Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hongera Samia kwa kubeba mshahara wa Stars

Adel Amrouche Kocha Stars Adel Amrouche, Kocha mpya Taifa Stars

Sat, 11 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), limemtangaza raia wa Algeria na Ubelgiji, Adel Amrouche kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya mpira wa miguu, Taifa Stars, ili kuziba pengo la raia wa Denmark Kim Poulsen aliyebadilishiwa majukumu mwaka uliopita. Hii ni hatua muhimu kwa mpira wa nchi hii.

Pamoja na uteuzi wa kocha mkuu, kilichonivutia zaidi ni uamuzi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua uamuzi wa kulipa mshahara wa kocha aliyeajiriwa na TFF. Huu ni mzigo mkubwa ambao serikali imeamua kulitua shirikisho.

Katika mpira wa miguu huwa tunapenda kusema kuwa serikali haitakiwi kuingilia mchezo huu unaopendwa na umma wa watu duniani. Watu wengi hushindwa kutafsiri maana ya utaratibu huu. Ukweli wake ni kwamba taasisi mbalimbali pamoja na serikali hazipaswi kuingilia utendaji wa kila siku katika uendeshaji wa mpira wa miguu kwani hiyo ni kazi ya vyama vya mpira. Hata hivyo, serikali inao wajibu wa kusimamia maendeleo ya michezo kwani ni sehemu ya ustawi wa raia wake.

Utashi wa kisiasa ni jambo la muhimu sana katika maendeleo ya sekta yotote, Afrika haiwezi kumsahau marehemu Kenneth Kaunda na mapenzi yake kwa mpira wa miguu na hasa timu ya Taifa ya Zambia iliyopewa jina la KK XI (Kenneth Kaunda Eleven).

Mpaka sasa hatua iliyopigwa na taifa hilo katika mpira wa miguu ni matokeo ya utashi wa kisiasa wa Rais Kenneth Kaunda.

Mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete, kupitia ukaribu uliokuwepo kati ya Tanzania na Brazil na zaidi kati yake na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil aliliwezesha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kupata makocha kutoka Brazil wakiwa chini ya Marcio Maximo.

Makocha hao,hasa Maximo, waliamsha hamasa ya mpira wa miguu nchini na mapenzi ya wananchi kwa timu yao ya Taifa ikiwa ni pamoja na kufuzu kucheza michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN). Hata Wabrazil hao, walipoondoka waliletwa makocha kutoka Denmark Jan Borge Poulsen na Kim Paulsen wakiifundisha Taifa Stars kwa vipindi tofauti. Serikali ililipa mishahara yao huku gharama nyingine za kiutendaji zikilipwa na TFF na wadhamini wa Taifa Stars.

Baada ya kuondoka akina Poulsen, serikali si tu kwamba ilijiweka pembeni katika kumlipia kocha mkuu wa timu ya Taifa bali pia ilijivua wajibu wa kodi zilizotakiwa kukatwa makocha ambao iliwalipa mishahara. Nikiwa mtendaji mkuu wa shirikisho,suala hili lilininyong’onyeza sana binafsi na wadau wengine wa mpira wa miguu kwani shirikisho na hata mali zake zilikuwa zinawekwa rehani baada ya serikali kubadili msimamo na kulibambikia shirikisho kodi ilizotakiwa kukata yenyewe na kulipa kwa mamlaka kwani ndiyo ilikuwa inalipa mishahara. Mambo yalikuwa magumu kwani kulipa mishahara ya makocha wa timu za taifa haikuwa kazi ndogo.

Mataifa makubwa katika mpira wa miguu kama Ujerumani, Ufaransa, Hispania ,Argentina, Brazil na mengine huwalipa makocha wa timu zao za Taifa kiwango kikubwa cha mshahara kwani hutafuta walio bora kutetea bendera ya Taifa. Hata mataifa mengine ya kiwango chetu hutafuta makocha wa kiwango cha juu mfano ni majirani zetu Zambia ambao wamemwajiri kocha wa zamani wa Chelsea na timu ya Taifa ya Ghana, Muisraeli Avram Grant. Hili kulitekeleza hilo, shirikisho la mpira wa miguu nchini halina rasilimali za kutosha kufikia malengo hayo.

Kurudi kwa serikali katika kutekeleza wajibu huu wa kumlipa mshahara kocha wa timu ya taifa naiona kama dalili njema na mwendelezo mzuri katika michezo kwa serikali ya awamu ya sita inapotimiza miaka miwili madarakani. Katika makala yangu ya kwanza ya nionavyo mwezi Agosti mwaka jana niliandika:

Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeonyesha mwanga na utashi wa kutosha katika kuleta maendeleo ya michezo,Sanaa, utalii na utamaduni. Pamoja na changamoto zilizopo, bado fursa ya kuwekeza na kufaidika katika sekta hizo ipo wazi labda kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya taifa hili.

Hata leo, bado serikali kwa kiasi kikubwa imeyaishi matumaini na matarajio ya wapenzi wa mpira wa miguu nchini pamoja na kwamba bado kuna changamoto kubwa sana katika maendeleo ya soka la vijana na miundombinu ya mpira wa miguu. Kwa hatua hii,nionavyo inampongeza sana Mama Samia Suluhu

Hassan na Shirikisho la mpira wa miguu. Muhimu ni kocha mpya kupewa mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kusaka vipaji nchini n ahata kutafuta wajukuu zetu wanaocheza mpira katika mataifa mbalimbali duniani ili kuweza kuimarisha Taifa Stars.

Mwandishi wa makala hii ni Afisa Mtendaji mkuu wa Shirika la kijamii la Life Coaching Organisation (Lico) na amewahi kuwa katibu mkuu wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF)

Columnist: Mwanaspoti