Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Caicedo ametukumbusha kila kitu maishani kwetu

Skysports Moises Caicedo Brighton 6016302 Moises Caicedo

Tue, 31 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Aliandika kitu mchezaji anayeitwa Moises Caicedo katika ukurasa wake wa Instagram Jumamosi mchana. Kitu ambacho sio kipya lakini kimeendelea kunikumbusha maisha yetu na ya wenzetu namna ambavyo yana tofauti kubwa ya fikra. Kuna mahala Sera za Ujamaa zilituangusha.

Caicedo anacheza klabu ya Brighton pale Ligi Kuu England. Anatakiwa na klabu ya Arsenal. Klabu yake inaamini Caicedo ana thamani ya Pauni 80 milioni wakati Arsenal wameweka mezani kiasi cha Pauni 65 milioni ambacho kimekataliwa.

Caicedo anatamani kucheza Arsenal. Anatamani kucheza klabu kubwa zaidi ya Arsenal, lakini anatamani pia kipato kikubwa. Amenifurahisha tu mambo mawili ambayo ameandika katika ujumbe wenye mambo mengi ya maana.

Aliandika “Namshukuru Bwana Gloom (mmiliki wa timu) na Brighton kwa kunipa nafasi ya kuja kucheza Ligi Kuu ya England na nadhani nimejitahidi sana kuonyesha ubora wangu. Siku zote nacheza soka nikiwa na tabasamu. Mimi ni kijana mdogo katika ndugu zangu 10 ambao tumekulia katika umaskini kitongoji cha Santa Domingo nchini Ecuador. Ndoto yangu siku zote ni kutaka kuwa mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Ecuador”

“Najivunia kuwa naweza kuleta rekodi bora zaidi ya uhamisho katika historia ya Brighton ambayo inaruhusu klabu kuwekeza katika mambo mengine na kuifanya iwe na mafanikio. Mashabiki wameniweka katika mioyo yao na siku zote watakuwa katika mioyo yangu nadhani wataelewa kwanini nataka kuondoka.” Unaendelea kusomeka ujumbe wake.

Kufikia hapo Caicedo alikuwa amenikosha kwa mambo mengi. Tuanzie na lipi? Hili la kwanza la namna gani amekulia katika umaskini uliotopea. Anataka kuikomboa familia yake katika maisha dunia na kuleta mwelekeo mpya katika familia.

Kiuchumi najua Ecuador ipo juu ya Tanzania. Najua wanaishi kibepari pia. Hapa Caicedo ananikumbusha stori ambazo nimezisikia mara nyingi kutoka kwa wachezaji wa Amerika Kusini na nchi kadhaa za Afrika. Stori za vijana maskini waliotoka katika umaskini na wamepania kubadilisha historia za familia zao.

Inanikumbusha wengi lakini mfano wa haraka haraka unanijia kutoka kwa Ronaldo de Lima. Hasira zake zilimfanya atumie kipaji chake vyema. Wakati huo akiwa kijana mdogo mama yake mzazi, Sonia alikuwa Mhudumu wa Baa. Nyumbani hakukuwa na dada wa kazi. Ronaldo alikuwa anaenda kazini kwa mama kwa sababu nyumbani hakukuwa na dada wa kazi kwa hiyo asingeweza kubaki nyumbani peke yake kwa sababu alikuwa mdogo.

Alichokuwa anaambulia kazini kwa mama yake ni kuona mzazi wake akishikwa makalio na walevi ambao alikuwa akiwahudumia kazini. Hakupenda. Aliweka dhamira angepambana kila awezavyo katika soka ili kumwondoa mama yake katika kazi hiyo.

Historia za namna hii kutoka kwa Ronaldo na Caicedo unaweza kuzikuta mara nyingi kwa wachezaji wa Amerika Kusini na Afrika kasoro Tanzania tu. Sijawahi kusikia wachezaji wetu wakielezea dhamira zao za kwanini wanapambana katika soka.

