Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ibrahim Ajibu ameongeza nguvu Congo?

99178 Ajibu+pic Wachezaji wa Yanga,Mukoko Tonombe (Kushoto) na Tuisila Kisinda

Wed, 11 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Rafiki yangu mmoja aliniuliza kwanini Yanga imekimbilia kusajili wachezaji kutoka DR Congo? Jibu langu lilikuwa rahisi tu, kwamba wachezaji wa Taifa hilo wameongeza kitu kikubwa katika miili yao. Kipaji ni kile kile tu.

Wakongo wamejaa pale Yanga. Mpaka kufikia kufungwa kwa dirisha la uhamisho nadhani wanaweza kufika sita. Wananikumbusha wakati ule Barcelona ilipokuwa ikitawaliwa na wachezaji kutoka Uholanzi. Huwa inatokea.

Kwa sasa Yanga ina Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Mayele, Herietier Makambo, anakuja Djuma Shaaban, lakini pia wapo mbioni kumnasa mlinzi wa nguvu kutoka DR Congo kutoka Morocco, Yannick Bangala Litombo.

Inavyoonekana kila Yanga wanapojaribu kusaka mchezaji kisha wakaenda katika video zake huwa wanashawishika zaidi. Hauwezi kuwalaumu sana kwa hiki wanachokifanya kwa sababu wamepewa kichwa na wachezaji wetu.

Wachezaji kutoka DR Congo wana maarifa uwanjani. Kifupi ni kwamba wana vipaji. Lakini hata sisi si tuna vipaji? Ndio, tena vikubwa. Wachezaji karibu wote wa Tanzania wana vipaji. Tofauti ni kwamba juu ya vipaji vya wachezaji wetu Wakongo wao wameongeza matumizi ya nguvu. Ni kitu ambacho kitawatofautisha wachezaji wetu na wale wa nje kwa muda mrefu. Sijui tunakosea wapi lakini ukweli ni kwamba licha ya ubishoo wao nje ya uwanja lakini wachezaji wa DR Congo wana matumizi makubwa ya nguvu na wanapania wanapocheza soka. Congo haina wachezaji legelege.

Nje ya uwanja wachezaji wa DR Congo ni mabishoo. Wanapenda kuvaa hereni, kusuka nywele, kuongeza rangi katika miili yao na mengineyo. Wakiingia uwanjani wanapiga kazi kuliko wachezaji wetu ambao wengi wao ni legelege. Sielewi tatizo linaanzia wapi. Ndivyo tulivyozaliwa? Hapana. Zamani tulikuwa na kizazi cha kina Athuman China na wengineo. Walikuwa wana vipaji vikubwa vya mpira lakini matumizi yao ya nguvu pia yalikuwa juu.

Leo wachezaji wenye matumizi ya nguvu nchini wamepotea. Wengi wamebakiza vipaji tu. Zamani hawa kina Hussein Masha walikuwa mabishoo lakini daima walicheza soka la shoka ambalo leo ndilo ambalo limehamia kwa Wakongo.

Nimechunguza kwa muda mrefu na kugundua kwamba kinachowatofautisha wachezaji wa Tanzania na nchi nyingine sio vipaji. Kinachowatofautisha ni ni nguvu, stamina, mnyumbuliko na mambo mengineyo.

Akili ya kufikiria inabakia kuwa ileile lakini kikubwa kinachokwenda tofauti ni matumizi ya vitu hivi vichache. Lakini hapahapa tufungue mjadala pia kuhusu maumbo ya wachezaji wetu. Mbona siku hizi wana maumbo madogo tofauti na zamani? Hili ni swali jingine. Nilikuwa namtazama Khalid Aucho katika picha. Moja kwa moja kitakachomtofautisha na wachezaji wenzake ni umbile lake. Hawazaliwi tena wachezaji kama hawa nchini. Marcio Maximo aliamua kulazimisha kuwa na wachezaji wenye maumbile makubwa hata kama hawana akili kubwa ya mpira.

Nimepitia video za wachezaji wa DR Congo wa Yanga na wote wanaonekana kuwa ‘tough’. Basi. Haitashangaza kama siku moja kikosi chote cha kwanza cha Yanga kitatoka DR Congo kama wakiendelea kuangalia sifa hizi mbili za mchezaji aliyekamilika.

Haijaanza katika dirisha hili la uhamisho. Kabla ya kina Mukoko alikuwepo hapa Papy Tshishimbi na mara zote alionekana kuwa mgumu kuliko viungo wengine wa Yanga. Nje ya uwanja alionekana kuwa mlaini tu na mwenye kujipenda zaidi kimavazi.

Wachezaji wa Tanzania wasijivunie vipaji tu. wajaribu kuendana na soka la kisasa ambalo lina mahitaji makubwa ya nguvu. Kule nje unamkuta mchezaji kama Fey Toto halafu ana nguvu kama za Mukoko. Shughuli huwa inaanzia hapo.

Hapo DR Congo unamkuta mchezaji ana kipaji kama cha Ibrahim Ajib au nusu tu ya Ajib, lakini matumizi yake ya nguvu ni kama ya Mukoko. Haishangazi kuona klabu zao TP Mazembe na AS Vita licha ya kuwa na wageni wachache lakini zimefanya vizuri katika michuano ya kimataifa kwa sababu ya kuwa na wachezaji imara wa nyumbani wenye utimamu na kiakili.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz