Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Inawezekana Victor Costa alicheza kabla ya muda wake

Victor Costa Inawezekana Victor Costa alicheza kabla ya muda wake

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nilikuwa nawaza. Labda huu ndio ungekuwa wakati mwafaka kwa Victor Costa ‘Nyumba‚‘ kucheza soka. Labda nyakati zingerudi nyuma halafu Costa angecheza nyakati hizi. Kwa sasa ndio muda ambao labda ungemfaa zaidi.

Katika pambano la Taifa Stars dhidi ya Msumbiji pale Uwanja wa Machava jijini Maputo, waandishi wa habari wa Msumbiji walikuwa wanalishangaa jina la Victor Costa. Ni jina ambalo limekaa Kibrazil au Kimsumbiji. Kina Victor Costa wengi wanapatikana Msumbiji, Ureno, Brazil na Angola.

Baada ya pambano kuanza mmoja wao alinifuata na kuniuliza kama nilikuwa na uhakika kuwa Victor Costa hakuwa mtu wao. Nilicheka. Ni kwa sababu mambo mengi ambayo alikuwa anayafanya uwanjani yalitofautiana na wachezaji wa Taifa Stars.

Taifa Stars ilipigwa presha kubwa lakini Costa alibakia kuwa yule yule. Alitulia na kumiliki mpira vema, alipiga chenga kuanzia nyuma, lakini zaidi ni hamu yake ya kuona timu inacheza kuanzia nyuma. Miaka mingi imepita lakini kwa sasa nimeanza kuhisi kwamba labda Costa alikuwa mbele ya muda.

Kocha anayeitwa Pep Guardiola amekuja duniani kutubadilishia mpira. Ni yeye ndiye muasisi wa kutaka timu icheze kuanzia nyuma. Anataka kipa awe na umiliki mkubwa wa miguu yake. Anataka walinzi wake wawe na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kucheza kandanda kuanzia chini, kisha mpira uende katikati halafu ndio uende mbele.

Nawafahamu walinzi ambao wangeshindwa kazi hii ndani na nje ya Tanzania. Nawafahamu wachezaji ambao wasingekuwa ‘wachezaji wa Pep Guardiola’. Mmoja wapo ni marahemu, Salum Kabunda. Asingeweza kuwa mchezaji wa Guardiola. Kule nje pale Arsenal nina mlinzi wangu, Sol Campbell asingeweza kuwa mchezaji wa Pep Guardiola.

Lakini hapa nchini, Costa alikuwa mchezaji wa Pep Guardiola. Kuna kila dalili kwamba alicheza mbele ya muda wake. Kuna wachezaji wengi wa zamani wangeweza kucheza nyakati hizi. Mmojawapo ni marehemu Method Mogella. Lakini kama tunazungumzia wachezaji waliong’ara na kuacha soka miaka ya 2000 basi Victor ndiye alikuwa mchezaji wa Guardiola hasa.

Victor angeweza kuanzishiwa mpira na kipa, akampunguza mshambuliaji mmoja na kuuacha mpira kwa mchezaji aliye mbele yake huku akifungua nafasi tena. Katika presha ya mpira mrefu uliopigwa nyuma yake huku akifukuzana na mshambuliaji mmoja, Victor angeweza kuukata mwili wake kwa ustadi na kumuacha mshambuliaji akienda kulia huku yeye akienda kushoto. Na baada ya hapo angepiga pasi kwenda kwa Suleiman Matola na sio kubutua.

Haya yote yalikuwa yakifanyika katika viwanja vya kawaida. Lakini kama Victor angecheza sasa hivi ina maana kwamba angekuwa katika raha zaidi kuliko zamani. Zamani kulikuwa na viwanja vichache vilivyokuwa katika hali nzuri. Uwanja wa Taifa na Uwanja wa CCM Kirumba.

