Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hongera Spika Ndugai, tunasubiri Bunge bora

E789be0b0cddd07f34a4238bb589ccbc Hongera Spika Ndugai, tunasubiri Bunge bora

Thu, 12 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BUNGE la 12 juzi lilimchagua Mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, Job Ndugai kuwa Spika wake baada ya ushindi wake mkubwa wa asilimia 99.7 ya kura halali zilizopigwa.

Ndugai ambaye hakuwa na mpinzani katika nafasi hiyo, amewaahidi Watanzania kuwa licha ya Bunge hilo kuwa na wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), halitakuwa la kukubali kila kitu na kukataa kila kitu, bali litakuwa lenye kuleta matokeo chanya na kuwa mfano bora kuliko mabunge mengine tangu Uhuru.

Amesema hilo litakuwa Bunge la kuwajibika vilivyo kwa wabunge hao. Amesema ni kweli kuwa wabunge wengi wanatoka CCM, lakini hilo halimaanishi kuwa Bunge hilo litakuwa la ndiyo, ndiyo, ndiyo wala hapana, hapana, bali anaamini litatekeleza wajibu wake kama ipasavyo.

Awali tunapenda kumpongeza Spika Ndugai kwa ushindi huo wa kishindo ambao tunaamini umetokana na imani kubwa ya chama chake, CCM pia na wabunge wenzake ambao wameridhishwa na kazi nzuri aliyoifanya katika Bunge la 11 ambalo pia alikuwa kiongozi wa mhimili huo wa dola.

Tunaamini imani huzaa imani, hivyo kama alivyoahidi mwenyewe, atakitendea haki kiti hicho alichokabidhiwa kwa maslahi makubwa ya Bunge, serikali na Watanzania kwa ujumla.

Lakini kubwa kama alivyoeleza mwenyewe, Bunge la 12 lina wabunge wengi kutoka CCM, hivyo kuna imani ya kwamba litakuwa Bunge la kukubali kila kitu kitakachowasilishwa mbele yao, lakini tunafarijika kwa kauli ya Spika Ndugai ya kuwa litakuwa Bunge lenye kuwajibika vilivyo kwa wabunge, na Watanzania kwa jumla.

Kwa hiyo wabunge kama alivyowaeleza Spika Ndugai, hawapaswi kuwa ‘mabubu’ wakiona kama ni njia sahihi ya kuisaidia serikali, bali wanapaswa kuishauri, kuisimamia na kuielekeza kwa weledi kwa nia ya kuhakikisha wananchi ambao ndio waliowatuma kuwawakilisha bungeni, wananufaika na kujiletea maendeleo.

Kuwa wabunge wengi wa CCM siyo dhambi, dhambi ni kujivika kofia ya chama na kuacha kuisimamia serikali vizuri katika kuhakikisha yote yaliyoahidiwa na kupangwa na serikali yanatekelezwa. Wabunge wasiende kufanya kazi za serikali ambazo siyo zao, wafanye majukumu yao kwa mujibu wa Katiba.

Tunafarijika kuona kwamba Spika Ndugai na pia Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, wameliona hilo na wamewaeleza wazi wabunge kuwa wanapaswa kuteleleza majukumu yao kikamilifu na mojawapo ni kuwatumikia kikamilifu wananchi waliowapa ushindi wa kishindo katika maeneo yao.

Tunategemea wabunge watazingatia ushauri huo na kwamba kama alivyoahidi kiongozi wao wa Bunge, watachapa kazi kwa weledi, watajituma, watajitolea kwa hali na mali kuwatumikia wananchi waliowatuma, lakini kubwa hawatasahau pia kwenda majimboni mwao kwani ndio baadhi hujisahau na kuyatelekeza majimbo yao.

Tunawatakia kila la heri na waifanye kazi ya kutukuka kwa niaba ya Watanzania wenzao.

Columnist: habarileo.co.tz