Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hongera serikali kutenga fedha kukabili mafuriko

California Wildfire Flash Flooding Hongera serikali kutenga fedha kukabili mafuriko

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMANNE na Alhamisi, Jiji la Dar es Salaam limepata mvua kubwa ambazo zimesababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali za watu na miundombinu mbalimbali, ikiwamo ya barabara.

Mvua iliyonyesha Jumanne kutwa nzima, ilisababisha jiji hilo kubwa la kibiashara nchini, shughuli zake za kijamii na kiuchumi kuathirika vibaya na wananchi kupata adha ya usafiri, lakini kubwa mafuriko katika maeneo mengi kiasi cha kusababisha njia kubwa za jiji kufungwa kwa muda mrefu ili maafa makubwa yasitokee.

Licha ya kuchukuliwa kwa tahadhari hizo, tumeshuhudia maafa ya vifo vya Watanzania zaidi ya wanane kutokana na mvua hizo pamoja na kuharibika kwa miundombinu hasa ya barabara na madaraja kwa baadhi ya maeneo.

Tungependa kutoa pole kwa wananchi ambao wamepatwa na maafa hayo ama kwa kupoteza wapendwa wao au wale ambao wamejeruhiwa na wengine kukosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kuharibiwa na mvua ambayo imeacha madhara makubwa kwa wakazi hao wa jiji na miundombinu tuliyoitaja.

Lakini wakati tukitoa pole hizo kwa wote waliokumbwa na maafa hayo ya mvua, tumefarijika kusikia kuwa serikali imetenga Sh bilioni 32 kwa ajili ya kujenga na kukarabati mitaro katika Jiji la Dar es Salaam ili kuzuia mafuriko.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kawe wilayani Kinondoni katika mikutano ya kampeni juzi kwa nyakati tofauti, Rais John Magufuli alisema serikali yake imetenga Sh bilioni 32 kwa ajili ya kujenga na kukarabati mitaro katika Jiji la Dar es Salaam ili kuzuia mafuriko, na katika hizo amewaahidi watu wa Kawe kuwapatia Sh bilioni tano.

Alisema ahadi hiyo kwa Jimbo la Kawe katika maeneo ya Tegeta, Basihaya hadi Ununio, pia itatekelezwa kwa maeneo mengine ya jiji yakiwamo ya wilaya za Kinondoni kama Mkwajuni na Mto Ng’ombe pamoja na Ilala katika Bonde la Msimbazi kuwa yatajengwa na kukarabatiwa kwa ajili ya kuhakikisha mafuriko yanazuiwa.

Tunapongeza hatua hii ya serikali ya kutenga fedha hizo kwa ajili ya kukabili mafuriko kutokana na ukweli kuwa mvua zimekuwa zikisababisha maafa makubwa kwa wakazi wa jiji na miundombinu yake kwa ujumla.

Hatua hii ya kujenga na kukarabati maeneo hayo yanayoathiriwa mara kwa mara na mafuriko ni ya kupongezwa na kuungwa mkono, hasa ikizingatiwa kuwa Jiji la Dar es Salaam ni mojawapo ya maeneo nchini ambayo yana mchango mkubwa katika Pato la Taifa kutokana na wingi wake wa watu na shughuli za kiuchumi.

Lakini wakati tukipongeza hatua hiyo ya serikali, ni vema pia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakatunza mazingira kwa kuhakikisha mifereji na mitaro ya maji inakuwa katika hali ya usafi wakati wote kwani moja ya chanzo kikubwa cha mafuriko ni kuziba kwa mifereji na mitaro, na hivyo maji kukosa njia ya kwenda mahali husika hasa baharini.

Kila mkazi wa jiji hilo anapaswa kuwa mlinzi wa kuhakikisha miundombinu inakuwa katika hali nzuri kwa sababu maafa yanapotokea hayabagui na yanamkumba mtu yeyote, hivyo mamlaka za Mkoa wa Dar es Salaam ziwe mstari wa mbele kukemea watu wasiotunza mazingira pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Columnist: habarileo.co.tz