Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ishu za rushwa kwa waamuzi na mbinu husika - 6

Waamuzi Againa Ishu za rushwa kwa waamuzi na mbinu husika - 6

Tue, 10 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mfululizo wa Ripoti Maalumu ya waamuzi Bongo jana tuliona na changamoto za usalama kwao na ishu nzima ya maadili yao kwa ujumla, huku mabosi wa Chama cha Waamuzi (FRAT) na Kamati ya Waamuzi ya TFFn wakifunguka.

Leo tunamalizia ishu ya maadili na kugusia tuhuma za rushwa wanazopewa waamuzi kama zina ukweli wowote, kwani jana vipengele hivyo vilikwamba kuingia kwa sababu ya kiufundi.

Ebu endelea nayo na kuona mambo mbalimbali wanayokumbana na waamuzi hao wa soka nchini na jinsi wakati mwingine zimewabebesha lawama zisizowahusu.

MAADILI YAO YAKOJE?

Nkongo anasema maadili ya waamuzi hayatofautiani sana na watendaji wengine, akifafanua hiyo ni kazi kama zilivyo kazi nyingine na zina miiko yake. Kauli ya Nkongo inakolezwa na katibu mkuu wa Chama cha waamuzi (FRAT), Charles Ndagala ambaye anasema maadili kwa waamuzi ni jambo la kwanza wanaloambiwa kabla hata ya kuanza mafunzo.

"Wapo ambao tuliwatimua kwa kukosa maadili, siwezi kuwataja kwa majina lakini walikuwa ni walevi kupindukia, hivyo waliondolewa kwenye orodha ya waamuzi nchini," anasema.

Anasema katika suala la maadili, cha kwanza anapofundishwa ni kutakiwa kuwa kioo cha jamii na mfano wa kuigwa kuanzia nyumbani, mtaani na anapoingia uwanjani. "Hii inajumuisha pia mavazi yake, anavyotembea, lugha na masuala mengine, aonekane mtu mwema mwenye maadili, pia anakanywa kuhusu rushwa, ushabiki wa timu na kuwa kwenye magenge yanayobishania mpira."

RUSHWA NA WAAMUZI

Wapo waliokiri kushawishiwa kuchukua rushwa, wapo ambao walipokea lakini wanasema hawakujua kuwa hayo ni mazingira ya rushwa na wengi wa waamuzi wanakiri kwenye soka nchini, rushwa haiepukiki, hivyo ni akili kichwani kwa mwamuzi aliyekutana nayo.

Mmoja wa waamuzi aliyeomba hifadhi ya jina anasema japo linafanyika kwa usiri mkubwa, lakini wengi wao wanapelekewa rushwa na uamuzi wa mhusika mwenyewe kusimamia sheria za soka au kuamua kuingia kwenye tamaa.

“Nimeshawahi kukutana na suala hilo, nakumbuka nilikuwa naenda kuchezesha mechi mkoani, moja kati ya timu kubwa zilikuwa zinaenda kucheza huko, siku moja kabla ya safari nililetewa tiketi ya ndege sikujua imetoka wapi ila imekamilika kila kitu kikinihusu mimi,” anasema na kuongeza;

“Sikusita kupokea kwani sikujua imetoka wapi siku ya safari ilipofika nilianza safari na baada ya kutua mkoa husika nilipokelewa na watu pia nisiowajua na kupelekwa hotelini, nilikuwa na ulinzi mkubwa bila kuelewa imekuwaje kila kitu nilihudumiwa na ulizi nilipewa,” anasema.

MBINU KALI

Mwamuzi huyo anasema usiku mkubwa alitembelewa na watu wakubwa ambao walimweleza kila kitu kilivyokuwa na kubaini kumbe ni timu fulani ilikuwa inamhudumia na kuamua kufanya mazungumzo nao wakimtaka kuwasaidia timu yao iweze kupata matokeo huku wakiwa na fungu lingine la pesa mkononi.

Anasema makubaliano hayakuenda kama walivyopanga, kwani hakukubali kupokea kitita cha pesa na kuwaambia atatafsiri sheria za soka hawezi kufanya kinyume na hilo.

“Baada ya kuondoka na kuniacha nipumzike usiku ulikuwa mrefu kwangu, kwani nilikesha naomba Mungu asimame na mimi mambo yaweze kwenda kama yanavyotakiwa kwani soka ukikosea kidogo hasa kwa watu ambao ni tofauti na wao ndipo unapoingia kwenye sakata la kuchukua rushwa kwa wapinzani na kukataa upande mwingine bila kujua kuwa na sisi ni binadamu tuna mapungufu.”

Mwamuzi mwingine anasema; “Matukio ya rushwa sio kwa waamuzi tu kila sehemu yapo hata kwa wachezaji wenyewe wanatumika, lakini waamuzi ndio tumekuwa tukitajwa zaidi kutokana na matukio ambayo yamekuwa yakionekana japo kuna ubinadamu lakini tunatajwa kupewa bahasha.”

Anasema kupokea au kutokupokea hakuwezi kutafsiriwa kwa wazi kwa sababu mchezo wa soka una makosa si kwa wachezaji pekee na kukiri hata wao wanateleza na baadaye wanachukuliwa tofauti.

“Nimeshawahi kupokea rushwa, lakini kilichotokea uwanjani kilikuwa tofauti kwani nilichezesha kwa kufuata sheria za soka, kikubwa ninachoshukuru waliotoa pesa siku hiyo walipata matokeo bila ya mimi kupindisha sheria yoyote,” anasema mwamuzi huyo aliyekataa kutajwa jina na kuongeza;

“Nilifanya hivyo kwa ujasiri mkubwa kwani niliamini hata ikiwa tofauti siwezi kufikishwa popote kwa sababu ushahidi wa hilo haukuwepo, pia sikujali vitisho kwa vile najiamini na niliamini lolote likitokea naweza kusimama bila shaka, pia sikuwafuata wala kuomba chochote kwao, ila ni wao ndio walinifuata na kunipa pesa.”

WAAMUZI KIMATAIFA

“Sio kweli waamuzi wa sasa hawawiki Kimataifa, ndani ya miaka mitato ya hivi karibuni Tanzania imepata nafasi ya kuwakilishwa na waamuzi wake kwenye mashindano ya Kimataifa,” anasema na kuongeza;

“Nakumbuka mara ya mwisho mwaka 1976, Hafidh Ally ndio aliiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Afcon akiwa mwamuzi baada ya hapo haijawahi kutokea tena hadi 2017 sasa ukiniambia zamani walikuwa wanawika unipe na data kitu ambacho hakipo,” anasema.

Mwamuzi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwenye gazeti alisisitiza miaka ya sasa waamuzi wameongeza ubora na wamekuwa wakipata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa.

“Mfano mzuri ni Frank Komba ameibeba nchi mara kadhaa, Islael Mkongo mwaka 2011 aliibeba Tanzania, Jonesia pia kachezesha mechi za kimataifa, shida hatutaki kusifia vya kwetu kutokana na makosa ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwenye ligi,” anasema.

Columnist: Mwanaspoti