Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Isingefikirika Onana katika mikono ya Sir Alex Ferguson

Andre Onana.jpeg Andre Onana

Sun, 23 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sir Alex Ferguson Waingereza walimuita ‘Red Nose’. Akiwa ana hasira pua inakuwa nyekundu. Big G zinateketea mdomoni mwake. Popote alipo atakuwa amechanganyikiwa. Namna ambavyo dunia inakwenda kasi kuliko hali halisi.

Miaka 10 sasa tangu aachane na Manchester United karibu kila kitu kinabadilika. Mpira umekwenda kasi. Klabu yake imekwenda kasi. Sir Alex hakuwahi kuwapenda sana wachezaji Waafrika. Sikiliza, wachezaji wa Waafrika sio wachezaji weusi.

Kisa? Alichukia namna ambavyo michuano ya mataifa ya Afrika ilikuwa inafanyika Januari. Makocha wa klabu za wazungu wanapata shida pale wachezaji muhimu kutoka Afrika wanapokwenda kuwakilisha mataifa katika dirisha la Januari, huku Ligi zinaendelea. Sir Alex alichukia.

Sidhani kama Sir Alex angemsajili kijana huyu mwenye futi 6’3 kwenda katika lango lake Old Trafford. Labda nyakati zingemlazimisha. Lakini miaka 10 baadaye, kocha anayeitwa Erik Ten Hag amelazimika kumsajili kipa wa kimataifa wa Cameroon, Andre Onana kukaa katika lango la Manchester United. Nyakati zimekwenda wapi?

Onana anakuwa kipa wa kwanza Mwafrika kudakia Manchester United. Fahari iliyoje kwetu!. Kuna kipa wa zamani wa Manchester United, Gary Bailey, huyu alizaliwa Ipswich pale England, lakini akakuliza Afrika Kusini kwa wazazi wake. Aliwahi kucheza timu za Afrika Kusini akiwa mdogo kisha akaibukia Manchester aliyoichezea kuanzia mwaka 1978 mpaka 1987.

Huyu hatuwezi kusema Mwafrika. Mwafrika haswa ni huyu Onana. Akizaliwa kutoka katika kitongoji cha vumbi cha Nkol Ngok pale Cameroon kisha akasota katika vumbi na kuibukia katika Shule ya soka ya Samuel Eto’o pale pale Cameroon na hatimaye akampeleka katika shule ya soka ya Barcelona. Huyu ni Mwafrika haswa.

Baadaye akaenda zake Ajax kabla hajasimama katika lango la wakubwa la Barcelona. Kisha akaenda Inter Milan ambako alikomaa zaidi. Na sasa anaibukia Manchester United akiwa kipa wa kwanza Mwafrika kufanya hivyo. Nyakati zimekwenda wapi?

Kuna mambo mawili hapa. Kwanza amemng’oa katika lango kipa wa mwisho wa Manchester United kusajiliwa na Sir Alex, David de Gea. Lakini De Gea pia ni mchezaji wa mwisho kusajiliwa na Manchester United katika kikosi hiki cha sasa cha United. Umewahi kufikiria kwanini Ten Hag amemchukua Onana? Nadhani Sir Alex angechukia zaidi. Yeye alimchukua De Gea kutokana na uhodari wake wa kupangua michomo ya wapinzani. Lakini Ten Hag amemchukua kutokana na uhodari wake wa namna anavyoitumia miguu yake vizuri zaidi.

Niliandika hapa majuzi namna ambavyo De Gea amesalitiwa na miguu yake. Sir Alex pua yake ingekuwa nyekundu zaidi kwa sababu mbili. Kwanza katika dunia ya leo angelazimika kumnunua kipa anayetumia miguu yake vizuri zaidi, lakini kipa huyo angekuwa anatoka Afrika bila ya kujali kwamba kila baada ya miaka miwili kunakuwa na michuano ya Mataifa ya Afrika.

Hili linaleta kitu kingine ambacho unalazimika kumpongeza zaidi Onana. Kuna nafasi mbili ambazo Wazungu hawaamini kama Mwafrika anaweza kuzitendea haki katika soka la kiwango cha juu duniani. Chunguza. Ni eneo la kipa na kiungo mshambuliaji.