Kwa wenzetu maisha ni magumu zaidi kuliko sisi. Nadhani sisi tuna watu wengi ndani ya familia ambao wana uwezo mkubwa wa kula na kuamka na ndio maana hatuoni sababu ya kupambana zaidi. Ujirani na urafiki kupitia sera zetu za ujamaa umefanya watu wengi, hata maskini, kuona maisha yetu ni rahisi wakati sio kweli.

Tunaishi katika umaskini uliotopea lakini ndoto zetu hazioni mbali. Na zaidi ya kila kitu ni kwamba huwa hatuzifanyii ndoto zetu na kujaribu kubadili mkondo wa maisha katika historia zetu. Tunaishi katika mazoea tu na hakuna kikubwa ambacho tunabadili.

Zamani kulikuwa na simulizi za kijinga pindi ukiwahoji wachezaji wetu. Wengi walikuwa wanadai kwamba ndoto zao ni kucheza Simba au Yanga. Halafu wale waliocheza Simba na Yanga walikimbilia kusema ndoto zao zilikuwa kucheza klabu hizo kongwe nchini.

Neno linaoashiria kuondoa umaskini katika familia zao halikuwepo. Leo baada ya miaka mingi, hauwezi kusikia simulizi kama za Caicedo na De Lima katika mahojiano na wachezaji wetu. Wapo wengi ambao watakwambia kwamba ndoto zao ni kucheza nje ya nchi. Hata hivyo hawazihishi ndoto zao. Wanatania tu. Ndoto zao feki na maisha halisi ni vitu tofauti.

Caicedo anaweza kuwa analipwa kiasi kikubwa cha pesa pale Brighton lakini ametukumbusha mambo mawili. Ametukumbusha bado ana familia kubwa ambayo imeendelea kumtegemea pale kwao Santi Domingo Ecuador huku yeye akiwa mdogo zaidi katika familia.

Angekuwa mchezaji wa Tanzania tayari angekuwa ameridhika kwa kucheza Brighton and Hove. Si ajabu hata Taifa lingekuwa limeridhika kwa kuwa na mchezaji ambaye anacheza Brighton. Ni kama wakati ule tuliporidhika kwa kuwa na Mbwana Samatta pale Aston Villa.

Pia Caicedo anatukumbusha kiu nyingine ambayo ni wazi wachezaji wetu hawana. Labda Samatta tu inawezekana alikuwa nayo. Kiu ya kuwa alama kubwa zaidi ya taifa katika soka au michezo kwa jumla.

Kuna mahala anadai anataka kuwa mchezaji mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Ecuador. Kumbuka Antonio Valencia amewahi kuichezea Manchester United na wengi tunamfahamu kama mchezaji mkubwa kuwahi kutokea Ecuador. Hata hivyo Caicedo anataka kwenda zaidi.

Unadhani vijana wetu wanataka kwenda zaidi? Hata wakisema unaweza kuwaamini? Akili zao zimebaki kama wachezaji wa zamani. Kucheza Simba na Yanga. Tunafahamu namna ambavyo wanahangaishwa na pesa za Simba, Yanga na Azam.

Lakini hapo hapo Caicedo amezikumbusha timu zetu jambo moja rahisi tu. Timu zetu nyingi zipo kwa ajili ya kutengeneza wachezaji na kulisha wale ambao wametuzidi kiuwezo wa kipesa.

Amewaambia Brighton pesa ambao wakubwa wameweka kwake ni nyingi na zinaweza kuwasaidia katika kuwekeza na kufanya maendeleo mengine.

Sisi huku kwetu wakubwa wanashikana mashati kwa ajili ya kusaka zaidi pointi tatu au kumfunga mtani. Hawaangalii namna gani ambavyo wanaweza kutengeneza wachezaji na kuwauza kwa ajili ya kupata pesa nyingi na kuwekeza zaidi klabuni.

Walau miaka ya karibuni wakubwa wameanza kuamka na kufanya biashara hii ya kuuza wachezaji lakini zamani ilikuwa mwiko. Caicedo anatukumbusha kwamba Brighton inaweza kufanya mambo makubwa kupitia dau ambalo akina Arsenal wameweka mezani.

Columnist: Mwanaspoti