Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ivory Coast wanarusha mawe barabarani kwa mastaa gani?

Ivory Coast Lost To Eq.jpeg Ivory Coast wanarusha mawe barabarani kwa mastaa gani?

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Alionekana mwenye sura ya fadhaa baada ya Guinea ya Ikweta kufunga bao la nne. Didier Drogba. Wote tulikuwa tunashangaa anawaza nini kichwani kwake. Hatuwezi kujua lakini ni wazi kwamba alikuwa anasikia uchungu mkubwa kwa kile ambacho alikuwa anakiona mbele yake.

Baadaye raia wenzake wa Ivory Coast wakaamua kufanya vurugu katika mitaa mbalimbali ya Abidjan. Sijui zilikuwa hasira za nini na sijui zilikuwa zinalenga nini. Kuanzia kwa Drogbamwenyewe hadi ndugu zake kuna kitu walikuwa wamekisahau.

Licha ya kwamba wao ni wenyeji wa michuano hii ya Mataifa ya Afrika, lakini nyakati zimewatupa mkono. Sio wao tu, timu nyingi za Afrika Magharibi zimepitwa na nyakati ambazo walikuwa wanatawala katika klabu kubwa za Ulaya.

Kama kizazi chao kingekuwa kinashiriki michuano hii basi wananchi walikuwa na haki ya kufanya vurugu. Bahati mbaya ni kwamba kizazi kile kimeondoka. Kizazi cha kina Drogba mwenyewe, Yaya Toure, Kolo Toure, Solomon Kalou, Cheick Tiote na wengineo.

Afrika Magharibi imekubwa na uhaba mkubwa wa mastaa kwa sasa. Kuanzia kwa Ivory Coast, Nigeria, Ghana, Mali na kwingineko. Wana wachezaji wengi ambao wanacheza nje, lakini wanacheza katika klabu za kawaida tu barani Ulaya.

Wale Ivory Coast waliokuwa wanateseka kwa Guinea ya Ikweta ni wachezaji wa kawaida tu wanaocheza katika klabu za kawaida tu barani Ulaya. Achilia mbali Thomas Partey wa Arsenal na Andre Onana wa Manchester United ni mchezaji gani mkubwa wa Afrika Magharibi anayecheza Manchester United, Arsenal, Liverpool, Real Madrid, Barcelona, Atletico Madrid, Juventus au Chelsea?

Zamani Chelsea ilikuwa ina Obi Mikel, Michael Essien, Kalou na Drogba. Zamani Barcelona walikuwa wanaweka mpira kwapani bila ya Samuel Eto’o. Zamani Real Madrid ilikuwa na watu kama Geremi Njitap na Mamadou Diara kutoka Mali.

Zamani Arsenal ilikuwa na Nwankwo Kanu. Liverpool iliwahi kuwa na kina El Hadji Diouf na Salif Diao achilia mbali Rigobert Song. Sasa hivi Afrika Magharibi imekaukiwa na vipaji vikubwa kama hivi na ndio maana mataifa ya kawaida kama Cape Verde na Mauritania yamekuwa yakiwadindishia.

Miaka ya hivi karibuni rafiki zetu Waarabu wa Afrika Kaskazini ndio walau wamepeleka mastaa wanaocheza timu kubwa na kutamba. Mohamed Salah ametamba pale Liverpool na Riyad Mahrez ametamba pale Manchester City.

Unatazama hii michuano na hauoni sana kama kuna wachezaji wanaoweza kwenda kutamba katika klabu kubwa. Labda Mohamed Kudus anaweza kutupa tumaini la kuwa mchezaji mwingine wa Afrika Magharibi anayeweza kutamba katika klabu kubwa barani Ulaya.

Wakati anatoka Ajax kwenda West Ham nilikuwa nashangaa kwanini timu kubwa zilikuwa haziwanii saini yake. Nadhani kwa sasa zinajuta na mwishoni mwa msimu West Ham huenda ikapata pesa nyingi kwa kumuuza Kudus kwenda katika klabu kubwa.

Staa mwingine ambaye inaonekana anaiwakilisha vema Afrika kwa sasa ni mshambuliaji wa Nigeria, Victor Osimhen anayecheza Napoli. Hata hivyo, Napoli bado haipo katika kiwango cha timu kubwa kama Manchester United au Real Madrid ingawa ni timu ya kihistoria.

Kukosekana kwa mastaa wakubwa katika nchi za Afrika Magharibi kumesababisha sasa hata wachezaji wa kawaida wenye asili ya nchi hizo ambao wamezaliwa Ulaya kurudi kwa kasi kuja kucheza katika nchi hizo. Namba zipo.

Leo Cameroon inajaza wachezaji wengi waliozaliwa Ulaya tofauti na wakati ule ikiwa na mastaa kama Eto’o mwenyewe, Marc-vivien Foe, Raymond Kala, Modest Mbami, Patrick Mboma, Geremi Njitap, Lauren Etame Mayer na wengineo wengi walikuwa wamezaliwa nyumbani.

Haishangazi kuona majuzi Eto’o alikuwa analalamika kwamba wachezaji waliozaliwa nje ya Cameroon walikuwa hawasikii sana uchungu kuvaa jezi ya Cameroon. Lakini hii yote imesababishwa na wazawa kuwa katika viwango vya kawaida.

Zama zao hawakuhitaji wachezaji waliozaliwa Ulaya waje kuwakilisha taifa. Ndio hiki hapa ambacho hata kinawatokea rafiki zao Ivory Coast. Mchezaji kama Nicolas Pepe atawasaidia nini pale uwanjani? Hawa ni wachezaji ambao wamejiona hawatoshi kuchezea nchi walizozaliwa na ndio maana wanarudi kucheza katika mataifa ya asili yao.

Kama Pepe angekuwa mzuri kiasi cha kuchezea timu ya taifa ya Ufaransa sidhani kama angerudi kucheza Ivory Coast. Ni ngumu kwa mchezaji kama Willy Saliba kuja kucheza Ivory Coast akiwa katika ubora huu na ndio maana amechagua kucheza Ufaransa.

Kitu kingine cha kawaida ambacho rafiki zangu wa Ivory Coast inabidi waelewe ni ukweli kwamba hata kama wangekuwa na kizazi cha dhahabu bado hawana haki na ulazima wa kushinda michuano hii. Mara kadhaa katika michuano mikubwa mwenyeji huwa anaondoshwa zake katika hatua yoyote ile ya michuano.

Kwa kumbukumbu za haraka haraka hata katika michuano ya Kombe la Dunia ni Ufaransa na England ndizo ambazo ziliweza kutwaa kombe hilo zikiwa katika ardhi ya nyumbani. England walifanya hivyo mwaka 1966 na Wafaransa walifanya hivyo mwaka 1998. Haikuhakikishii kutwaa kombe ukicheza nyumbani na kwa mpira wa Afrika maisha yamekuwa magumu zaidi baada ya kuingizwa kwa teknolojia ya VAR. Zamani naamini mabao yote mawili ya Ivory Coast ambayo yalikataliwa dhidi ya Guinea ya Ikweta yangekubaliwa.

Tuendelee kutazama Afcon na sasa Ivory Coast wamefanikiwa kupenya katika tundu la sindano na watacheza na rafiki zao Senegal ambao wana timu kali. Kwa namna ninavyoona Ivory Coast wanaweza kufungasha tena virago na wakafanya vurugu. Hawana timu ya kufanya maajabu katika michuano hii licha ya kuwa wenyeji.

Huu ndio ukweli wenyewe.

Columnist: Mwanaspoti