Yawezekana nina ugonjwa wa kusahau. Labda ubongo wangu umeanza kuvurugwa na zile kemikali za Wazungu tunazokunywa ili kuondoa baridi. Yawezekana lakini.
Ila jambo moja ambalo bado nina uhakika nalo japo nimeishi miaka mingi, akili yangu bado iko sawa sana. Bado nina utashi wa kuona mambo kwa mbali kuliko hawa vijana wadogo Kama Ahmed Ally na Ally Kamwe.
Kuishi kwingi ni kuona mengi. Haya si maneno ya Kinjekitile Ngwale wala Hayati Magufuli. Ni maneno ya wahenga. Lakini tatizo siku hizi watu wanakwenda sana kwa upepo. Wakiambiwa hiki, wanasahau walichofanyiwa jana. Ndio maisha ya Utandawazi.
Wakati wa Ujamaa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere hatukuwa hivi. Watu walifanya vitu mpaka vikakamilika ndipo wakafanya vingine. Ndio sababu wakati ule ilikuwa rahisi kuwahamisha watu kuwapeleka kwenye Vijiji vya Ujamaa. Apumzike kwa amani Baba wa Taifa.
Baada ya kushiba chapati na maharage ya Mbeya leo asubuhi nimejikuta nakumbuka ule mchakato wa mabadiliko wa Yanga. Hivi uliishia wapi? Nimewaza sana.
Yanga walikuja kwa kasi na kuanza mchakato wa mabadiliko kama Simba. Wakatengeneza katiba mpya kwa haraka sana.
Katiba mpya ikaweka utaratibu mpya. Wakaamua kuwa Yanga itakuwa na wawekezaji na wanachama. Asilimia zikagawanywa na kuwekwa kwenye maandishi. Wenye timu yao wakapewa asilimia 51 na 49 zikaachwa kwa wawekezaji. Wakasema hawataki mwekezaji mmoja kama Simba, wao watakuwa na wanne.
Ukatengenezwa mfumo mpya wa uchaguzi. Ikaamuliwa kuwa kwa sasa siyo kila mwanachama ataweza kupiga kura katika Mkutano Mkuu. Ukawekwa uchaguzi wa matawi unaotambulika rasmi na wawakilishi watano wangekwenda katika Mkutano Mkuu.
Huu ndio mfumo uliowaweka kina Hersi Said na wasaidizi wake madarakani pale Yanga. Walifanya uchaguzi kwa Katiba mpya baada ya kupata idhini kwa Msajili. Ilikuwa ni hatua kubwa.
Ulipita muda mrefu tangu Yanga iwe na Katiba mpya. Ilitia moyo sasa kuona wamepiga hatua. Nakumbuka mchakato huu wa mabadiliko ulisimamiwa na Senzo Mazingisa ambaye aliajiriwa na Yanga baada ya kuacha kazi pale Simba.
Senzo aliusimamia mchakato vyema sana pamoja na wasaidizi wake. Kwanini aliondoka kabla mchakato haujakamilika? Inafikirisha sana.
Ni miezi kadhaa imepita sasa tangu Hersi na wenzake wapewe ofisi pale Yanga. Hata hivyo mchakato wa mabadiliko bado umesimama kama sanamu la pale Posta au YMCA pale Moshi. Umesimama su.
Hakuna kitu kipya kimeendelea mpaka leo. Ama ilikuwa geresha tu kwa Yanga kuonekana wanafuata nyayo za Simba? Kwanini Yanga hawajasema chochote mpaka sasa.
Mfumo mpya wa mabadiliko pale Yanga umetoa taratibu za uongozi mpya utakavyokuwa. Umeeleza namna watendaji watakavyofanya kazi. Lakini ili mfumo ufanye kazi vizuri ni lazima pande zote mbili zikamilike.
Kwanini mchakato wa kupata wawekezaji pale Yanga haujaanza? Kuna hofu gani? Kwanini hawataki kusonga mbele.
Wenzao wa Simba walikwenda haraka. Japo mchakato umekwama mwishoni, lakini angalau walifanya na sasa imebaki wao na mamlaka nyingine kulimaliza jambo lao. Kuna kitu gani nyuma ya pazia kwenye mchakato wa mabadiliko pale Yanga? Acha tusubiri na kuona.
Hata hivyo kwa ushamba wa baadhi ya machawa pale Yanga wataanza kusema hizi ni propaganda za wapinzani wao. Inabidi waseme hivyo ili kutetea ugali wao.
Hawawezi kujibu hoja hata siku moja. Wataishia kumsema mtoa hoja. Ndio maana hapo majuzi mwandishi wa habari mmoja alipohoji kuhusu baadhi ya wachezaji waliosajiliwa pale Yanga alishambuliwa kila kona.
Wakamuita majina yote mabaya lakini mpaka leo hoja zake hazijajibiwa. Sitashangaa kuona wakianza kurukaruka kama maharage yanayotaka kuiva katika hoja hii. Ila baada ya yote, watuambie mchakato umefikia wapi?