Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Huyu Mpole si mpole mjue!

Mpole Pic Huyu Mpole si mpole mjue!

Mon, 6 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara ipo hatua ya lala salama kabla ya kumalizika kwa msimu, huku kwenye orodha ya wafungaji mabao nyota wawili wa timu za Yanga na Geita Gold wakitunishiana misuli.

Fiston Mayele anayekipiga Yanga na George Mpole wa Geita wanaonyeshana ufundi wa kutupia mabao kambani kila mmoja akiwa nayo 14.

Tofauti na Mayele anayepaishwa sana kwenye vyombo vya habari na kufuatiliwa na mashabiki wengi, ukweli ni kwamba Mpole tofauti na jina lake ni balaa kwelikweli akiwabeba nyota wa Kitanzania hadi sasa katika ligi hiyo baada ya Reliants Lusajo wa Namungo kuyumba kidogo.

Achana na mabao yake 14 aliyofunga kwa staili mbalimbali ikiwamo yale ya nje ya 18, mipira ya kutenga, kichwa na penalti, lakini jamaa hata kule kuwatesa mabeki na makipa kumemfanya asiwe mpole tofauti na jina lake na Mwanaspoti linakuchambulia mabao yake kwa kina.

MATATU NJE YA 18

Pazia la mabao ya aina hii alilifungua katika mchezo wa 14 wa ligi kwa kumtungua goli kwa shuti kali kipa wa Polisi Tanzania, Aron Kalambo katika dakika ya 23, kisha akafanya hivyo tena kwenye Uwanja wa Sokoine dhidi ya Mbeya City dakika ya 14. Bao jingine la aina hiyo alilifunga dhidi ya Azam FC dakika ya 26 baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa timu hiyo na kuachia shuti kali lililomuacha goli kipa, Ahmed Salula akiwa hana cha kufanya.

Idadi hiyo ya mabao matatu nje ya boksi inaonyesha kuwa Mpole amefunga mabao mengi zaidi ndani ya 18, ambapo amefunga mabao 11 jambo ambalo linatoa taswira kwamba mshambuliaji huyo ana uwezo mkubwa wa kufika katika eneo la hatari na kuzitumia nafasi anazozipata.

MATATU YA KICHWA

Mabao yote matatu ya kichwa ameyafunga dhidi ya Kagera Sugar ambapo mawili aliyafunga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Geita Gold wakiwa ugenini akipokea krosi ya Amos Kadikilo dakika ya kwanza ya mchezo, huku jingine akifunga dakika ya 35, ilhali la tatu akiwafunga tena Kagera Sugar kwenye mchezo wa mzunguko wa pili dakika 12, baada ya kuunganisha mpira wa kona uliopingwa na Kadikilo.

TISA MGUU WA KULIA

Mpole anaonekana zaidi kuutumia vyema mguu wake wa kulia kwa kufunga mabao tisa kati ya 14 aliyofunga hadi sasa. Licha ya kuutumia zaidi mguu wake wa kulia kwenye kufunga mabao, Mpole ameutumia pia mguu wake wa kushoto ambapo matatu ameyafunga kupitia mguu wa kushoto akizifunga Azam FC, Polisi Tanzania na Mbeya City

FRIIKIKI MOJA

Bao pekee na la kwanza la mpira wa kutenga alilifunga dhidi Polisi Tanzania katika dakika ya 23 baada ya Daniel Lynga kuchezewa rafu nje ya 18, ambapo straika huyo alikwenda kuupiga mpira huo na kufanikiwa kuuvusha kwenye ukuta na kwenda moja kwa moja langoni akitikisa nyavu licha ya Aron Kalambo kufanya jitihada za kuokoa.

PENALTI MBILI

Mpole amezitumia vyema penalti mbili alizopata kufunga bila kukosa hata moja, ambapo ya kwanza aliipata dhidi ya Mbeya Kwanza katika dakika ya 51, iliyotokana na yeye kuchezewa rafu kwenye eneo la hatari na Rolland Msonjo, ilhali nyingine aliipiga dhidi ya Coastal Union katika dakika ya 35 iliyotokana na kuchezewa rafu na Musa Said Athuman

NYUMBANI BALAA

Katika mabao hayo 14, Mpole amefunga mabao 10 kwenye uwanja wa nyumbani jambo linaloonyesha kuwa mshambuliaji huyo anautumia vyema uwanja wa Nyankumbu uliopo mjini Geita ambapo hadi sasa amezifunga Mbeya city, Ruvu Shooting, Mbeya Kwanza, Polisi Tanzania, Coastal Union, Namungo, KMC, Azam FC, Kagera Sugar pamoja na Simba.

UGENINI ANA MANNE

Hadi hivi sasa Mshambuliaji huyo amefunga mabao manne tu ugenini ambapo mawili ya mwanzo aliyafunga kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera dhidi ya Kagera Sugar, huko moja akilifunga kwenye Uwanja wa Sokoine ni Mbeya akiwafunga Mbeya City kisha akaenda kuwafunga Mbeya kwanza kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

TISA KATUPIA KIPINDI CHA KWANZA

Katika mabao aliyofunga mchezaji huyo, tisa katupia kipindi cha kwanza na inaonyesha kuwa Mpole ni mshambuliaji anayeipa timu yake matokeo chanya kwenye ng’we ya kwanza tu ya mchezo ambapo moja ya mabao hayo amelifunga mbele ya Simba kwenye mchezo wa mzunguko wa pili uliopingwa Uwanja wa CCM - Kirumba, Mwanza katika dakika ya 23.

Mengine aliyafunga dhidi ya Kagera Sugar katika dakika kwanza na 35, Polisi Tanzania dakika 23, Coastal Union dakika 35, Mbeya City ya 14, Mbeya Kwanza dakika ya 11 pamoja na Azam FC katika dakika ya 12.

Licha ya idadi hiyo ya mabao aliyofunga kipindi cha kwanza, bado Mpole ameonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao katika vipindi vyote kwani pia amefunga matano katika kipindi cha pili.

WASIKIE WADAU

Akimzungumzia Mpole, Kocha wa Geita Gold, Fred Felix ‘Minziro’ alisema kuna mabadiliko makubwa kwa straika huyo ukilinganisha na misimu kadhaa iliyopita jambo ambalo limefanya utofauti mkubwa wa kiwango chake na kumfanya kuwa na ubunifu mkubwa wa kufunga mabao.

“Alianza kuonyesha dalili za kuwa na ubora na kiwango hiki tangu mwazoni mwa msimu. Napongeza kwa utulivu alionao anapokuwa katika lango la adui jambo ambalo linamfanya kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya uamuzi sahihi na kufunga mabao muhimu,” alisema Minziro.

Naye nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay alisema matokeo mazuri ya kikosi cha Geita Gold yanachagizwa na uwezo lilionao benchi la ufundi la kikosi hicho.

“Uwezo mkubwa wa Mpole umekuwa chachu ya ushindi kwa Geita Gold,” anasema Mayay.

MPOLE HUYU HAPA

Katika mahojiano na Mwanaspoti hivi karibuni, Mpole alikaririwa akisema anapokuwa uwanjani hutanguliza mbele maslahi ya timu kuliko yake, akilenga kuisaidia kupata ushindi.

“Suala la kufunga linakuja, lakini muhimu ni timu ipate ushindi kabla ya lolote,” alisema.

Columnist: Mwanaspoti