Kuna mastaa wengi wa Afrika wameaminiwa kuwa mabeki wa pembeni, mabeki wa kati, viungo wakabaji, mawinga pamoja na washambuliaji. Eneo lile wanalocheza kina Mesut Ozil, Cesc Fabregas, Bruno Fernandes huwa halitolewi kiurahisi kwa wachezaji kutoka Afrika.

Wanaamini kwamba miongoni mwa akili kubwa katika mpira inabidi zikae hapo. Wanaamini hivyo hivyo katika lango. Hawaamini kwamba mtoto aliyepigwa na vumbi Temeke anaweza kukaa lango lao kiurahisi. Ukiona kipa kama Edouard Mendy anaaminiwa kukaa katika lango huku akiitwa Mwafrika fikiria mara mbili. Sio kweli. Alizaliwa Ufaransa.

Lakini haishangazi sana kwa Onana. Katika Afrika anatoka katika nchi ya makipa. Cameroon ndio nchi ya Afrika ambayo imewahi kutoa makipa bora zaidi waliowahi kutamba Ulaya enzi hizo. Kwa vijana wa sasa hawawezi kuelewa zaidi.

Kulikuwa na Thomas Nkono. Mmoja kati ya makipa bora kuwahi kutokea Afrika. Kipa mahiri wa Italia, Gigi Buffon alimpa mwanae jina la Thomas kwa sababu ya Thomas Nkono. Mwaka 1990 wakati Cameroon ilipokuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika robo fainali za Kombe la Dunia pale Italia, Buffon ambaye alikuwa kijana mdogo muokota mipira alikoshwa na uwezo wa Nkono kiasi akavutika kuwa kipa. Alipopata mtoto wa kiume akamuita Thomas kwa sababu ya Nkono.

Wakati huo Nkono alikuwa akicheza katika klabu ya Espanyol ambayo ni wapinzani wakubwa wa Barcelona. Baadaye akaenda kuzurura kwingine. Lakini achilia mbali Nkono kuliwahi kuwa na Joseph-Antoine Bell. Huyu Bell bada ya kuanzia Afrika akenda kuzurura katika klabu za Marseille, Toulon, Bordeaux na Saint-Etiene zote za Ufaransa. Ni wapi unampata kipa wa Afrika aliyezurura sana katika zama hizo hadi sasa? Inatokea kwa nadra.

Wacameroon pia waliwahi kutulea kipa aliyeitwa, Jacques Sang’oo ambaye katika ubora wake alitamba na Toulon, Le Mans, Metz na Deportivo la Coruna. Hawa ndio Wacameroon katika ubora wao wanapoamua kukaa langoni.

Ghafla namna hii umemsahau Idris Kameni? Wengi wanamkumbuka huyu kwa sababu ni wa zama hizi. Hadi sasa hivi anacheza katika klabu ya Sant Coloma ya Andorra. Ubora wake umeshuka kwa sasa, lakini akiwa katika ubora wake alitamba zaidi Hispania akiwa ameanzia Ufaransa.

Kameni alianzia Ufaransa kukipiga na Le Havre kisha Saint Ettiene. Lakini akaibukia Hispania ambako kwa muda mrefu alitamba na Espanyol kisha Malaga. Amecheza katika hizi timu mbili kwa kipindi cha miaka 13. Baadaye akaenda kumalizia soka la kiwango cha juu kwa Waturuki pale Fenerbahce.

Na sasa mkononi kwetu kuna Onana. Pengine kuliko makipa wengine wote wa Cameroon au tuseme Afrika kwa ujumla huyu anakwenda kucheza katika timu kubwa zaidi, Manchester United. Na zaidi ya kila kitu anakwenda kucheza soka la kisasa zaidi. Soka la kipa kutumia vizuri zaidi miguu yake pengine kuliko mikono.

Ni fahari kwa Afrika kutoa kipa wa namna hii katika zama hizi. Hatujui kama kina Sir Alex kama wangebadilika katika zama hizi na kuanza kucheza soka la Pep Guardiola. haikufikirika kama mtu kama Onana angeweza kukaa katika lango la Sir Alex katika zama zozote zile na kuwa kipa wa kwanza. Tusubiri.

Columnist: Mwanaspoti