Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Itarushwa shilingi, ikitokea timu zikilingana pointi Qatar

Senegal Gal Itarushwa shilingi, ikitokea timu zikilingana pointi Qatar

Thu, 1 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

HATUA ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa sasa inaelekea ukingoni huko Qatar. Hivi, ushawahi kuwaza inakuwaje kama timu kundi moja zitaligana pointi?

Shirikisho la Kimataifa la Kaandanda (Fifa) limekuwa na utaratibu tofauti na michuano mingine ilivyo inapotokea timu zimelingana pointi kwenye kundi moja.

Inakuwaje? Mambo yapo hivi. Kama timu mbili au zaidi zimelingana pointi hatua ya makundi kitu cha kwanza kinachotazamwa ni tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Hicho ndicho kigezo kikubwa kinachotazamwa na Fifa. Waamini hapo watapata ufumbuzi wa kuzitofautisha na kujua ipi inasonga mbele.

Kanuni hiyo ilianza kutumika tangu 1962 na bado inaendelea licha ya michuano mingine ya soka duniani kuhamia kwenye kanuni ya matokeo ya timu mbili husika zilipokutana ilikuwaje endapo kama pointi zitakuwa zimelingana. Uefa, Shirikisho la Soka la Ulaya linatumia kanuni ya matokeo ya timu husika zilipokutana likitumia utaratibu huo kwenye michuano ya ubingwa wa Ulaya na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Huko La Liga, utaratibu unatumika pia ni ule wa matokeo ya timu husika zilipokutana.

Hata hivyo, kwenye Kombe la Dunia, huo pia ni moja ya utaratibu utakaotumika, lakini tu vigezo vingine vimeshindwa kutoa suluhisho. Mikikimikiki ya Kombe la Dunia ina vigezo saba vya kutofautisha timu zinapolingana pointi. Vigezo hivyo vimegawanywa makundi manne; rekodi za jumla kwa maana ya tofauti ya mabao, matokeo ya timu husika zilipokutana (head-to-head) fair play na kurusha shilingi.

Hizi hapa njia saba ambazo Fifa itatumia kuzitofautisha timu kwenye makundi ikitokea zimelingana pointi na zinapaswa kutinga hatua inayofuata.

REKODI ZA JUMLA

1. TOFAUTI YA MABAO

Tangu hatua ya makundi ilipoanza kwenye Kombe la Dunia 1950, timu 13 zilitolewa kwenye mchakato wa kuingia raundi inayofuata kwa kigezo cha tofauti ya mabao. Nchi ya karibuni zaidi kukumbana na sakata hilo ilikuwa Ureno kwenye fainali za 2014, ambapo iliondoshwa na Marekani kwenye Kundi C kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Fifa ilianza kutumia kigezo cha tofauti ya mabao timu zinapolingana pointi kwenye makundi ya Kombe la Dunia zilikuja baada ya huko awali ilikuwa inahitajika kucheza mechi ya mchujo kama ilivyokuwa Sweden 1958.

Miongo mitatu baadaye, Kombe la Dunia lilikuwa na mtindo wa tofauti ya mabao na ya kwanza uliiponza Algeria kutolewa Hispania 1982. Baada ya kuwafunga Chile 3-2 katika mechi za mwisho za makundi, Algeria ilikuwa na pointi nne na hapo ilikuwa ikisubiri mechi baina ya Ujerumani Magharibi na Austria iliyokuwa inachezwa siku inayofuata.

Ilikuwa mechi iliyokuja kudaiwa ni ya matokeo ya kupangwa. Ujerumani na Austria zilifahamu wazi kwamba zitasonga mbele kwa tofauti ya mabao kama kama tu Ujerumani itashindwa kwa tofauti isiyozidi mabao mawili. Ujerumani ikashinda 1-0, matokeo ambayo yaliyafanya mataifa hayo ya Ulaya yote kutinga hatua inayofuata na hapo ndipo Fifa walipokuja na mtindo wa mechi za mwisho za hatua ya makundi zote zichezwa muda mmoja.

