Ni raha iliyoje kwa Tanzania, kushuhudiwa vijana chini ya miaka 20 wakipigania ndoto zao kwenye akademi mbalimbali barani Ulaya? Ni wazi kuwa wanabeba matumaini ya kikosi kijacho cha Taifa Stars.
Jabir Mpanda ambaye kwa sasa yupo nchini kwa mapumziko mafupi akitokea Hispania kwenye akademi ya Getafe ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania ambao wapo kwenye kundi hilo, linaloongozwa na Kelvin John pamoja na Novatus Dismas ambao wameanza kuonyesha makali yao huko Ubelgij.
Kinda huyo mwenye miaka 16, alitembelea ofisi zetu za Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata jijini Dar es Salaam na kueleza maisha ya Hispania kwenye akademi ya Getafe huku akionyesha kuvutiwa kwa karibu na nyota wa Real Madrid, Vini Jr ambaye siku chache zilizopita alitoka kuwafanya kitu kibaya Liverpool.
Jabir anapenda kushambulia akitokea pembeni na hiyo ndio sababu ya kuvutiwa na Vini Jr ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali akiwa na wababe hao wa soka la Hispania kiasi cha kumpoteza Eden Hazard.
KWANINI VINI JR
Anasema ni kutokana na utofauti ambao yupo nao, amekuwa akicheza kitimu zaidi tofauti na mawinga wengine,"Wapo wachezaji wazuri ambao ukisema uwaorodheshe orodha itakuwa ndefu sana, lakini binafsi huwa navutiwa na mchezaji ambaye anacheza kwa ajili ya kusaidia timu,"
"Wapo mawinga ambao hucheza kwa ajili ya kuonekana na sio maslahi ya timu, Vini Jr ni tofauti sana ndio maana nimekuwa nikimfuatilia na kwa bahati nzuri niliwahi kupata nafasi ya kumtazama Santiago Bernabeu."
"Sitaki kuwa yeye, nataka kuwa mimi lakini ni vizuri kujifunza kutoka kwa wachezaji ambao wanafanya vizuri,"anasema kinda huyo.
MAISHA YA GETAFE
Licha ya kuwa huu ni msimu wake wa kwanza akiwa na akademi ya Getafe, Jabir anaeleza kufurahia maisha ndani ya akademi hiyo.
"Kwanza kabisa nimekuwa nikitoa shukrani zangu kwa SPF ambao wao ndio walianza kulea kipaji changu kwa Hispania kabla ya kupata nafasi Getafe ambako nilianza kwa kufanya majaribio, maisha ya hapa ni mzuri sana,"
"Hakuna tabu yoyote kubwa ambayo nakumbana nayo kwa sababu hapo kabla nilipita kwenye akademi, nilijifunza lugha na mambo mengine ambayo yamenifanya kutoteteleka, ninauwezo mzuri tu wa kufanya mawasiliano na mtu yeyote kwa Kihispaniola, chakula nimezoea," anasema.
Kuhusu aina ya soka la Getafe, Jabir anaeleza kuwa mfumo wao umekaa kichani na anaamini kuwa anaweza kumsaidia kucheza kirahisi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kama atapandishwa wakati utakapofika.
"Kila kitu kinawakati wake, kwa sasa ni mchezaji wa timu za vijana lakini natamani baadae kucheza kikosi cha kwanza," anasema.
UNAL NI BALAA
Jabir amemtaja Enes Unal kuwa miongoni mwa wachezaji hatari wa Getafe kwenye Ligi ya Hispania ambayo ni maarufu kama La Liga.
"Bado sijapata nafasi ya kukutana na mchezaji yeyote wa kikosi cha kwanza, nadhani wapo bize na michezo ya kimashindano, lakini Unal ni kati ya wachezaji bora wa Getafe," anasema.
Unal mwenye uwezo wa kucheza kama winga wa kulia au mshambuliaji wa kati, ameifungia Getafe mabao saba kwenye La Liga.
Raia huyo wa Uturuki anatarajiwa leo, Jumatatu kuongoza mashambulizi ya timu hiyo ambayo itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Villarreal.
TARIQ NA BARKA WANAKUJA
Jabir anawaona mbali wadogo zake, Barka na Tariq na anaamini miaka michache ijayo watapiga hatua kubwa kama ilivyo kwake kutokana na vipaji walivyonavyo,"Nimekuwa nikiongea nao maana kwa bahati nzuri wote tupo Hispania, nimekuwa nikiwapa moyo kama kaka yao,"
"Najua kuwa wanavipaji vikubwa, wanatakiwa kuendelea kufanyia kazi yale ambayo watakuwa wakifundishwa, muda ukifika milango yao nao itafunguka kama ambavyo ilikuwa kwangu, ulikuwa ni wakati wa Mungu," anasema.
Barka yupo MARCET Football University ambayo alipita Ansu Fati akiwa mdogo kabla ya kuibukia Barcelona huku Tariq akiwa SPF.