Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hongera Namungo mmetoa funzo kwa wengine

1e8e1bfb408b3e2b164b801921f48db9 Hongera Namungo mmetoa funzo kwa wengine

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TIMU ya Soka ya Namungo imefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni mara ya kwanza kwake kushiriki mashindano hayo na kuvuka hatua kubwa.

Unaweza kusema ushiriki wao umekuwa wenye bahati kubwa kutoka hatua za awali hadi ilipofikia lakini kingine, juhudi zao zimechangia kufikia mafanikio.

Kufika hatua ya makundi sio bure bali kuna kiwango cha fedha watanufaika nacho kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa hiyo ni faida kubwa kwao ziwasaidie katika mahitaji yao muhimu ya kiuendeshaji.

Faida nyingine ni kwamba timu hiyo imesaidia kuongeza pointi kwa taifa lakini inaonesha ni jinsi gani Tanzania kuna ligi bora kwa sasa ukilinganisha na miaka iliyopita.

Miaka ya nyuma ilikuwa ni vigumu kuona timu zinaingia hatua ya makundi tena kama ziko mbili zote zicheze michuano yote miwili kwa maana ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kisha zikatinga hatua hiyo, lakini awamu hii Simba na Namungo hakika zimefanya kazi kubwa na zinahitaji pongezi.

Pongezi pia, kwa wachezaji kwa kujitoa sio kwamba Namungo ina kikosi kinachotisha ila ni upambanaji wao na maandalizi mazuri kutoka kwa viongozi wao na wachezaji wamefanya kazi ipasavyo.

Namungo imetoa funzo kwa timu nyingine ambazo zinajiona kuwa haziwezi hata zikichukua Kombe la Shirikisho la Azam (FA) hazitafika popote.

Kulikuwa na dhana imejengeka kuwa labda Yanga na Simba ndio timu zinazostahili kushiriki mashindano makubwa kama hayo na kufanya vizuri na wengine kwasababu wana vikosi vya kawaida hawawezi.

Sasa Namungo imefuta hiyo dhana kwamba inawezekana kwa timu nyingine kushiriki mashindano ya kimataifa na kupeperusha vyema bendera ya taifa.

Kikubwa ni umejipangaje kuanzia wachezaji, benchi la ufundi na maandalizi ya timu husika dhidi ya fitna za kisoka na kisaikolijia dhidi ya wapinzani.

Kwasababu mpira wa Afrika unaongozwa na mambo mengi pamoja na ubora wa kikosi kuna fitna za kisoka zinafahamika, lakini ukienda na dhana ya Simba lazima afe mtu nyumbani na kujipanga ndani na nje ya uwanja yaani kila mtu ashinde kwake basi unafika pazuri.

Msimu wa mwaka juzi Mtibwa iliwakilisha lakini iliishia hatua za awali na kutolewa.

Na wengine watakaopata nafasi baadaye ya uwakilishi wa kimataifa lipo funzo wanahitaji kujifunza kwa hao waliofanikiwa wamefanyaje wakafika walipofika.

Sio mbaya kujifunza kwa wenye mafanikio lengo ni ili kufanya vizuri na kupeperusha vyema bendera ya nchi.

Kwa hatua waliyofikia Namungo wamejitahidi kwa hiyo wakiamua wafike mbali zaidi wanaweza.

Wanachotakiwa kufanya ni kutoogopa majina makubwa yaliyoko katika kundi lao lenye timu kubwa na zenye ushindani.

Kundi la Namungo kuna Raja Casablanca ya Morocco, Nkana ya Zambia na Pyramids ya Misri.

Ili Namungo wafanikiwe wajipange mechi za nyumbani asichomoke yeyote salama, watoe kipigo wakirudi kwao wahadithie.

Kwa mawazo yangu, naamini Namungo ikijipanga inaweza, muhimu ni kuondoa woga, kuwaona inaokutana nao hawana tofauti na wao na kingine kuwaheshimu wapinzani wao kwa kuja na mbinu za kuwamaliza.

Pengine ninyi mnaweza kuonekana ndio timu ndogo na hilo halifichiki katika uzoefu hamlingani na mnaokwenda kukutana nao.

Linapokuja suala la uwanjani, lazima muwe tofauti kuwaonesha watu kuwa hamkubahatisha. Msikubali kutosheka na mlipofikia mnaweza kufika mbali zaidi na kutengeneza historia mpya.

Ingependeza miaka ijayo kuwe na wawakilishi tofauti na wale waliozoeleka na wafanye vizuri kama Namungo ili soka letu liinuke na watu watambue kuna nchi inaitwa Tanzania ina vipaji lukuki.

Columnist: habarileo.co.tz