Zama hizi kuna viwanja ambavyo ni uhakika kwa timu kucheza vema kuanzia nyuma bila ya hofu. Uwanja wa Ben Mkapa, uwanja wa zamani wa Taifa, Uwanja wa Azam Complex, uwanja wa Kaitaba pale Kagera. Na bado Bodi ya Ligi imehakikisha baadhi ya viwanja vingine vina nyasi nzuri.

Lakini pia Costa angepata wakati mzuri wa kucheza nyakati kama hizi kwa sababu watu wengi washafahamu kile alichokuwa anajaribu kukifanya. Zamani tulikuwa hatumuamini yeye wala wachezaji wengine waliokuwa wanajaribu kucheza kuanzia nyuma. Kwanza tulikuwa hatuamini akili zao, lakini pia tulikuwa hatuviamini viwanja vyetu. Muda mwingi tulipenda wabutue ili mpira ukaangukie mbele ambapo ni eneo salama zaidi mbali na golikipa.

Leo watu wengi wamegundua kwamba ni rahisi kwa mpira kufika mbele kama mkipasiana kutokea nyuma kuliko kubutua kama walinzi wa zamani walivyokuwa wanafanya. Ina maana kwamba Costa alicheza mbele ya muda na leo wala tusingekuwa na hofu na kile ambacho alikuwa anakifanya uwanjani.

Baadaye Victor alipata nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Maritzburg ya Afrika Kusini lakini watu wake wa karibu wananiambia kwamba alitoroka zake na kurudi nyumbani. Kisa? Alikuwa anaumwa ule ugonjwa wa kupenda nyumbani (Home sickness).

Alikuwa anaumwa ule ugonjwa ambao unawasumbua wachezaji wengi wa nchi hii. Jamaa walimkubali lakini akili yake ilikuwa nyumbani. Labda kwa sababu nyumbani alikuwa anaimbwa zaidi. Labda kwa sababu nyumbani alikuwa anapata pesa nyingi za pembeni tofauti na nchi za watu ambapo watu huwa wanaishi kwa mishahara yao tu.

Leo si ajabu Victor angeendelea kucheza nje. Kuna wachezaji ambao wamewafundisha Watanzania namna ya kuishi ughaibuni na kusaka maisha. Ni wachezaji ambao tuwashukuru kwa namna moja au nyingine kwamba wamekuwa wakiwatia tamaa vijana wengi waende kucheza soka la kulipwa ya mipaka yetu.

Kuna Mbwana Samatta, kuna Thomas Ulimwengu, Kuna Simon Msuva, kuna Kelvin John, kuna Novatus Dismas na wachache wengine. Labda Costa angeishi katika nyakati hizi angeweza kuingiwa wivu na mafanikio ya wenzake wanaocheza nje na angeweza kukaa nje kwa muda mrefu.

Hili nalo ni jambo ambalo naamini kwamba alicheza soka kabla ya muda wake. Kwa kile ambacho alikuwa anakionyesha uwanjani huku utandawazi wake ukiwa haujaenea si ajabu angepata timu nzuri kuliko aliyokwenda, na si ajabu angedumu nje kwa muda mrefu zaidi kama ambavyo kina Samatta wamefanya.

Nimekutana na wachezaji wengi wa zamani ambao walijaribu bahati zao kucheza nje lakini wakarudi ndani ya muda mfupi tu. Wengi wananiambia kwamba wanajuta na kwamba sababu walizotoa wakati ule wakirudi zilikuwa za uongo tu kwa ajili ya kuhalalisha kurudi kwao ili wasionekane wajinga.

Sio wao tu, kuna wale ambao walikuwa wametafutiwa nafasi ya kwenda kucheza nje lakini wakapiga chenga ili waendelee kucheza mpira wa uwanja wa Taifa. Wengi wanajuta na wanaamini hawakufanya uamuzi sahihi.

Ukiwaangalia walinzi wetu wengi wa sasa, Costa angeweza kufika mbali zaidi kwa aina yake ya soka.

Columnist: www.tanzaniaweb.live