2. MABAO YA KUFUNGA

Kama timu zitalingana pointi na tofauti ya mabao, timu ambayo imefunga idadi kubwa ya mabao itakuwa juu kwenye msimamo wa kundi husika. Utaratibu huo ulizinufaisha timu nne kwenye fainali za Kombe la Dunia, hasa ile ya Italia iliyokwenda kubeba ubingwa wa dunia 1982 baada ya kuwaengua Cameroon kwa kuwa wao walifunga bao moja pungufu ya mabao iliyokuwa imefunga Italia.

Awali nyingine ilitokea Marekani ‘94, ambao mabao ya kufunga yalizitofautisha Mexico, Jamhuri ya Ireland, Italia na Norway wakati zote zilipomaliza na pointi nne na idadi sawa ya tofauti ya mabao. Mexico, Ireland na Italia zilifuzu hatua iliyofutia kwenye kipindi hicho cha timu 24.

MATOKEO YA WENYEWE KWA WENYEWE

3. POINTI ZILIZOVUNWA KWENYE MECHI

4. TOFAUTI YA MABAO KWENYE MECHI

5. MABAO YALIFUNGWA KWENYE MECHI

Kigezo hiki hakijawahi kutumika kwenye fainali za Kombe la Dunia ili kupata timu ya kusonga hatua inayofuata kutokea kwenye makundi. Mwaka 1978, Scotland ilitupwa nje kwenye hatua ya makundi baada ya kushindwa kwa tofauti ya mabao dhidi ya Uholanzi, ambayo ilikwenda na kufika fainali. Kama Fifa ingetumia kigezo cha matokeo baina ya timu hizo mbili zilipokutana zenyewe, basi ni Scotland ndiyo iliyopaswa kusonga mbele. Kwa bao safi kabisa la juhudi binafsi la mkali Archie Gemmill, Scotland iliichapa Uholanzi 3-2 wakati timu hizo zilipokuatana kwenye mechi ya mwisho ya Kundi 4.

FAIR PLAY

6. POINTI NYINGI ZA NIDHAMU

Kama timu zitalingana pointi na utaratibu wa tofauti ya mabao, mabao ya kufunga na ile ya matokeo ya wenyewe kwa wenyeji ukishindwa kutumika, basi Fifa inahamia kwenye kigezo cha fair-play. Kwenye fainali za Kombe la Dunia kila timu imekuwa ikivuna pointi zinazotokana na nidhamu kwenye mchezo, ambapo pointi hizo zinapungua kwa idadi ya kadi itakayonyeshwa timu husika.

Pointi moja inapungua kwa kila kadi ya njano na pointi mbili kwa kadi nyekundu inayotokana na kadi mbili za njano na pointi nne kama kadi nyekundu iliyoonyeshwa ni ya moja kwa moja. Hivyo, timu ambayo imepata kadi chache za njano na nyekundu ikitokea imelingana pointi na timu nyingine yenye kadi nyingi za njano na nyekundu, basi yenye kadi chache inasonga mbele.

Kanuni hii ilitumika mara moja kwenye fainali za Kombe la Dunia, Russia 2018, wakati Japan ilipsonga mbele kwenye hatua ya 16 bora mbele ya Senegal kutokana na kuwa na -4 ya pointi za fair play dhidi ya -6 ya pointi ilizokuwa nazo Simba wa Teranga.

MWISHO...

7. BAHATI, KURUSHA SARAFU

Kama vigezo vyote hivyo sita vya juu vya kutofautisha timu zilizolingana pointi vikishindwa kufanya kazi, basi chaguo la mwisho la Fifa ni bahati nasibu ya kurusha sarafu. Katika utaratibu huu hakuna timu iliyowahi kutupwa nje fainali za Kombe la Dunia. Mwaka 1990, Uholanzi na Jamhuri ya Ireland zote zilifuzu Kundi F, baada ya zoezi la kurusha sarafu ili kujua ni timu gani ilipaswa kuongoza kundi na ipi ilipaswa kuwa ya pili baada ya kuwa na pointi sawa.

Hiyo iliyokea pia 1970 wakati Urusi na Mexico zilimaliza zikiwa na pointi sawa na tofauti sawa ya mabao, ambapo kwa kipindi hicho, kigezo cha mabao ya kufunga na matokeo ya ana kwa ana timu hizo zilipokutana zenyewe vilikuwa bado havitumiki kuzitofautisha timu zinapolingana kwa pointi.

Columnist: Mwanaspoti