Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Ajibu ametupa majibu ya kibepari, nyakati zitaongea

Ibrahim Ajib Migomba Dd Ibrahim Ajib katika jezi ya Singida Big Stars

Tue, 17 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Rafiki yangu Ibrahim Ajibu Migomba alikuwa katika ubora wake mbele ya vinasa sauti vya waandishi wa habari baada ya pambano kati ya Singida Big Stars na Mlandege kumalizika Ijumaa usiku katika Uwanja wa Amaan pale Unguja.

Ajibu alikuwa ameulizwa maswali mawili mazuri na mwandishi wa habari. Swali la kwanza aliulizwa kuhusu kuhamahama kwake kutoka Simba, Yanga na Azam. Alijibu vema kwamba yeye hakuwa amezaliwa Simba, Yanga wala Azam.

Majibu mazuri na ya halali. Hata Mwalimu Nyerere aliwahi kutuambia kwamba CCM haikuwa baba yake wala mama yake. Labda Ajibu alikuwa sahihi zaidi katika jambo hili. Kwanini tumbishie? Labda mwenzetu hakuwa na ndoto sana za kucheza Simba, Yanga wala Azam. Na wala haoni kama kuondoka katika timu hizo na kwenda Singida inaweza kuwa hatua moja tu.

Labda kwake Simba, Yanga na Azam sio timu ambazo zinaweza kuishurutisha akili yake kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa Kitanzania ambao wanatamani kufika katika klabu hizo kwa ajili ya mafanikio ya kipato na mchezo wenyewe kwa ujumla.

Na baada ya hapo Ajibu akaulizwa kuhusu mpango wa kwenda kucheza Ulaya. Kwamba mashabiki wengi wangependa kuona akicheza soka la kulipwa barani Ulaya kutokana na kuwa na kipaji maridadi. Na swali hili pia Ajibu alilijibu vema.

Kwamba hata sisi wauza madafu tunaweza kwenda kufanya kazi zetu Ulaya. Kwamba sio yeye peke yake ambaye analazimika kwenda kufanya kazi Ulaya. Kwamba hata muuza mkaa anaweza kwenda kufanya kazi yake Ulaya kwa sababu na Ulaya wanapikia mkaa.

Majibu ya Ajibu yamenifurahisha. Ni majibu ya kibepari. Kifupi ni kwamba katika dunia ya kibepari kila mtu aishi kwa kadri anavyojua na hakuna haja ya kufuatanafuatana. Kila mtu ana uhuru wake na maamuzi yake ya kufanya anachokifanya.

Katika dunia za kibepari hivi ndivyo ambavyo watu wanaishi. Binafsi niliacha muda mrefu kufuatilia habari za Ajibu au kumsisitizia atafute malisho mema nje ya mipaka ya Tanzania. Baadaye nilikuja kugundua kwamba kila mtu awe makini zaidi na familia yake kuliko familia ya mwenzake.

Mwisho wa siku katika hizi kazi ambazo tunafanya hatima yetu ndio ambayo itahalalisha maamuzi ambayo tumewahi kuyafanya siku za nyuma. Nyakati hizo zikifika ni bora kila mtu afe na familia yake kuliko kuombana michango ya kuuguzana.

Kuna mastaa wengi wa zamani ambao kwa sasa wanajuta kwanini walichukua maamuzi mabovu katika maisha yao ya soka angali wakiwa mastaa. inawezekana Ajibu anajua anachokifanya kwa sasa. Yeye ni mtu mzima. Hakuna haja sana ya kumlazimisha kuchukua baadhi ya maamuzi katika maisha yake ya sasa.

Kitu ambacho hatutapenda kusikia ni vilio vya siku za mbele kwamba wachezaji wa zamani wametupwa na hawathaminiwi. Barani Ulaya na kwingineko mchezaji wa zamani akishindwa kuingia katika mifumo mingine ya maisha baada ya kustaafu soka basi anabakia kuwa kama mtu mwingine tu.

Kwa mfano, barani ulaya hauwezi kusikia vilio kutoka kwa wachezaji wa zamani kwamba wametelekezwa. Inaaminika kwamba katika maisha yao ya ustaa walikuwa wanalipwa vizuri, wanachukua maamuzi yao vizuri bila ya kujali unazi kwa klabu zao. Ni kama ambavyo Ajibu ametupa jibu la swali la kwanza.

Hauwezi kusikia michango ya kumuuguza mchezaji wa zamani. Na ndio maana wala haukusikia klabu ya Santos inalaumiwa kwa kutomuuguza Pele. Wenzetu wanakwenda mbali zaidi kiasi kwamba wachezaji wa zamani hawaingii bure katika viwanja vya soka.

Huku utasikia vilio vya wachezaji wa zamani kutaka kuingia bure viwanjani kwa sababu walilitumikia taifa. Ulaya wachezaji wa zamani wananunua tiketi za kwenda viwanjani. Wakati mwingine pia huwa wanaviomba vilabu vyao viwape tiketi za kuingia uwanjani (Complimentary), lakini haiwi lazima.

Kuna wachezaji wamecheza soka miaka ya juzi tu wakifundishwa na kocha, Marcio Maximo lakini tayari wameanza vilio. Hii inaonyesha namna gani maisha ya soka hapa nchini kwetu yanakwenda kasi. Ni majuzi tu tulikuwa tunawashauri wakajaribu kucheza soka la kulipwa Ulaya lakini wakatupa majibu ya Ajibu na sasa wameanza vilio. Ukikutana nao wanalalamika kwamba wametupwa klabu zao. tukumbuke kwamba walikuwa wanalipwa vizuri tu na klabu zao.

Mara nyingi ushauri wa kwenda nje utolewa kwa wachezaji wenye vipaji kwa sababu huwa tunaamini kwamba wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kulipwa vema zaidi kuliko wakibakia nchini. Lakini nimefurahishwa na majibu ya Ajibu ambayo yanaashiria kwamba ‘tusifuatane’ na kila mtu aishi kivyake.

Mara nyingi uhalali wa majibu haya huwa unakuja wakati mchezaji au mwanadamu anapokuwa amestaafu kuifanya kazi yake. Mara nyingi nyakati huwa zinaongea zaidi kuliko wanadamu. Kwa sasa tunaweza kulazimisha mambo ambayo tunadhani yana msingi halafu tukadharauliwa. Inabidi tuvumilie tu kwa sababu nyakati ndizo huwa zinahalalisha matendo yetu ya sasa.

Ajibu ameturudisha katika majibu ya kibepari ambayo inabidi tuyatafakari na tuache tabia zetu za kijamaa za kufuatiliana kila wakati. Ni vema tusifuatiliane nyakati hizi na wala tusifuatiliane nyakati za kustaafu kwetu. Tusifuatiliane nyakati za magonjwa wala misiba. Hivi ndivyo ubepari ulivyo.

Wenzetu wanaishi hivi. Tukiamua kuishi hivi nadhani itakuwa poa zaidi na tutaacha kufuatiliana au kukumbushana habari za kuchangiana katika habari za magonjwa kwa wachezaji wa zamani. Muda si mrefu wachezaji wa sasa watakuwa wachezaji wa zamani na kila mmoja atakuwa ameshika hatima yake mahala.

Columnist: Mwanaspoti