Ghafla tumemfanya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kama staa mpya katika soka letu. Wakati mwingine soka letu linachekesha sana. Fei ni yule yule tu. Hajawahi kubadilika. Kipaji maridhawa kutoka Zanzibar. Upande ule huwa unatoa viungo wengi maridhawa katika soka letu.
Naweza kukuhesabia kwa vidole viungo wanane wanaotamba Ligi yetu wanatokea Zanzibar. Fei Toto ni kiongozi wao kwa sasa. Ni staa wao zaidi kama ambavyo wakati fulani tulikuwa na Abdi Kassim ‘Babi’ kutoka katika upande ule. Kinachonishangaza ni namna ambavyo tumemgeuza Fei kuwa staa mpya.
Fei angeweza kuwa staa tangu zamani kidogo. Kilichobadilika ni mabao yake ya siku za karibuni. Angeweza kuwa nayo muda mrefu tu ingawa zamani alikuwa anafunga kwa kuibiaibia. Watu wa kwanza waliomchelewesha Fei Yanga ni wale makocha wa awali.
Ni Mohammed Nabi, kocha wake wa sasa ndiye aliyemsogeza mbele kidogo akacheze maeneo karibu na lango la wapinzani. Sawa Fei ni mkabaji mzuri, msambazaji mzuri, mpiga chenga mzuri, lakini zamani hakuwa na madhara sana. Kumbe alipaswa kusogea mbele na kufanya hayo katika lango la wapinzani.
Kwa miaka kadhaa sasa Yanga walikuwa wanasaka kiungo wa aina ya kiungo aliyewatesa sana kutoka kwa wapinzani wao, Clatous Chama ambaye kwa sasa ameondoka. Yanga walikuwa wanahitaji mtu ambaye atalainisha mambo katika eneo la mwisho. Hawakuweza kumpata kiurahisi.
Wakati fulani walisafiri hadi Angola kwenda kumfuata chotara wa Kireno, Carlinhos ili aje kufanya kazi hiyo. Carlinhos alijitahidi lakini hakuweza kuwa Chama wa Yanga. Alicheza katika staili tofauti ya kujikuta akiwa mtaalamu wa mipira mirefu na ile iliyokufa. Basi. Baadaye akaondoka zake baada ya kushindwana na maisha yetu.
Baadaye akaja Saido Ntibazonkiza. Wakamuita Antibiotic. Alisisimua siku za kwanza, lakini inaonekana alikuja na miguu iliyochoka alipotua uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere. Baadaye akafifia na sasa imebakia historia tu miongoni mwa mashabiki wa Yanga.
Alichofanya Nabi ni kuendelea kumsaka Chama mpya ndani ya kikosi kilichopo na sio nje ya kikosi. Akagundua kwamba Fei angesogea mbele angekuwa na madhara makubwa. Na ndicho alichofanya. Na ndicho ambacho Fei ameendelea kufanya kwa ufasaha. Zamani Fei angeweza kupiga chenga maridadi katikati ya uwanja mashabiki wakashangilia na kisha angetoa pasi fupi kwa mtu aliye karibu naye.
Zamani Fei angeweza kupiga visigino maridadi katikati ya uwanja na mashabiki wangefura kwa hasira. Hata hivyo, vitu vingi ambavyo alikuwa anafanya vilikuwa vinavutia kwa macho lakini havikuwa na tija sana katika eneo la mwisho kama ambavyo kina Chama walikuja kufanya baadaye.
Fei ameibuka baada ya Nabi kumpa leseni ya kwenda mbele msimu uliopita. Na Nabi aliukuta msimu ukiwa katikati. Nabi alikuwa anaweza kuwapanga Zawadi Mauya na Tonombe Mukoko kama viungo wawili wa nyuma (double pivot) na kisha kumpa leseni Fei afanye anachotaka mbele.
Hapo ndipo Fei alijikuta katika maeneo ambayo alipaswa kuwa ‘serious’ na lango la adui kuliko nyuma. Alipaswa ama kupiga shuti na kufunga au kupiga pasi ya mwisho. Ubora zaidi wa Fei umeonekana hapo baada ya kupunguziwa majukumu mengine ya eneo la kiungo. Ndio huu ubora wa Fei ambao tunauona sasa.
Ubora mwingine wa Fei umeletwa na timu yenyewe ya Yanga ya sasa. Kumbuka kwamba Fei alipishana na kikosi cha moto cha kina Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Simon Msuva na wengineo. Wakati yeye anaingia Yanga kikosi kile ndio kilikuwa kinasambaratika na umaskini ulikuwa umeanza kuingia Yanga.
Wachezaji bora huwa wanang’arishana. Fei angeonyesha ubora wake kama angecheza sambamba na kina Kamusoko na kama angetumika vema uwanjani. Badala yake alijikuta katika Yanga nzito sambamba na kina Ibrahim Ajibu ambao walijaribu kusukuma jahazi.
Lakini sasa Nabi amempa jukumu jipya akiwa na mafundi wa mpira kando yake na nyuma yake. Ubora wa kina Yannick Bangala na Khalid Aucho unamfanya Fei auone mpira kuwa rahisi zaidi. Hakuna anayebutua kati yao na anasimama akisubiri pasi zinazofika akiwa huru.
Kulia na kushoto pia kuna watu wa maana. Zaidi ya yote Yanga wenyewe wa sasa wanacheza mpira ambao Fei anaupenda. Mpira wa pasi. Na anajikuta ana raha zaidi kwa sababu Yanga wanakaa na mpira kwa muda mwingi. Wachezaji mafundi wanafurahia kuona timu yao ikimiliki mpira kwa muda mrefu.
Majuzi tu tulimuona Cristiano Ronaldo akimpiga mateke staa mmoja wa Manchester City aliyekuwa chini. Kisa? Pale Ronaldo alikuwa ameudhika tu na namna ambavyo City walikuwa wamekaa na mpira kwa muda mrefu huku wao wakifanyishwa ‘Hangaisha bwege’. Hakukuwa na kingine.
Ubora wa Chama ulichangiwa na ubora wa wachezaji wengine wa Simba. Ubora wa Chama ulichangiwa na ubora wa kina Jose Luis Miquissone, kina Jonas Mkude, kina Thadeo Lwanga, kina Shomari Kapombe na wengineo. Mastaa wanasaidiana kuwa mastaa.
Hata Barcelona ya Pep Guardiola mastaa walisaidiana kuwa mastaa. Ungeweza kuiona Barcelona ya miaka ya karibuni ambayo Lionel Messi alilazimika kuikimbia. Alijikuta akifanya kazi kubwa peke yake uwanjani mpaka akachoka. Zamani alikuwa akinga’arishana tu na kina Xavi, Iniesta, Dani Alves, Sergio Busquets, David Villa na wengineo.
Ustaa wa Fei sio jambo jipya. Alikosewa tu kwa muda mrefu na sasa anajikuta akicheza katika timu mwafaka, sambamba na wachezaji mwafaka chini ya kocha mwafaka kwake. Natabiri kwamba Fei angekuwa staa muda mrefu zaidi ya hivi kama angecheza chini ya Hans van der Pluijm na mastaa kina Kamusoko.
Mchezaji wa kizawa ambaye hataimarika kwa kikosi kilichopo sasa atakuwa mzembe. Kama timu yake inacheza soka maridadi na mchezaji mwenyewe anacheza katika nafasi mwafaka kwanini ashindwe kucheza soka maridadi pengine kuliko wakati wowote wa maisha yake ya soka?