Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

I Can, I Must, I Will: Kitabu kilichokonga nyoyo

MENGI I CAN.png I Can, I Must, I Will: Kitabu kilichokonga nyoyo

Fri, 1 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

ALIPOANDIKA kitabu cha maisha yake, Dk. Reginald Mengi hakuwa na habari kuwa kwa upande mmoja alikuwa anawausia vijana na hata baadhi ya watu wa kizazi chake na kichofuata, kuhusu siri ya mafanikio yake.

Huwezi kusema kuwa alitoa siri zote za mafanikio yake katika kitabu cha ‘I Can, I Must, I Will,’ lakini kimsingi alidhihirisha kuwa dhamira ni jambo la msingi sana katika maisha.

Bila dhamira iliyo imara mtu hawezi kusimama kwa muda mrefu katika uelekeo fulani, ayumbishwe na mitikisiko ya hapa na pale, akate tamaa.

Profesa mmoja wa masuala ya kimataifa Chuo Kikuu cha Bordeaux I (sasa marehemu) aliasa katika darasa (wanaita mhadhara) mwisho wa mwaka 1985 kuwa mtu akishafikia umri wa miaka 35 hawezi kubadilika tena.

Ina maana kuwa mwelekeo wa maisha unaandaliwa wakati mtu yuko katika ujana, akishavuka kipindi hicho hawezi tena kuelekezwa njia moja au nyingine, labda iwe ni nidhamu ya woga.

Kujifunza kikamilifu kimsingi kunaendana na kipindi cha ujana, mtu anapojenga msingi wa kimawazo wa kukabili matatizo, hisia ya ufanisi wa kuyatatua.

Watu waliosoma kitabu hicho na kufanya mapitio katika mitandao waliunganishwa na ‘habari’ moja ya msingi, kuwa “this is a powerful account of the story of Africa told through the life of one of its contemporary shapers, Reginald Abraham Mengi of Tanzania.

I Can, I Must, I Will comes at a time when Africa is casting a new vision that is guided largely by the power of entrepreneurship.”

Siyo rahisi kuboresha kilichosemwa hapo, kuwa ni kitabu hasa cha picha na sura ya Afrika katika kipindi cha kujinasua kutoka utegemezi kwa serikali, kuingia hatua ya ujasiriamali kwa sehemu isiyo ndogo ya jamii.

Dk. Mengi alikuwa mfano, siyo tu wa kuigwa ila hata kuiga ni kazi ngumu; ndiyo maana watu wanasoma kutafuta siri za ujasiri huo.

Wasomaji hao wako wa aina mbili, kwa msingi wa mhadhiri huyo wa Ufaransa, wale ambao tayari maisha yao yameshachukua mwelekeo ambao hauwezi kubadilishwa kwa kujifunza hiki au kile, na wale ambao bado wanajifunza.

Wengi wao ndiyo walioko au walikuwa katika vyuo na vyuo vikuu wakati kitabu hicho kinachapishwa mwaka 2018, na kwa sehemu kubwa ndiyo wenye uwezo wa kutafakari ujumbe wake, kupata mbinu za kujijenga kimaisha na kibiashara.

Uelekeo wa mtu kimaisha haujengwi na kitu kimoja ila mchango wa maana unaweza kuelekeza mawazo au akili ya mtu katika uelekeo unaohitajiwa, akichuja yaliyokuwapo awali, abadilike.

Unaweza pia kusema kuwa kitabu hicho kiliendana na jitihada za kupambanua sera zinazofaa katika kustawisha uchumi wa nchi, kati ya mwelekeo wa kidola unaosisitiza ufanisi wa sekta ya umma na usimamizi wa nguvu wa sekta binafsi.

Kwa upande fulani mwelekeo huo unatokana na historia ya Tanzania katika awamu ya kwanza, kuona wafanyabiashara kama wahujumu uchumi.

Hisia hiyo haijamalizika na kwa maisha yake, siyo tu kufaulu ila kuwajali wengine, Dk. Mengi alibadili sura ya mfumo wa soko ikawa ni eneo ambako Waafrika wanaweza, si kuonewa.

Mfano wa Dk. Mengi kama mbunifu na mjasiriamali aliyeangalia na kuona kuna kitu hakipo kwenye soko inabidi kupatikane ulichangamsha hisia za Waafrika kila mahali.

Wakati mmoja (mwaka 2004) aliyekuwa Waziri wa Elimu nchini Zimbabwe, Dk. Jonathan Moyo, aliuambia mhadhara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (ilikuwa ni wakati wa likizo, hapakuwa na wahudhuriaji wengi) kuwa akirudi nyumbani angeandaa ujumbe wa vyombo vya habari vya Zimbabwe na Afrika Kusini kuja Tanzania.

Sababu ni kufika IPP Media na kujionea wenyewe, wathibitishe kuwa ‘kumbe inawezekana’ kwa Waafrika nao kuwa vyombo vikubwa vya habari.

Ukichukulia hisia hiyo kutoka kwa waziri wa Zimbabwe unapata picha ya upana wa kustaajabu na kutaka kujua uwezo huo ulipotokea, na kwa vile bado ni mapema tangu ameondoka kati yetu, ni wazi kuwa kitabu hicho kitaendelea kutafutwa na vijana wa rika la vyuo na vyuo vikuu.

Hata miongoni mwa wajasiriamali wengine waliokuwepo wakati huo, miaka ya 1980 mwishoni, siyo rahisi kupata waliofanikiwa kwa mwelekeo kama wa Dk. Mengi.

Tofauti yake na wengine ni kuwa hakujikita katika fani moja na kuishia hapo ila alithubutu kuingia katika fani tofauti na kimsingi alifaulu kote.

Aliachia kampuni au shughuli idondoke kama hana hamasa nayo tena, iwe ni kwa sababu faida yake inapungua au atumie muda wake kwingine zaidi kwa wakati huo.

Yako maeneo ambayo baadhi ya vijana wa vyuo na vyuo vikuu watakuwa wameanza kujifunza kutoka katika kitabu hicho, na hata ingebidi ‘kujiongeza’ kwa kiasi fulani baada ya kusoma kitabu au kupata picha ya mtiririko wake kimsingi.

Mojawapo ni ulazima wa kujenga rasilimali mtu akiwa bado kijana, wakati ana nguvu zaidi za kufanya kazi na nyakati tofauti anaweza kuwa mshauri katika maeneo tofauti.

Pesa katika maisha haziji kila wakati, lakini zinapotokea katika mazingira haya au yale inabidi zitumike vizuri, si kwa kuweka benki ambako thamani yake hupungua au hisa ambako ongezeko haliji haraka ila ardhi.

Dk. Mengi alitumia ujana wake na kipato chake kama mtaalamu wa uhasibu kuweka msingi wa uwekezaji (tofauti na ujasiriamali wa kawaida) nyakati zilipobadilika uwekezaji ukaanza kuthaminiwa. Ilikuwa ni kujikumbushia alichojifunza awali kwa Mwalimu Nyerere,’it can be done if you play your part.’

Columnist: www.tanzaniaweb.live