi mabeki basi ujue hakukuwa na mabao. Na zaidi ukiona kwamba hakuna kipa aliyeokoa michomo basi ujue mabeki walifanya maeneo ya makipa yakawa salama zaidi. Shomari Kibwana ni mbishi.

Anacheza upande wa kushoto huku akitumia mguu wa kulia na kuwaweka benchi wachezaji wenye nafasi yao, Yassin Mustapha na David Bryson. Kulikuwa na wasiwasi kuhusu nafasi yake ya kulia wakati Djuma Shaban alipowasili. Hata hivyo ameweza kuondoa utata huo kwa kuhamia sehemu ambayo sio yake na ameitendea haki.

Juzi kwa nyakati tofauti aliweza kuwanyamazisha watu wote aliopelekewa upande wake kuanzia Morrison hadi Sakho. Lakini kama haitoshi, sio tu kwamba aliwadhibiti, lakini aliipandisha timu yake. Kwa uchezaji wake, Kibwana ni mchezaji halisi wa Yanga. Yanga huwa ina aina ya wachezaji wake. Wakati mwingine sio mafundi sana lakini huwa wanacheza kama vile kesho haipo.

Inonga naye alikuwa na mechi nzuri dhidi ya Mayele. Safari hii ni yeye hasa ndiye aliyemdhibiti Mayele. Mechi ya kwanza alijaribu kuiba sifa za Onyango kwa kumsindikiza Mayele katika benchi wakati anatolewa. Safari alijikuta katika matukio halisi na Mayele na akafanya tackling tatu nzuri.

Inonga anaonekana kuwa mwepesi wa mbio za ghafla. Lakini anapofika anakuwa na timing nzuri za kulala chini na kuiba mpira. Asingekuwa kuwa mwepesi huenda sasa hivi tungekuwa tunazungumzia hadithi nyingine kwa Mayele. Angeweza kutetema.

Hadi tunaondoka uwanjani tulikuwa tunawaimba Inonga na Kibwana zaidi. Lakini kama ni faida ya matokeo basi Yanga watakuwa wamenufaika zaidi na sare kwa sababu pengo lao na watani linaendelea kuwa lile lile tu huku zaidi wakiwa katika nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne kupita kavu.

Lakini hatuna muda wa kusubiri sana. Kuna uwezekano mkubwa wakubwa hawa wakakutana katika nusu fainali ya kombe la FA. Simba anatazamiwa kumfunga Pamba na kukutana na Yanga. Itakuwa nusu fainali ambayo kila mtu angetamani iwe fainali. Labda siku hiyo hatutawasifu mabeki na badala yake tutawasifu zaidi washambuliaji au viungo wachezaji.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz